MAONI YA MHARIRI: Wanafunzi wasome, wasifanye siasa shuleni

Muktasari:

Kilichotushtua zaidi ni mwalimu huyo kuadhibiwa kwa kusimamia sheria inayokataza shughuli za kisiasa maeneo ya shule na pia kutekeleza agizo la Rais John Magufuli la kuzuia michango isiyo ya lazima kutoka kwa wazazi.

Tumeshtushwa kusikia kwamba Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kasamwa ya mkoani Geita, Dennis Otieno ameshushwa cheo kutokana na kudaiwa kuzuia wanafunzi kuvaa sare za CCM kwenye mahafali ya kidato cha nne.

Kilichotushtua zaidi ni mwalimu huyo kuadhibiwa kwa kusimamia sheria inayokataza shughuli za kisiasa maeneo ya shule na pia kutekeleza agizo la Rais John Magufuli la kuzuia michango isiyo ya lazima kutoka kwa wazazi.

Tukumbushane. Wakati Tanzania Bara inapata uhuru, mfumo wa kisiasa ulikuwa wa vyama vingi lakini mabadiliko ya Katiba yaliyofanyika mwaka 1965 yalifuta mfumo huo ukapitishwa mfumo wa chama kimoja. Hizo ndiyo enzi chama kilishika hatamu.

Baada ya kwenda hivyo kwa muda na baadaye kuonekana utendaji serikalini ulikuwa unakwenda kwa mazoezi bila kupata changamoto na kutokana na upepo wa mabadiliko ya kisiasa duniani uliovuma kuanzia mwishoni mwa miaka ya 1980, Serikali iliamua kuandaa Waraka Na 1 (White Paper) ambapo wananchi walipata fursa ya kutoa maoni aina ya mfumo wa kisiasa.

Julai 1992 yalifanyika mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo yalirejesha mfumo wa vyama vingi. Serikali ikijua ya kuwa siasa zinaweza kusababisha mitafaruku mahali pa kazi, ilitoa mwongozo kuelekeza namna watumishi wa umma watakavyoshiriki shughuli za siasa na maeneo ambayo siasa ni marufuku. Kutokana na mwongozo huo, matawi yote ya CCM maeneo ya kazi, shuleni, vyuoni na majeshini yaliondolewa. Pia, vyama vilipigwa marufuku kufungua matawi kutekeleza, bila shaka, kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu japokuwa ilikuwa haijabuniwa.

Kwa dhana hiyo hiyo ya Hapa Kazi Tu, mwongozo ulitaja makundi ya watu ambao hawakuruhusiwa kujihusisha na siasa japokuwa waliruhusiwa kupiga kura. Makundi hayo ni ya askari wote walioko kazini; JWTZ, JKT, polisi, magereza, uhamiaji na zimamoto.

Wengine ni majaji na mahakimu wa mahakama ngazi zote, wenyeviti, wajumbe na watumishi wote wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi pamoja na wasimamizi wa uchaguzi. Sheria hiyo ilitungwa wakati wa mfumo wa chama kimoja na ilipitishwa na wabunge wa chama tawala. Lakini katika miaka ya hivi karibuni, baada ya vijana wengi kushabikia siasa za mageuzi, kumekuwa na ukiukwaji wa sheria hiyo.

CCM iliamua kuanzisha matawi yaliyounganishwa na walichokiita mkoa wa elimu ya juu unaowashirikisha wanafunzi wa vyuo vikuu; pia, askari wenye magwanda wakaanza kupewa uongozi wa kiraia huku wakiwa na magwanda yao.

Safari hii, Shule ya Sekondari ya Kasamwa inatumiwa kama chachu ya kuanzisha rasmi matawi shuleni kwa jina la klabu ili kujenga uhalali wa kuvaa sare za chama halafu mkuu wa shule anayetetea sheria ya kuzuia matawi ya vyama vya siasa anaonekana mkosaji, ameadhibiwa.

Tujiulize hivi ni halali wanafunzi na walimu hao kuanzia klabu za aina hiyo katika mazingira ya shule? Ikiwa klabu za aina hiyo zitaruhusiwa shuleni, jambo ambalo ni kinyume cha sheria, itakuwaje ikiwa katika shule hiyo hiyo zitafunguliwa klabu ambazo walezi wao wanashabikia mageuzi?

Je, huu si ukiukwaji wa utumishi wa mwalimu huyo? Kama mwalimu anaadhibiwa kwa kusimamia sheria, je, Watanzania wajue kuwa ni taarifa kwamba huko tuendako utawala wa sheria hautaheshimiwa?

Tunaishauri Serikali isimamie sheria zilizopo ili kutoruhusu ushabiki na mitafaruku ya kisiasa mahali pa kazi na shuleni.