Wakulima wengi hawana ujuzi wa kulima muhogo

Baadhi ya magugu yanayoathiri muhogo kuwa ni Rumbugu au kwekwe (Adropogon spp, Imperata cylindrical, Panicum maximum andPennisetum spp mengine ni ndago, kafura na kijiji.

Zao la muhogo limekuwa likilimwa nchini kwa muda mrefu. Zao hilo hulimwa na nchi zaidi ya 90  duniani, Ni zao muhimu na huliwa na zaidi ya watu milioni  12 katika mabara ya  Afrika, Asia na Latin America.

Muhogo ni muhimu kwa kinga ya njaa na biashara na hutumika kutengeneza chakula cha mifugo na malighafi kwa viwanda.

Hata hivyo, kutokana na changamoto za uzalishaji kama vile magonjwa, ukame na ukosefu wa utalaamu uzalishaji wa muhogo nchini haujafikia kiwango cha kimataifa wa tani 10 kwa hekta, badala yake wakulima wengi wamekuwa wakipata tani tano  hadi saba kwa hekta.

Utafiti umeonyesha kuwa muhogo unaweza kutoa mazao kuanzia tani 20 hadi 50 kwa hekta kama kanuni za kilimo bora zikifuatwa na wakulima wakatumia mbegu bora za muhogo.

Wakieleza uzoefu wao katika ziara ya wataalamu kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) na Kituo cha utafiti wa kilimo Ukiriguru (Mwanza), baadhi ya wakulima wilayani Chato mkoani Geita hivi karibuni, wanasema uzalishaji wa muhogo umekuwa ukishuka siku hadi siku kutokana na magonjwa.

Lazaro Kagundulilo ambaye ni mkulima katika kijiji cha Ipandikilo wilayani humo, anasema awali kijiji hicho kilichoanzishwa enzi za vijiji vya ujamaa mwaka 1973 kilikuwa kinastawi kila aina ya mazao, lakini sasa magonjwa yamekuwa kikwazo.

“Maana ya jina la Ipandikilo ni kupata, maana yake wakati vijiji vya ujamaa vinaazishwa kulikuwa na ardhi yenye rutuba inayokubali mazao mengi. Wengi tulishawishika kuhamia huku. Lakini sasa magonjwa yametuzidi,” anasema Kagundulilo mwenye shamba la ekari nne za muhogo.

“Magonjwa ya muhogo hasa michirizi na batobato yalianza mwaka 2009 kiasi kwamba sasa mavuno yameshuka. Katika shamba hili la ekari nne nategemea kupata tani moja au mbili za muhogo. Nimelima pia viazi na mahindi,” anasema.

Mkulima mwingine mwenye masikitiko ni Andrew Misano mwenye ekari saba za muhogo anayesema magonjwa hayo mawili yanampa wakati mgumu.

“Nimepanda aina nne za muhogo ambazo ni lyongo, misongoma, mwanabukombe na muhogo mtamu. Mihogo hutumia kati ya mwaka mmoja na nusu hadi miwili kuvunwa. Hapa natarajia kuapa tano tano tu kwa sababu ya magonjwa,” anasema.

Ofisa kilimo wa kijiji hicho, Khamis Matesi alisema kijiji hicho kina kaya 228 zionazolima muhogo na huenda wakakabiliwa na njaa kwa sababu ya magonjwa.

“Tunawashauri wakulima wang’oe mashina ya mihogo yaliyoathiriwa kwa sababu hakuna dawa inayotibu. Asilimia 50 ya mihogo imeathirika,”  anasema Matesi.

Ofisa kilimo wilayani Chato, Faizaya Memitansago anasema asilimia 60 ya wakulima wa muhogo wameathiriwa na magonjwa hivyo wananyemelewa na njaa.

Uzalishaji bora wa muhogo

Akizungumza na wakulima hao, mtaalamu wa mazao ya mazao ya mizizi kutoka katika kituo cha utafiti wa mazao ya kilimo Ukiriguru Mwanza, Dk Simon Jeremiah anasema kabla ya kulima, mkulima anapaswa kuangalia historia ya eneo hilo.

“Hii ni muhimu ili kuelewa kama kuna magugu hatari na wadudu au magonjwa kwenye eneo hilo  ili kubuni mbinu za kuyazuia au kuyaangamiza mapema,”  anasema.

Anasema shamba la muhogo linatakiwa kupandwa mwanzoni mwa msimu wa mvua ili kupata mavuno mengi (Oktoba hadi Machi/Aprili).

“Chagua mimea isiyo na wadudu au magonjwa. Pingili zenye afya na macho ya kutosha zitumike kupanda. Panda mapema pingili za muhogo baada ya kuzikata

“Mbegu za kupanda zitokane na chanzo cha uhakika kama ‘tissue culture’. Pia mbegu ziwe zile zilizosafishwa kwa mionzi na kuzalishwa katika hali ya usafi mkubwa kutoka kwenye mashamba yanayokidhi vigezo vya mashamba ya mbegu yanayokaguliwa mara kwa mara na Taasisi ya udhibiti wa ubora wa mbegu Tanzania (TOSCI),” anasema Dk Jeremiah.

Anazitaja mbegu mpya tisa za muhogo zilizobainika kuwa na uvumilivu wa kutosha kuwa ni TZ 130, Mkumba, Mkuranga 1,Kipusa, Chereko, Nziva, Kizimbani, F10-30R2 na Pwani.

Magonjwa

Akizungumzia magonjwa ya muhogo, Dk Jeremiah anautaja ugonjwa wa Batobato akisema mmea hupata mabaka ya njano kwenye majani na kupoteza umbo la majani na matokeo yake hushindwa kuweka muhogo.

“Wakati mwingine majani ya juu hubadilika na kuwa na mabaka  kama ishara ya mmea kuugua baada ya wadudu kuleta virusi kutoka mimea mingine,” anasema.

Anautaja pia ugonjwa wa michirizi kahawia unaoweka mabaka yaliyoungana kwenye majani ya chini na mmea kukauka kuanzia juu na michirizi kwenye majani ya chini pekee.

Ugonjwa mwingine ni Baka bacteria unaosababisha mabaka ya kahawia yasiyo na umbo maalum kwenye majani ya chini na wakati mwingine sehemu iliyoungua huondoka na kubaki mashimo katikati.

Mbali na magonjwa anataja pia wadudu wanaoshambulia muhogo kuwa ni Vidungata wanaoonekana kufunikwa na vitu laini vyeupe, Tanabui wa kijani  na Inzi weupe

Anamtaja pia panzi kunuka ambaye hujitokeza kuwa tatizo wakati wa kiangazi, hivyo wakulima hushauriwa kulima mapema kabla ya kiangazi.

Mdudu mwingine ni ‘cassava scale’ ambaye hushambulia shina la muhogo na kufyonza majimaji ya mmea.

Pamoja na kukabiliana na magonjwa, Dk Jeremiah anashauri wakulima kurutubisha ardhi kwa kuweka mbolea za samadi na za viwandani.

“Tahadhari lazima ichukuliwe kabla ya matumizi ya mbolea, kwani unaweza kustawisha majani na shina badala ya mizizi. Inashauriwa kutumika tu pale rutuba ya shamba inapokuwa chini sana. Kiwango bado kinafanyiwa kazi,” anasema.

Kuhusu uvunaji anashauri ufanyike wakati wa kiangazi , wakati huu mihogo huwa na wanga wa kutosha, Pia, utengenezaji wa makopa au udaga ukaushaji huwa rahisi.

“Aina za muhogo zinazowahi kukomaa huchukua kati ya miezi sita na nane tangu kupandwa , na kwa zinazochelewa huchukua miezi 12 and 19

“Wingi wa mavuno huanzia tani 20 mpaka  30 kwa hekta kwa mbegu za kienyeji na kuanzia tani 25 to 70 kwa hekta kwa mbegu zilizoboreshwa

Mihogo ikivunwa huchukua siku mbili mpaka tatu kuanza kuharibika na kuoza, hivyo anashauri mbinu za kuihifadhi ikiwa pamoja na kuweka kwenye mashimo yaliyofunikwa na majani, kutunza kwenye taka za mbao zenye unyevu na kutunza kwenye mifuko ya plastiki yenye unyevu.

Mshauri wa Jukwa la Baioteknolojia (OFAB) lililo chini ya Costech, Dk Nicholas Nyange anasema kwa sasa Serikali imeanzisha utafiti wa uzalishaji wa mbegu za mahindi na muhogo kwa teknolojia ya uhandisi jeni (GMO) ili kukabiliana na magonjwa na ukame.