UCHAMBUZI: Walichokisema Chadema kina ukweli ndani yake

Muktasari:

Maelezo hayo ya Mwalimu Nyerere yapo kwenye kitabu chake cha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania kilichoandikwa mwaka 1994 na kutolewa 1995.

Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kupendekeza kuanzishwa Serikali ya Tanganyika, kama sharti la kuingia kwenye Shirikisho la Afrika Mashariki.

Maelezo hayo ya Mwalimu Nyerere yapo kwenye kitabu chake cha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania kilichoandikwa mwaka 1994 na kutolewa 1995.

“Wakati Mwalimu anaandika kitabu hiki mwaka 1994 Taifa letu lilikuwa linakabiliwa na changamoto kadhaa za kihistoria ambazo ndizo zilimfanya kuingilia kati na kuandika kijitabu hiki ambacho kilikuwa kama nasaha, onyo, na usia kwa Watanzania,” inasema sehemu ya utangulizi wa kitabu hicho.

Katika kitabu hicho Mwalimu Nyerere alisema iwapo nchi za Afrika Mashariki zikiamua kuungana na Tanzania ikawa mshiriki, anaamini kuwa ni rahisi zaidi kushirikisha Tanzania yenye serikali mbili ya Zanzibar na ya Tanganyika kuliko Tanzania yenye serikali mbili, ya Tanzania na Zanzibar.

Alisema kwa kufanya hivyo, wapendao Utanganyika watakuwa wazalendo zaidi, badala ya kuwa wasaliti, wakiazimia Afrika ya Mashariki iliyoungana kuwa nchi moja, kuliko Tanzania ilyotengana ikawa nch mbili.

Kila mtu anakumbuka jinsi mjadala wa mfumo wa Serikali mbili au tatu ulivyoshika kasi ulipoanza mchakato wa kuandika Katiba Mpya.

Mwalimu Nyerere alikuwa miongoni mwa viongozi wanaoweza kubadilika kulingana na wakati na nini wananchi wanataka. Alikubali mfumo wa vyama vingi vya siasa licha ya kupingwa na wafuasi wa chama chake.

Jumatano iliyopita Chadema kilitangaza mikakati mitatu ya kupinga ukandamizaji wa haki na demokrasia unaodaiwa kufanywa na Serikali, na moja ya mikakati yake ni kufanya mikutano ya hadhara na maandamano nchi nzima.

Mikakati yake mingine ni kuanzisha operesheni iliyopewa jina la Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta) na kwenda mahakamani kudai tafsiri ya kisheria juu ya masuala yote ya ukiukwaji wa Katiba, sheria na taratibu yanayofanywa na Serikali.

Unaweza usikubaliane na Chadema kuhusu udikteta, maandamano na mikutano ya hadhara lakini ndani ya mambo hayo ambayo ‘unaweza kutokubaliana nayo’, kuna mengi ya msingi yaliyoelezwa. Ni kama Mwalimu Nyerere alivyokuwa mwepesi wa kushauri jambo na wakati mwingine kwenda tofauti na wengi, ndivyo inavyopaswa kuigwa na viongozi wetu wa sasa.

Si kila anayekosoa mambo yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano ni adui. Wapo wanaokosoa masuala ya msingi ambayo yakifanyiwa kazi yanaweza kuwa na faida kubwa kwa Taifa. Chadema wamegusia suala muhimu sana juu ya Jeshi la Polisi kuzuia shughuli za siasa nchini. Chama hiki pamoja na mambo mengine kimetumia nafasi yake kukosoa baadhi ya mambo yanayotendeka sasa.

Wakosoaji ni watu muhimu katika taifa lolote lile duniani. Watu hawa wanaona mambo mabaya na kushauri yawe mazuri na kisha kutaka yadumu yakiwa na tija na kama ni mazuri basi hutoa ushauri ili kuboresha uzuri wa jambo husika ili liwe na tija.

Watu husahau kuwa hata jambo zuri lina changamoto zake ambazo ni vyema zikawekewa misingi imara. Kinachofurahisha zaidi ni haya yanayofanywa na Rais John Magufuli leo, hivi ni nani hakuwahi kuyasikia yakizungumzwa na wapinzani miaka ya nyuma?

Nchi yetu pengine ni miongoni mwa nchi zenye watu wanaotenda miujiza bila kujijua. Miaka michache iliyopita hoja za upinzani kuhusu ufisadi, ubadhirifu, wizi, uzembe, rushwa, mazoea kazini na unyang’anyi zilipuuzwa na kuonekana si lolote. Lakini leo watu hao hao wanamshangilia rais anayepambana na masuala hayo

Naikumbuka hoja ya ‘ukubwa wa baraza la mawaziri la JK’, bila shaka utakumbuka pale bungeni Dodoma jinsi wana-CCM walivyowashukia wenzao wa upinzani eti kwa sababu ya kupinga ukubwa wa baraza la JK.

Yupo waziri mmoja alidiriki kusimama huku akiweka sawa tai yake na kueleza faida za safari za nje za Rais Kikwete, hiyo ni baada ya hoja ya John Mnyika na Freeman Mbowe juu ya safari za nje za rais huyo wa Awamu ya Nne.

Dk Magufuli kuingia tu kateua baraza lenye mawaziri 34 kutoka 55 wa JK na uamuzi huo unaonekana mzuri. Tujiulize kama tungekuwa na baraza dogo tangu mwaka 2005 tungeokoa kiasi gani cha fedha.

Kumbuka JK alianza na baraza la mawaziri 60 na akamaliza na mawaziri 55.

Huku kwenye safari za nje mambo ndiyo yapo wazi kabisa, Rais Magufuli ameeleza wazi kuwa kuanzia mwaka 2013 hadi 2015, safari hizo zimeigharimu Serikali Sh356.3bilioni, fedha ambazo alisema zingeweza kujenga barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 400.

Kuwa mpinzani na kuhoji masuala muhimu kwa maslahi ya taifa si dhambi na wala hautakamatwa kwa kuhisishwa na uhalifu. Kukosoa Serikali na watendaji wake kwa hoja na ushahidi ndiyo chanzo cha mabadiliko duniani. Watu waliwacheka wapinzani wakati wakiibua hoja zao bungeni lakini kwa hii staili ya Hapa Kazi Tu, hakika watu hawa wanaanza kuumbuka taratibu. Waliyoyapinga jana wakati yakisemwa upande wa pili, wanayashangilia leo kwa sababu yanafanywa na upande wao. Ubinafsi gani huu wa maendeleo ya nchi yetu!

Walichokisema Chadema kina maswali mengi lakini kuna ukweli ndani yake, huo uchukuliwe na kufanyiwa kazi na watawala.

0754 597315