Wanafunzi wa kiume nao wanahitaji ulinzi wa karibu

Wanafunzi wakiwa na mabango yanayoashiria ulinzi kwa watoto wa kiume kama ilivyo kwa wenzao wa kike .Picha na Tumaini Msowoya

Muktasari:

  • Jamii inawatazama watoto wa kiume kama watu wasioonewa, wenye nguvu na uwezo wa kukabiliana na mambo magumu na wakati mwingine na huonekana hawapo kwenye mazingira hatarishi.

Kama utasikia ulinzi wa mtoto unazungumzwa na kupigiwa kelele kwa nguvu zote, kipaumbele huwa kwa mtoto wa kike na sio wa kiume.

Jamii inawatazama watoto wa kiume kama watu wasioonewa, wenye nguvu na uwezo wa kukabiliana na mambo magumu na wakati mwingine na huonekana hawapo kwenye mazingira hatarishi.

Mtoto wa kike anaangaliwa zaidi kwa sababu ya maumbile yake, hivyo wakati yeye anapewa vipaumbele vingi, mtoto wa kiume anasahaulika.

Wadau wa elimu wakiwamo walimu wanasema hali ni mbaya hata kwa watoto wa kiume.

Walimu waliohudhuria katika kampeni ya ‘Tumkumbuke na Mtoto wa Kiume’ inayoongozwa na Dahuu Foundation, iliyofanyika katika viwanja vya shule ya Msingi, Muhimbili jijini Dar es Salaam walivunja ukimya wakisema; ‘ hata watoto wa kiume wanahitaji kulindwa’.

Wanasema yapo matukio mengi ya watoto wa kiume kufanyiwa ukatili wa kijinsia ikiwamo kulawitiwa, huku jamii ikiwapa kisogo kwa kutowasikiliza.

Mwalimu wa shule ya msingi Mivinjeni, Manispaa ya Ilala Kiemena Athumani anasema wazazi wengi wamejisahau kwa kumhofia zaidi mtoto wa kike wakiamini wa kiume yupo salama.

“Ninayo mifano dhahiri ya watoto kufanyiwa ukatili huu, matukio haya yapo kwa kweli na ukatili huu unafanywa na ndugu wa karibu huko majumbani kama wajomba, kaka hata majirani,” anasema na kuongeza;

“Niliwahi kutana na kesi ya baba mdogo kumfanyia ukatili mtoto wa kaka yake, wazazi kuwalaza watoto wa kiume na wakubwa wakiamini ni salama ni hatari sana, sio salama kabisa,”

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Muhimbili, Jovitha Mushi anasema matukio mengi yanawakuta watoto wa kiume bila kujua kwa sababu jamii imejikita zaidi kumkumbatia mtoto wa kike.

“Tumeshindwa kukimbia na mtoto wa kiume kama tunavyokimbia na watoto wa kike, hii ni hatari na uwepo wa kampeni hii utawakumbusha wazazi wajibu wao,”alisema.

Kaimu Ofisa Elimu wa Wilaya ya Ilala, Rehema Msologonhe anakiri kuwapo kwa ukatili mkubwa kwa watoto wa kiume kama ilivyo kwa watoto wa kike, japo wamesahaulika.

Anasema kuna hatari ya kuwapoteza kina baba bora na kuwa na wanaume wasio na nguvu za kiume siku za usoni, kama hali iliyopo itakaliwa kimya.

“Tunahitaji baba asimame kwenye nafasi yake kama baba, sasa tusipowasaidia watoto wetu itakuwaje? Ni kweli watoto wa kiume wanafanyiwa ukatili na wamesahaulika, ” anasema Msologonhe.

Mwanaharakati wa Haki za Binadamu, Efero Kusala anasema wakati mwingine mtoto wa kiume anaweza kuchelewa nyumbani wazazi wasihoji wala kutaka kutafiti alikokuwa wakiamini ni salama.

“Kumbe wakati anarudi amekutana na mtu aliyemfanyia jambo baya lakini amemkanya asiseme, kwa hiyo mtoto anaishia kuwa mnyonge mwisho, anaharibika,”anasema.

Anasema vile anavyolindwa mtoto wa kiume, hata wa kike anapaswa kulindwa vivyo hivyo, ili kuleta usawa wa kijinsia na kuwasaidia watimize ndoto zao za kielimu.

Simulizi ya watoto

“Sijawahi kufanyiwa chochote ila rafiki yangu alikuwa anapigwa na mjomba wake. Kila siku akija shuleni anashindwa kutembea ila alishaacha shule,”anasimulia mmoja wa wanafunzi waliokuwa kwenye maadhimisho hayo.

Mwanafunzi mwingine anasema aliwahi kukutana na ukatili siku moja kutoka kwa mgeni waliyemkaribisha nyumbani kwao.

“Mgeni alikuja nyumbani nikalala naye, siku moja lakini usiku alianza kuniumiza, nilimwambia mama akamfukuza,” anasema mwanafunzi huyo.

Miaka miwili iliyopita, mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 11, mkazi wa Buguruni Madenge jijini Dar es salaam jijini Dar es salaam alidaiwa kufanyiwa vitendo vya ulawiti na dereva wa bodaboada katika kituo cha Buguruni Sheli ambae alidaiwa kutoweka na kwenda mahali kusikojulikana mara baada ya tukio hilo kufanyika.

Mtaalamu wa masuala ya kuzuia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kutoka Shirika la Afya Duniani (Unicef), Hafsa Khalfani, anakiri kuwa Tanzania ni kati ya nchi zenye matukio ya unyanyasaji kwa watoto wote.

Takwimu za Unicef zinaonyesha asilimia 72 ya watoto wa kiume na 74 ya watoto wa kike, wamefanyiwa ukatili ikiwamo kipigo.

Takwimu hizo pia zinaonyesha asilimia 25 ya watoto wa kiume na kike wameshafanyiwa ukatili wa kisaikolojia.

Hafsa anasema uchunguzi wao unaonyesha pia watoto wa kwanza na wa mwisho kupanda magari ya wanafunzi wapo hatarini kufanyiwa ukatili wa kingono na wahudumu wa magari hayo.

“Kwa hiyo wazazi wawe tu makini kuwalinda watoto wote,“anasema.

Nini kifanyike?

Mkurugenzi wa Dahuu Foundation, Husna Abdul anasema wameanzisha kampeni ya kumkumbuka mtoto wa kiume baada ya kufanya tafiti shuleni na kugundua hali ni mbaya.

Husna aliyeamua kuanzisha harakati za kuwatetea watoto wakiume, anasema utafiti wake umeonyesha wengi wanafanyiwa vitendo hivyo na ndugu zao wa karibu.

“Watoto wengi wanafanyiwa ukatili na wazazi wao hawajui chochote kwa sababu hofu yao kubwa wameiweka kwa watoto wa kike peke yao, hii ni hatari,”anasema na kuongeza:

“Tulichogundua watoto wa kiume hawasikilizwi kabisa na chanzo cha ukatili huu kwa watoto ni sisi wazazi. Sasa tuvunje ukimya huu, tuwape nafasi tuwalinde pia na kuwasikiliza kama kweli baadaye tunahitaji baba bora.’’

Ofisa Programu wa idara ya utafiti na uchambuzi wa sera-HakiElimu, Florige Lyelu anasema njia pekee ya kupambana na hali hiyo kwa wanafunzi wa kiume ni wazazi na walezi kuwalinda bila ubaguzi kwa kuona wao hawapo hatarini.

“Kwa kweli kesi zipo nyingi tu hata mimi hilo nalitambua, kikubwa ni uangalizi wa karibu kwa watoto wetu. Wazazi na walezi waongee na watoto wao bila ubaguzi na kuhakikisha wanajua kila hatua ya makuzi yao,” anaeleza.

Kauli ya Serikali

Mkuu wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema anatoa wito kwa wahusika ikiwamo madawati ya jinsia kutowafumbia macho watuhumiwa wa kesi za ulawiti na ubakaji watoto.

Anasema dawa yao ni kuwachukulia hatua za kisheria ikiwamo kuwafikisha mahakamani.

“Watoto wazuri msikubali kabisa, hata kama mtu akisema atawapa pipi kataeni na mkaseme kwa wazazi au walimu au mtu yeyote awasaidie. Msikubali hata kidogo sawa ee!”anasema Mjema wakati akizungumza na watoto wa kiume wa shule ya msingi Muhimbili na kuongeza;

“Inaumiza jamani, hawa watu wakikamatwa wafungwe kabisa wakaishie huko huko jela wasionekane kabisa kwenye jamii yetu, hii ni hatari mno.”