Wakulima wa vitungu Simanjiro walilia masoko

Muktasari:

Ni eneo linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, lakini kwa sababu ya ukosefu wa mitaji wakulima wengi wanashindwa kumudu gharama za uendeshaji wa kilimo hicho. Lakini hata wanaolima kwa sasa, kila siku wamekuwa wakilia kukabiliwa na changamoto mbalimbali kubwa ikiwa ni kukosa masoko ya uhakika na kupunjwa.

Pamoja na bonde la kilimo cha vitunguu lililopo Tarafa ya Ruvu Remit wilayani Simanjiro kuwa na hekta 10,000 zinazofaa kwa kilimo hicho, kwa sasa hekta zinazolimwa hazivuki 3,000.

Ni eneo linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, lakini kwa sababu ya ukosefu wa mitaji wakulima wengi wanashindwa kumudu gharama za uendeshaji wa kilimo hicho. Lakini hata wanaolima kwa sasa, kila siku wamekuwa wakilia kukabiliwa na changamoto mbalimbali kubwa ikiwa ni kukosa masoko ya uhakika na kupunjwa.

Ni kwa sababu hii, wakulima wa zao hilo katika Kijiji cha Gunge, wanaiomba Serikali kuwapatia utaalamu wa kilimo cha umwagiliaji utakaosaidia kuongeza uzalishaji na kupata soko la uhakika ndani na nje ya nchi.

Aidha, wakulima hao wanaiomba Serikali kupunguza ushuru unaotozwa kwenye zao hilo kutoka

Sh2,000 za sasa kwa gunia hadi kufikia Sh1,000. Kiasi hicho wanachotozwa, wanasema kinawaingizia hasara hivyo kushindwa kuondokana na umasikini wa kipato.

Mkulima Rashid Seif akizungumza kuhusu changamto za soko kwenye mradi wa shamba la vitunguu kwenye kijiji hicho cha Gunge, anasema Serikali itazame jambo hilo kwa upana mkubwa kwani ushuru wanaotozwa unawarudisha mno.

“Serikali inapaswa kututafutia soko la uhakika ili tuuze mazao kwenye sehemu sahihi kuliko hivi sasa inapotubana kwa kutoza ushuru mkubwa, ilihali haijaboresha fursa za soko la uhakika zaidi ya kunyonywa na wachuuzi,” anaeleza.

Mkulima mwingine, Mary Laizer anasema kutokana na ukosefu wa soko la uhakika, wachuuzi kutoka Kenya wamekuwa wakija Simanjiro kununua mazao yao na kuyasafirisha, huku wakiyawekea nembo kuwa yamezalishwa Kenya.

Hata hivyo, Mary anasema kwa hali ilivyo katika soko, wakulima wengi pamoja na kupunjwa wanapendelea kuuza mazao yao kwa wafanyabiashara wa Kenya ambao kidogo wana afadhali kuliko wafanyabiashara wa ndani anaosema wanawanyonya zaidi katika bei.

“Pamoja na changamoto ya ukosefu wa soko la uhakika pia tunauza mazao yetu kwa kupimiwa kwenye madebe, viroba na magunia, badala ya kutumia mizani ili kubaini uzani wa mazao ndipo yauzwe, hivyo wakulima tunazidi kunyonywa kwa kutumia vipimo vya kienyeji,” anasema.

Pamoja na changamoto hizo, anasema kwa kupitia kilimo cha umwagiliaji wa kitunguu, wangeweza kujifunza matumizi sahihi ya mbolea na viuatilifu pamoja na kujua taratibu za kilimo cha zao hilo katika ukanda wa tambarare na miinuko.

Changamoto nyingine ni pamoja na mazao kusahambuliwa na wadudu na magonjwa, kukosa utaalamu wa kilimo cha umwagiliaji na ghala la kuhifadhia mazao.

Kauli ya Serikali

Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Mahamoud Kambona hivi karibuni alitembelea eneo la Ngage na kuzungumza na wakulima wa vitunguu, akiwaahidi Serikali kuboresha kilimo hicho ikiwamo kuwatafutia soko la uhakika.

Alisema kuwa wakulima wanapaswa kuboresha kilimo chao, huku Serikali kwa upande wake ikiwa na wajibu wa kuwapatia pembejeo za kilimo kama mbolea za kupandia, kukuzia na mbegu.

“Pamoja na hayo ninyi wakulima wa bonde la eneo hili msilime zao moja la vitunguu pekee, mnaweza kulima mazao mengine mbadala kama mahindi au maharagwe kwa kutumia umwagiliaji huu,” anasema Kambona.

Anasema, “Maisha bora ya Mtanzania hutokana na kujishughulisha kwa shughuli mbalimbali halali, hivyo changamoto zenu zibadilisheni ziwe fursa na mtafanikiwa kupitia kilimo hiki cha vitunguu.”

Onyo kwa wafugaji

Ofisa kilimo na umwagiliaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Claude Losioki, aliwataka wafugaji wa eneo hilo kutoingiza mifugo yao kwenye skimu za umwagiliaji wa kilimo hicho cha vitunguu, kwani wanaharibu miundombinu hiyo.

Losioki anasema, Serikali imetumia gharama kubwa kuzitengeneza skimu hizo za umwagiliaji wa vitunguu, hivyo siyo jambo la busara kuingiza mifugo kwenye eneo lililotengwa kwa ajili ya shughuli la kilimo na kisha kuziharibu.

“Kinachotakiwa ni kuheshimu matumizi bora ya ardhi kwani kila kijiji kimetenga maeneo ya kilimo, kuchungia mifugo kwa malisho, makazi, nyumba za ibada na huduma nyingine, hivyo wafugaji msiwaingilie wakulima,” anaeleza.