Wakati mgumu wa kisiasa kwa nchi tatu za Afrika Mashariki

Muktasari:

  • Ukiangalia siasa za nchi hizi, unaweza kujiuliza nchi gani ina nafuu; ni ngumu kujua.

Tunaweza kukieleza kama kipindi cha majaribu makubwa kwa nchi tatu kuu za Afrika Mashariki; Tanzania, Kenya na Uganda. Changamoto za kisiasa ambazo nchi hizi zinapitia zinatishia umoja, amani na maendeleo ya nchi hizo.

Ukiangalia siasa za nchi hizi, unaweza kujiuliza nchi gani ina nafuu; ni ngumu kujua.

Kenya, kunyoa au kusuka?

Pale Kenya, baada ya Mahakama ya Juu nchini Kenya, kufuta uchaguzi wa Agosti 8, kumekuwa na mabishano makali juu ya namna ya kuelekea uchaguzi mpya, huku kila upande ukichukua msimamo mkali.

Upande wa upinzani, chini ya muungano wa ushirika wa Nasa wanataka mabadiliko katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), wakitaja maofisa sita ambao wanadhani hawapaswi kuendelea kushika nyadhifa zao, akiwamo Ofisa Mtendaji Mkuu, Ezra Chiloba na msaidizi wake Betty Nyabuto.

Nasa wanaamini maofisa hao walishiriki katika njama za kuiba kura kumsaidia Rais Uhuru Kenyatta, madai ambayo yamepingwa na chama cha Jubilee cha Kenyatta, ambao nao wakitumia wingi wao bungeni wanataka kubadili sheria kuepusha utata mwingine utakaopelekea kufutwa uchaguzi.

Kwanza, Jubilee wanataka matokeo yatakayojumlishwa kwa makaratasi (manually) yawe ndiyo mamlaka ya mwisho katika utangazaji matokeo na kwamba matokeo yanayotangazwa vituoni ndiyo msingi wa matokeo. Mabadiliko hayo pia yanatoa adhabu kwa maofisa wanaoharibu uchaguzi.

Ukiangalia mapendekezo haya, ni vigumu kuona walakini, lakini wachambuzi wanasema muda ambao mapendekezo haya ya mabadiliko yameletwa, unatia shaka. Ni sawa na kubadili sheria za mchezo wakati mechi ikiendelea.

Yote kwa yote, kipindi ambapo Raila Odinga amejiondoa kwenye uchaguzi, huku maandamano yakiendelea kila wiki ukizingatia nguvu ya ushawsishi wa mwanasiasa huyo nguli na muungano wake wa Nasa, maandamano yao si ya kupuuza. Yanatosha kuitikisa nchi na ikaathirika kiuchumi.

Kwa kawaida siku za maandamano kunakuwa na wizi mwingi na hivyo biashara nyingi hufungwa. Vilevile, wageni wengi wanaotaka kuitembelea Kenya kiutalii huenda wakahofia fujo na kufuta safari zao. Kwa ujumla, ni vigumu uchumi kustawi katika nchi yenye migogoro ya kisiasa.

Maandamano ya upinzani, enzi hizo chini ya muungano wa Cord, yalichangia kuiondoa madarakani tume iliyopita iliyoongozwa na Ahmed Issack Hassan .

Safari hii kama uchaguzi utapita Oktoba 26, hayatakuwa maandamo ya kupinga IEBC tu bali Serikali ambayo kwa wapinzani wataichukulia kama si halali.

Kitisho kikubwa kwa Kenya wakati haya yakiendelea ni hisia za chuki za ukabila zinazojengeka, hususan kati ya makabila mawili makubwa Wakikuyu na Waluo. Kenya ilishaonja machafuko huko nyuma, hivyo wanasiasa wanapaswa kuchukua tahadhari kubwa, ukizingatia kuwa chama tawala na wapinzani wana nguvu karibu sawa na wamegawana maeneo ya ushawishi.

Museveni, rais wa milele?

Tukigeukia Uganda, licha ya umri wake wa miaka 73 na akiwa ametawala zaidi ya miaka 30, Rais, Yoweri Museveni haelekei kutaka kuachia madaraka ifikapo 2021.

Museveni ambaye amekuwa madarakani tangu 1986, ni wa nne katika orodha ya viongozi wa Afrika waliokaa sana madarakani wakiongozwa na Teodoro Obiang Nguema Mbasogo wa Equatorial Guinea (miaka 36), Robert Mugabe wa Zimbabwe (miaka 35) na Paul Biya wa Cameroon (miaka 33).

Vijana walio chini ya miaka ya 30, ambao kwa vyovyote ni zaidi ya asilimia 65 ya Waganda wote, hawajawahi kuishi chini ya utawala mwingine zaidi ya Museveni.

Museveni amewaona marais watano wa Marekani wakipita Ikulu ya nchi hiyo. Aliingia madarakani wakati wa Ronald Reagan, na mpaka sasa wamepita George H.W. Bush (baba), Bill Clinton, George W. Bush (mtoto), Barack Obama na sasa yupo Donald Trump.

Museveni aliingia madarakani mwaka mmoja tu baada ya Tanzania kumchagua Rais wa awamu ya pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi mwka 1985. Mwinyi alistaafu 1995 na baada yake marais wawili wamepita waliotawala miaka 10 kila mmoja na sasa Magufuli katika awamu ya tano.

Ukomo wa utawala wa vipindi viwili uliowekwa kikatiba ulifutwa mwaka 2005 kwa kura ya Bunge na kumuwezesha Museveni kubaki madarakani. Shida inayoikumba Uganda hivi sasa imekuja baada ya Museveni na chama chake cha NRM kuanza jitihada za kuondoa ukomo wa umri wa miaka 75, kikwazo pekee kilichobaki dhidi ya Museveni kuelekea kutawala mpaka afe- akipenda au apoteze uwezo kwa sababu yoyote.

Katika mapambano ya kuzuia pendekezo hilo, ngumi zimepigwa bungeni siku mbili mfululizo na kuifanya nchi hiyo kuingia katika historia ya aina yake. Licha ya upinzani mkali bungeni, Waganda wengi walijitokeza mitaani kuandamana kuonyesha hasira zao dhidi ya hatua ya wabunge wanaomuunga mkono Museveni kutaka kuondoa ukomo wa umri.

Mapambano ya kupigania demokrasia au tuite ya kumuondoa Museveni madarakani yamekuwapo kwa kipindi kirefu. Lakini, wakijua wazi kuwa ni ngumu kumuondoa Museveni kupitia uchaguzi, wapinzani wamekuwa wakitegemea ukomo wa Katiba kuwahakikishia mabadiliko ya uongozi hivi karibuni.

Baada ya ukomo wa vipindi kuondolewa; iwapo ukomo wa umri nao ukiondolewa, hakuna kitakachomzuia Museveni kuendelea kutawala. Wakilijua hilo, inaonekana hakuna jambo ambalo wapinzani na wapenda mabadiliko wengine wataacha kulifanya alimradi wafanikishe kumzuia Museveni.

Kwa mtazamo huo, Katikkro (Waziri Mkuu) wa zamani wa Ufalme wa Buganda, Dan Muliika amenukuliwa hivi karibuni akionya kuwa Museveni anajenga mapinduzi dhidi yake mwenyewe bila kujijua.

“Tumerudi mwanzo. Tuko ‘bize’ tunajenga mapinduzi mengine, kama yale uliyoyaona enzi za Obote (Milton) yalimpelekea kutimuliwa…hata Obote hakuona kuwa anajenga mapinduzi dhidi yake mwenyewe. Hivi ndivyo ianzavyo,” alisema Muliika.

Tanzania na awamu ya tano

Tanzania nayo inapitia kipindi kigumu. Hali ya kisiasa Tanzania inatia wasiwasi. Kwa sasa ajenda kuu ya vyama vya upinzani siyo tena maendeleo bali ni mapambano ya kurejesha haki zao za kisiasa, kudumishwa kwa demokarasia na utawala bora.

Nikiwa Mtanzania,na katika mazingira haya nasita na naogopa kulaumu sana, lakini itoshe kusema kuwa tuna tatizo la msingi. Demokrasia haifanyi kazi kwa namna ile ilivyopaswa kufanya.

Kwa sababu ya kamatakamata nyingi kwa sababu tu ya watu kusema, kuna woga fulani unaimarika miongoni mwa watu. Woga huu unaojengeka ni mbaya kwa sababu demokrasia ni kujenga hoja, kutoa maoni na kukosoa.

Unapojenga hoja, kukosea ni jambo la afya na la kibinadamu. Ilitegemewa kuwa unayebishana naye, yaani asiyekubaliana nawe arekebishe. Hivyo, ni busara kwa Serikali kuongeza kiwango cha uvumilivu wa kauli za ukosoaji.

Mambo mengine mahsusi ambayo yaanalalamikiwa ni vikwazo vingi vya namna ya kufanya mikutano ya kisiasa, kuhaririwa kwa hotuba za wapinzani bungeni, kufungiwa, kufutwa kwa vyombo vya habari, kauli za viongozi zinazotafsiriwa kuwa ni za vitisho dhidi ya usalama wa wapinzani.

Upande wa Serikali nao wanalalamika kuwa wapinzani na baadhi ya vyombo vya habari wamekosa uzalendo, wanatumiwa na watu wenye nia ya kuhujumu nchi, wana fujo, hawaheshimu Serikali, wanakashifu viongozi na wanafanya uchochezi.

Yote niliyoyataja hapo juu, siyo matatizo makubwa. Yanakuwa matatizo makubwa pale tu kunapokosekana namna na jukwaa la kujadiliana, kusikilizana na kufikia maelewano fulani juu ya namna ya kuendesha siasa.

Ubaya ni kwamba haya yanayolalamikiwa ni sheria za mchezo wenyewe wa siasa za demokrasia. Kama sheria hazikubaliki na timu zote shiriki, mashindano haya yatachezwaje?