Wameshirikishana zaidi ya mara moja kwenye nyimbo

Muktasari:

Mara nyingi wasanii hufanya kolabo na mtu mara moja tu na kutorudia tena, lakini wakati fulani kulingana na sababu moja ama nyingine wasanii hurudia kufanya kolabo.

Wasanii wa muziki duniani kote wamekuwa na kawaida ya kushirikishana kwenye kazi zao za sanaa lengo kuu likiwa ni kuungana mkono, kuonyesha kukubali au kupenda kile kinachofanywa na mwingine na pia kutafuta kutangaza kazi husika kupitia jina la msanii anayeshirikishwa.

Mara nyingi wasanii hufanya kolabo na mtu mara moja tu na kutorudia tena, lakini wakati fulani kulingana na sababu moja ama nyingine wasanii hurudia kufanya kolabo.

Kwa bahati mbaya au nzuri mara nyingi wasanii wanapofanya kolabo ya mara ya kwanza huwa nzuri, wanaporudia nyingi hushindwa kubamba.

 

Ommy Dimpoz ft Alikiba

Mara ya kwanza Ommy Dimpoz alimshirikisha Kiba katikati ya mwaka 2012 kwenye wimbo uitwao ‘Nainai’ ambao kimsingi ulikuwa ni wimbo wake wa kwanza kuwazawadia Watanzania na uliompa ramani ya kuelekea kwenye orodha ya wasanii wakubwa wa Bongo Fleva.

Miaka minne baadaye Dimpoz akaamua kufanya kitu kingine tena na Alikiba kwa kumshirikisha katika ngoma yake iitwayo ‘Kajiandae’ iliyoachiwa mwanzoni mwa mwezi huu.

 

 

Ney Wa Mitego ft Diamond

Pengine hakuna shabiki aliyewahi kufikiria kusikia ngoma ya pamoja ya Ney wa Mitego na Diamond kutokana na tofauti ya aina ya muziki wanaofanya.

Mwaka 2013 Ney wa Mitego alifanya kinyume na mitazamo ya wengi kwa kumshirikisha Diamond Platnumz kwenye wimbo uitwao “Muziki Gani” ambao waliimba kama watu wanaotupiana madongo yanayofanana na maisha yao halisi.

Mwaka 2015 akamshirikisha tena Diamond katika wimbo wake wa “Mapenzi au Pesa” ambao nao waliimba kwa mtindo ule ule wa kujibizana juu ya maisha yao halisi.

Licha ya nyimbo zote kuwa nzuri, bado “Muziki Gani” ulibamba kuliko “Mapenzi au Pesa”.

 

Shetta na Diamond

Katikati ya mwaka 2012 Shetta alitulia na kuwapikia mashabiki wake ladha ya muziki mtamu kwa kuachia ngoma kali iitwayo “Nidanganye” ambayo alimshirikisha Diamond Platnumz.

Haikuwa mwisho, miaka miwili baadae Shetta akamtafuta tena Diamond na kumshirikisha kwenye wimbo wake uitwao “Kerewa”. Kati ya Nidanganye na Kerewa upi ulifanya vizuri? Wewe shabiki wa wanamuziki hawa unalo jibu.

 

Stamina ft Fid Q

Miongoni mwa vitu ambavyo Stamina haoni soni kuvisema hata mbele za watu ni suala la kumkubali mkongwe wa muziki wa ‘Hip Hop’ nchini, Fid Q.

Ili kuthibitisha hilo, Stamina alimshirikisha Fid Q kwenye wimbo uitwao “Ushauri Nasaha” ambao kwa bahati mbaya ulivuja na kuwafikia mashabiki kabla ya muda waliopanga.

Hata hivyo, Stamina hakukata tamaa, alimshirikisha kwa mara ya pili Fid Q kwenye wimbo mwingine uitwao ‘Wazo la Leo’.

Mwaka 2015 alimshirikisha tena kwenye wimbo wake uitwao ‘Like Father Like Son’ na huenda tutarajie kazi zaidi ya hizo kutoka kwa wawili hao.

 

Abby Skillz ft Mr Blue na Kiba

Abby skillz aliamua kufanya kitu cha tofauti katika ulimwengu wa muziki mwanzoni mwa miaka 2000 aliachia ngoma iitwayo ‘Maria’ ambayo alimshirikisha Mr Blue pamoja na Ali Kiba.

Mwaka 2016 Abby aliamua kufanya kama alichokifanya awali kwa kuwashirikisha tena Mr Blue na Alikiba kwenye ngoma yake iitwayo ‘Averina’.

Nyimbo hizi mbili pamoja na kuchezwa na wasanii wakubwa zimeshindwa kuwa maarufu, huku ya kwanza ikitamba zaidi na kuipoteza kabisa ya pili.

 

Stamina ft Rich Mavoko

Watanzania wengi wamemfahamu Stamina kutokana na wimbo wake wa ‘Kabwela’ ambao ulibeba ujumbe murua kupitia mashairi yake mazito ya kiutu uzima.

Katika wimbo huo Stamina alimshirikisha Rich Mavoko ambaye aliimba kiitikio.

Mwaka mmoja baadae Stamina alimtafuta tena Rich Mavoko na kumpa nafasi ya kuimba kiitikio katika wimbo mwingine uitwao ‘Najuta Kubalehe’

 

Mwana Fa ft Lady Jay dee

Kama unaikumbuka ‘Alikufa kwa Ngoma’ ya Mwana FA basi huwezi kusahau kuwa alimshirikisha Komando Lady Jay Dee ambaye aliimba kiitikio.

Lakini hiyo haikuwa mwisho, Mwana FA aliachia wimbo mwingine alimshirikisha Lady Jay Dee; kibao kiliitwa ‘Hawajui’.

Zote zilikuwa nzuri na umahiri wa wasanii hao wawili ulichangia, lakini kila moja iliishinda nyingine.