KUTOKA LONDON : Wanagombania sehemu ya kuomba omba ...

Muktasari:

  • Sasa hivi kimepita king’ora cha polisi. Wanakimbilia sehemu. Msimu wa jua kali huu Ulaya. Vituko kila mahali. Linapowaka jua wenyeji hugeuka wazimu. Kama fisi walioona simba kamuua nyati wanaitaka minofu.

Nitakivunja vunja kichwa chako!”

Anachacharuka kwa Kiingereza. Kakaa chini. Nje ya supamaketi kubwa la Sainsburys, London. Hapa ni kando ya barabara kuu si mbali na mtaa ninaoishi. Hupita magari mwendo wa kasi. Mwendo unaotakiwa ni kilometa 40.

Sasa hivi kimepita king’ora cha polisi. Wanakimbilia sehemu. Msimu wa jua kali huu Ulaya. Vituko kila mahali. Linapowaka jua wenyeji hugeuka wazimu. Kama fisi walioona simba kamuua nyati wanaitaka minofu.

Kila muda askari hupigiwa simu kusuluhisha ama gari limegonga, watu wamepigana au mtu kalewa hadi hajiwezi kaanguka kando ya njia. Nilipokuwa natoka duka moja nilimwona jamaa fulani na chupa ya bia mkononi kainama anatapika. Jua Ulaya ni hafla, sherehe, arusi, shasmara shamra. Huchanganya na kuchakuchua shauri adimu...

“Hawa jamaa wa hapa huwa wanakunywa kabla ya kula...” Husema wageni wa nchi nyingine. Wazungu wanatofautiana tabia. Watokao Ulaya ya Mashariki hususan Poland, Urusi na nchi za ukanda huo hupata posho nzito kabla ya kunywa. Nyama za nguruwe, kondoo au ng’ombe. Mboga za majani. Wazawa wa mataifa ya Kilatini: Italia, Ufaransa, Hispania na Ureno hula na kunywa pamoja. Ni utamaduni ulioenea. Hata jadi ya kunywa pombe Ufaransa ni tofauti kabisa na Uingereza. Ndiyo maana mvinyo, msosi na mila za kula kijumla Ufaransa ni kinyume kabisa na Uingereza.

Sisi Afrika watumiaji wa wanga (ugali), mihogo, mahindi, viazi vitamu au vikuu, ubwabwa nk. Msosi mkuu wa wanga kwa wenyeji wa Ulaya ni viazi Ulaya, wali na ngano. Ngano imeenea. Utaikuta katika mikate, Pasta, Makaroni, nk. Mzungu akitaka kujaza tumbo atakula pasta au pizza. Vyote vya ngano. Sisi Waafrika hatukuzoea hivyo. Ila wote tunakubaliana katika michuzi. Mboga na nyama.

Sasa Waingereza kijumla, hasa miji mikubwa kama London hawali sana kabla ya kunywa. Lengo ni kunywa ili kulewa.

Tabia hii inayoitwa “binge drinking” imeshika hatamu mwanakwetu. Mwingereza atatoka kazini mathalan siku ya Ijumaa. Na wenzake moja kwa moja wataelekea pabu au baa. Wataivamia pombe. Msosi hauliwi sana maana wengi huogopa unene. Baadaye sasa ulevi kichwani, keshawaka mtu, ndiyo kula vijimikate na hatimaye kutapika.

Kuona walevi wakitapika, hasa wanawake siku za wikiendi imekuwa sura na wajih mahsusi nchi hii miaka mingi.

Ni utamaduni au mila na desturi ambayo Waafrika wengi hatuizoei. Sisi tunaotoka makabila yenye desturi ya kula halafu ndiyo unywe , au kunywa na kula pamoja, kwa mfano Wachagga, hushindana na jadi hizi.

Sasa basi nilikuwa naelekea nyumbani saa za jioni ...kwenye saa mbili hivi. Nasema “jioni” (si usiku), shauri, msimu huu wa kiangazi, jua huwaka hadi saa tatu usiku. Tuseme mwangaza upo hadi saa hizo. Kiangazi kikipita, miezi ya Novemba kuendelea, kiza huingia mapema zaidi. Ikifika Februari au Machi, utajikuta uko gizani saa kumi alasiri. Ndiyo tofauti za kisayari na mazingira hizo. Jiografia ya Mungu Muumba.

“Nikishavunja vunja kichwa chako ntakitundika palee. Mtoto wa mbwa...!”

Matusi makali wanatukanana wale omba omba. Kando yao mtu, mkewe na watoto wao wawili mbele yangu wanasita kisha wanaendelea kwa tahadhari.

Omba omba wanne, mwanamke mmoja na wanaume watatu wamesimama mbele yetu, wameshika chupa za bia.

Mwenzao aliyewatukana kakaa chini, kitako, mbele ya hilo duka kubwa la Sainsurys.

Yeye ndiye anayeshusha matusi.

“Mnakuja hapa kunizuzua?”

“Muda tumekupa. Shauri yako kama unauharibu!”

“Nnauharibu, nnauharibu vipi wapumbavu nyinyi?”

“Una uharibu mwenyewe!”

Wanarushiana matusi. Kelele kubwa. Zinatisha.

Kisa baadaye ukichunguza kikoje?

Omba omba hupangiana mida za kukaa sehemu kuomba hela.

Ila na aghalabu wanakatazwa na serikali. Kawaida serikali husaidia watu wasiojiweza. Wasio na kazi au makazi. Huna kazi, unajiorodhesha ofisi kadhaa mijini, kufuatana na umbali wa unapoishi unapigiwa simu kazi inapopatikana. Kazi zipo. Kazi za kusafisha makazi. Kuzoa takataka. Kusambaza vikaratasi vya matangazo. Kuuza madukani au supamaketi. Sasa tatizo la jamaa wengi (hasa wenyeji) ni kutozipenda hizi kazi. Wanavizia tu fedha ya posho ya serikali inayotolewa kila juma – kisha wanaitumia kwa pombe na dawa za kulevya.

Kwa kuwa ulevi ni aghali baada ya muda huishia kuomba omba majiani.

“Msiwape fedha hawa jamaa. Serikali inawasaidia. Ukitaka kuwasaidia,” halmashauri za miji na askari huasa,”wape chakula au wanunulie chai.”

Omba omba atataka chai kweli?

Wee uulizwe unataka chai au bia, mpenda chang’aa na wiski, utachagua chai kweli?

Wengine ndiyo hao wavuta bangi.

Bangi aghali London. Bei ya chini kabisa ya majani haya makavu ni paundi kumi. Hizo ni kama Sh25,000. Aghali. Kwa hiyo paundi kumi unaweza kula misosi miwili ya kawaida vijihoteli vya bei nafuu vichochoroni.

Sasa wale omba omba wanachogombania nimekuja elezwa baada ya kuishi hapa miaka mingi ni mosi wanapigania sehemu za kukaa ili waombe. PIli, wanapigania pombe au bangi. Mmoja kamchukulia mwenzake pale alipoificha. Tatu, wanataka pia kulisha mbwa wanaowafuga. Mzungu na mbwa ni kama funza na kidole. Hata awe maskini. Hata awe omba omba, atamfuga, mwandani wake. Basi inakuwa mzozo.

Wakati nnapita nikiwazua hilo, akaja jamaa mmoja akasema zamani alikuwa akilala mitaani. Akagundua anacho kipaji cha kuandika mashairi. Siku hizi ajira yake ni fasihi. Anafundisha madarasa ya kuandika. Anatunga maneno kwa ajili ya matangazo ya biashara. Anasahihisha mitihani kwa wanafunzi toka nchi zisizo zungumza Kiingereza.

Kifupi aliyageuza maisha yake kuwa ya manufaa.

“Je, huo uomba omba uliunzia wapi?”

Jamaa anakwaruza koo.

“Nikiwa mtoto wazazi wangu waliachana. Baba alikuwa mvuta bangi. Mama hadi leo mtu wa sindano na unga. Nyumba ilikuwa vurugu tupu. Nikaachwa yatima. Nilikuwa na miaka tisa tu. Nikachukuliwa na serikali. Kule ilikuwa mateso ya watoto wengine waliokuwa wamefyatuka kunizidi. Nikiwa na miaka kumi na mbili nikatoroka. Nikishi mitaani. Nikakamatwa tena. Nikarudishwa. Ikawa hivyo hadi nilipobahatika kupata masomo.”

Zipo njia za kukwepa maisha haya Ulaya.

Tovuti: www.freddymacha.com