Waliobwagwa Kenya wakimbilia kujitenga

Kuna ramani inayazungushwa katika mitandao ya kijamii tangu muungano wa National Super Alliance (Nasa), kupoteza kinyang’anyiro cha urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa Kenya wiki tatu zilizopita.

Ramani hiyo imezua mijadala kote nchini humo. Hii si ramani ya kawaida; na ndio sababu imeibua mjadala wa kukata na shoka. Ramani hiyo inaonyesha Kenya mbili zilizojitenga.

Kenya ya kwanza inaanzia Lau katika mwambao wa Pwani na kuelekea eneo la Nyanza, eneo la Magharibi mwa Kenya hadi jimbo la Turkana. Hii ndiyo Kenya ambayo inaitwa United People’s Republic of Kenya. Eneo hili lote lina ufuasi mkubwa wa Nasa unaoongozwa na Raila Odinga.

Kenya ya pili inayoitwa Central Republic of Kenya inajumuisha maeneo ya Kaskazini mwa Kenya (Kwa Wasomali), Eneo la Kati ya Kenya(Kwa Wakikuyu) na Kanda ya Bonde la Ufa inayomilikiwa na jamii ya Wakalenjin.

Jamii hizi (Kikuyu, Kalenjin na Wasomali) zinaunga mkono chama tawala cha Jubilee kinachoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta. Kwa kifupi, kuna watu wenye mawazo ya kizamani wanaotaka kugawanya nchi kulingana na maeneo ya Nasa na ya Jubilee.

Tayari, ombi linalowataka Wakenya wanaokubaliana na hatua hii linaendelea kusambazwa kuwatafuta wenye mawazo kama hayo kutia sahihi ili kuipa kibali cha kisheria kugawanywa kwa nchi.

Wanaosukuma wazo hili wanasema wanahitaji saini milioni 15 ili waweze kupata haki kisheria kujitenga na sehemu nyingine ya nchi na wana sababu zao za kufanya hivyo.

Mawazo haya yameenea nchini kote huku upinzani ikisisitiza kuwa wanapanga maandamano makubwa kushinikiza Serikali kukubali masharti yao.

Wito huu wa kutaka watu waweke saini katika ombi hilo la kutaka kujitenga kwa sehemu zingine za Kenya unaendelea bila bughudha mitandaoni.

Wanaousukuma wanapania kuuwasilisha katika kitengo cha sheria cha Umoja wa Afrika na pia Tume ya Afrika ya Haki za Kibinadamu.

Si mara ya kwanza

Hii si mara ya kwanza wito kama huu kufanywa. Mwaka 2012, watu fulani kutoka Pwani waliunda chama kinachoitwa Mombasa Republican Council (MRC) kilichokuwa na mawazo na falsafa kama hii lakini Serikali ya kitaifa ilifanya kila liwezalo kukizima.

Waanzilishi wake walitiwa mbaroni na kufunguliwa mashtaka. Hatimaye moto waliokuwa wameuwasha kwenye fikra za Watu wa pwani ulizimwa. Hata hivyo, MRC ingali iko kwa sababu haikufutwa.

Wanaouza wazo kama hii sasa wanaweza kujiunga na MRC na kuanza upya mchakato wa kupigia debe fikra ya maeneo kadhaa ya Kenya kujitenga na kupata uhuru wa kujitawala kama nchi nyingine.

Waasisi wa MRC wanasema watu wa pwani wamenyanyaswa kiuchumi na kijamii kwa miaka mingi na imefika wakati wa eneo hilo kujitenga na kujitawala.

Mmoja wa wanaharakati wa wazo hilo ni msomi maarufu wa masuala wa kiuchumi, Dk David Ndii ambaye pia ni mshauri mkuu wa Raila.

Mwaka jana, Ndii aliandika makala kwenye gazeti moja la kila siku nchini ambayo ilizua mjadala ulioendelea kwa takriban mwezi mmoja. Ndii anasema inasikisha kuwa kwa miaka 54 tangu Kenya kujinyakulia uhuru, maeneo mengi ya nchi bado yako nyuma kimaendeleo.

Isitoshe, anasema kuwa makabila mengine yamebaguliwa na kutengwa na Serikali zote tangu 1963 na kilichosalia sasa ni maeneo yanayosongwa na athari za kutengwa kuanza kujitawala.

Ndii anaitazama Kenya kama ndoa ambayo imejaa udhalimu na unyanyasaji wa muda mrefu na kilichosalia ni talaka.

La kustaajabisha ni kuwa, wengi wa Wakenya wana mawazo kama yake ndio maana unaona sahihi zikiendelea kuwekwa kwenye ombi lililo mitandaoni.

Wiki jana, alipokuwa akizungumza kwenye runinga ya NTV, msomi huyo alisisitiza kuwa hakuna matumaini ya Kenya kuwa taifa lenye viongozi wanaotenda haki kwa wananchi wote bila kujali msingi wao wa kabila wala siasa.

“Kama demokrasia na hatua za amani zimekosa kuleta usawa katika jamii, basi mtutu wa bunduki ndio utaleta usawa huo na haki kwa wote,” anasema Ndii.

Ombi la sasa linaeleza kuwa kumekuwa visa vingi vya wizi wa kura miaka nenda rudi na mauaji ya kiholela ya watu wasio na hatia.

Haya ndiyo misingi ya ombi lao la kutaka kujitenga na kuwa na taifa lao linaloitwa Jamhuri ya Watu wa Kenya (People’s Republic of Kenya). Kisheria hii inaitwa kujitawala.

Msingi wa ukabila

Inaeleweka kwa nini wanaosukuma wazo hili wamewatenga Wakalenjin na Wakikuyu kwa kuwafungia nje ya ramani yao mpya; Tangu Kenya ijinyakulie uhuru 1963, ni makabila mawili ambazo yamekuwa yakiongoza kati ya makabila 44.

Hiyo haingekuwa hoja kama viongozi wa makabila haya (Kalenjin na Kikuyu) wangefanya haki na usawa kwa wananchi wote. Hii ndio kidonda kinachowauma wengi wanaohisi kuwa ingawa ni Wakenya, hawatambuliwi na sera za maendeleo, kisiasa na kiuchumi.

Jamii nyingi za Kenya zinahisi kuwa raslimali za nchi zinawanufaisha watu wachache huku wengi wakielea kwenye lindi la ufukara uliokithiri. Zinasema imefika wakati wa kila mtu kupewa sehemu yake ili aweze kujikimu awezavyo.

Wanaosukuma wazo hili wanasema pia kuwa uchaguzi wa mwaka huu ulivurugwa kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu na wanasema wamevumilia vya kutosha na imefika wakati wa kusema basi.

Punde tu baada ya uchaguzi wa Agosti 8, 2017, utata kuhusu wizi wa kura ulianza na kusababisha Serikali ya Uhuru Kenyatta kutumia polisi kukabiliana na waliotaka kuandamana, ingawa baadaye Rais huyo akatangaza ruksa ya kuandamana bila kuharibu mali za wananchi.

Duru zinasema katika maandamano ya awali, wafuasi wa Raila wapatao 24 waliuawa kwa risasi wakiwamo watoto wawili. Wengine zaidi walijeruhiwa. Hii, Nasa inasema ni dhuluma na ukiukaji wa Katiba.

Licha ya kuenea kwa habari za watu kutaka kujitenga na kujitawala, muungano wa Nasa haujagusia suala hili lakini kwamba ni mmoja wao anaipigia debe suala hilo ni sababu tosha ya kuamini kuwa muungano huu uko ndani ya mipango hii.

Hivi sasa Nasa iko mahakamani kupinga ushindi wa Rais Uhuru, ikisema matokeo ya urais yaliyompa kiongozi huyo ushindi yalikuwa ya kughushi kwa sababu yalitengenezwa kwa kompyuta. Hii ndiyo sababu Raila anawaita viongozi wa Jubilee “vifaranga wa kompyuta”.

Baadhi ya wafuasi na marafiki wa Raila kama vile Mwenyekiti wa ODM, John Mbadi wanasema ikiwa wizi wa kura wa mara kwa mara hautarekebishwa, “ni bora Wakenya wengine wajiondoe na kujitawala kivyao.”

Baadhi ya Wakenya kutoka jamii zinazohisi kudhulumiwa na Serikali kwa miaka mingi wanasema inasikitisha kuwa kuna baadhi ya jamii zinazoamini kwamba uongozi ni urithi wao na kamwe watafanya kila wawezalo kuwafungia wengine nje ya uongozi wapende wasipende.

Mwanasheria Mkuu wa Kenya, Githu Mungai anasema Katiba ya nchi hiyo inasisitiza umoja wa taifa lote na hiyo ni sheria ambayo haiwezi kupingwa na yeyote na hivyo wanaotaka kujitenga wanakwenda kinyume cha sheria.

Kipengee cha 5 cha Katiba ya Kenya hakikubali eneo lolote la nchi kujiondoa lakini kinakubali eneo kuongezewa kwa nchi kupanuliwa. Kwa hivyo, wanaojitaka kujitenga watakuwa na wakati mgumu kisheria.

Hali ya kujitenga hutokea wakati watu wanapotangaza uhuru wao kutoka kwa Serikali. Wakati kikundi kisichoridhika kinapojitenga, kinaunda mfumo wake wa Serikali kwa pengo lililoachwa na serikali ya hapo awali.

Hata hivyo, hali hiyo ya kujitenga si suala jepesi, ni zito mno na linaweza kutoa nafasi ya vita. Kujitenga pia huathiri uhusiano wa kimataifa na amani ya taifa na wananchi wake ambao wameamua kujitawala.

Nchi nyingi zinalitazama suala la kujitenga kwa miji au majimbo kama kitendo cha uhalifu ambao unaweza kusukuma Serikali kutumia nguvu kuhakikisha wenye fikra za sampuli hii wanasalimu amri.