Wananchi washirikishwe vita dhidi ya uvuvi wa baruti nchini

Muktasari:

Licha ya maziwa, mito mikubwa na mabwawa yaliyopo nchini, Tanzania ina ufukwe wa Bahari ya Hindi wenye urefu wa kilomita 1,424 ambao unajumuisha Zanzibar, Tanga, Pwani, Dar es Salaam, Lindi na Mtwara. Kwenye maeneo hayo yote, uvuvi haramu umekuwa ukifanywa na wavuvi ambao hawajali madhara yatakayojitokeza kutokana na vitendo hivyo. Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kukomesha uvuvi huo ambao umekuwa ukiharibu mazalia ya samaki na kutishia kitoweo hicho kutoweka nchini hili licha ya mafanikio
haba yanayopatikana.

Uvuvi wa kutumia baruti athari zake kwa afya, mazingira na uchumi ni kubwa na unazidi kukithiri nchini hivyo kuhitaji mbinu mpya za kukabiliana nao.
Licha ya maziwa, mito mikubwa na mabwawa yaliyopo nchini, Tanzania ina ufukwe wa Bahari ya Hindi wenye urefu wa kilomita 1,424 ambao unajumuisha Zanzibar, Tanga, Pwani, Dar es Salaam, Lindi na Mtwara. Kwenye maeneo hayo yote, uvuvi haramu umekuwa ukifanywa na wavuvi ambao hawajali madhara yatakayojitokeza kutokana na vitendo hivyo. Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kukomesha uvuvi huo ambao umekuwa ukiharibu mazalia ya samaki na kutishia kitoweo hicho kutoweka nchini hili licha ya mafanikio
haba yanayopatikana.
Uchomaji wa nyavu zenye matundu madogo ni miongoni mwa hatua za kukabiliana na uvuvi haramu ambao umekuwa
ukitekelezwa maeneo mengi nchini. Licha ya juhudi hizi za ndani, Serikali inaungana na jumuiya za kimataifa kukabiliana na uvuvi wa kutumia baruti. Kwenye uvuvi huu, baruti hurushwa majini na mlipuko wake kuwaua samaki na viumbe wengine hai kabla wavuvi hawajawakusanya samaki
waliokufa ambao huelea juu ya maji.
Kwa kushirikiana na washirika wa kimataifa wa uhifadhi wa mazingira na fukwe za bahari kudhibiti uvuvi huo, vikundi vya
wananchi wanaokaa maeneo ya bahari viliundwa ili kuongeza nguvu.
Kutokana na jukumu la ulinzi kuvishirikisha zaidi vyombo vya Serikali, vikundi hivi havipati ushirikiano wa kutosha kufanikisha majukumu yao, hivyo kuzidisha matumizi ya vilipuzi kwenye uvuvi nchini.
Kiongozi wa kikundi cha utunzaji wa bahari na fukwe kutoka Mafia, Mussa Bahati anasema zipo changamoto za kiuchumi
na kiusalama ambazo Serikali ikizishughulikia wananchi watakuwa na nafasi kubwa na kuimarisha uvuvi salama.

“Tulipewa boti ya kufanyia doria usiku na Shirika la Uhifadhi Wanyamapori na Mazingira Duniani (WWF) ingawa kuna changamoto za gharama za uendeshaji. Siku nyingine tunapigwa au kutishiwa kuuawa na wavuvi haramu kutokana na kukosa ulinzi,” anasema Bahati.

Anasema endapo Serikali itasaidia kugharimia mafuta na kuweka askari polisi kwa kila boti, itakuwa rahisi kukomesha uvuvi huo. Anapendekeza, doria ifanyike muda wote.

Hoja ya ukosefu wa vifaa vya usalama kwa vikundi vya ulinzi inaungwa mkono na Diwani wa Kata ya Kimbiji, iliyopo Temeke jijini Dar es Salaam, Joseph Nyalandu akisema hana kifaa chochote ofisini kwake licha ya eneo lake kuwa miongoni mwa yanayoathiriwa na uvuvi wa baruti.

“Mtu akipiga baruti baharini mnamsikia lakini hakuna chombo cha kuweza kufuatilia. Ni vigumu kumaliza tatizo hili bila Serikali kuviwezesha vikundi vya ulinzi shirikishi,” anasema Nyalandu.

Kwa mujibu wa diwani huo, Jeshi la Polisi ndilo lenye boti ziendazo kasi ingawa askari wake hawafanyi doria maeneo yote, hivyo kutoa mwanya wa kuendelea kufanyika kwa uvuvi haramu.

Licha ya uchache wa askari hao ambao unasababisha doria isifanyike maeneo yote, taarifa zinaeleza nyakati za Uchaguzi Mkuu huwa mkazo unalegezwa. Ingawa inaweza kuwa ni kutokana na nguvu nyingi kuelekezwa kwenye usalama wa kampeni, wapo wanaoamini kwamba ni mkakati wa kupata kura kutoka kwa wananchi hao.

Utafiti uliofanywa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) mwaka 2012 ulibaini kutokea kwa hilo kwenye Uchaguzi Mkuu wa miaka ya 1995, 2000, 2005 na 2010.

Katika vipindi hivyo vya uchaguzi, maofisa uvuvi wa sehemu husika walilazimika kusimamisha doria kutokana na kukosa askari wa kushirikiana nao. Licha ya matukio muhimu kama hayo, baadhi ya wananchi wanapendekeza ushirikishaji mpana ili kuwanasa wahusika ambao wapo kwenye jamii.

Jamary Mfaume, mvuvi mdogo anasema anaamini kuna viongozi wanashiriki katika uvuvi haramu ndiyo maana inakuwa vigumu kukomesha vitendo hivyo viovu. Anasema hayo, kwa mtazamo wake kutokana na ukweli kwamba wahalifu wanafahamika ingawa hakuna anayewakamata wala kuwachukulia hatua yoyote.

“Huwa tunawaripoti wavuvi tunaoona wanatumia baruti, lakini wakikamatwa baada ya muda huachiwa na wakimgundua aliyetoa taarifa zao hukiandama chombo chake wakati anavua na kumrushia vilipuzi ili kumzamisha,” anasema Mfaume.

Hata hivyo, anasema Serikali inapaswa kuchukua hatua na ikiwezekana kulifungia Soko la Ferry kwa madai kuwa ndilo linaloongoza kwa biashara ya samaki waliovuliwa kwa baruti.

Kususia ununuaji wa samaki waliovuliwa kwa baruti ni suluhisho linalopendekezwa sehemu mbalimbali duniani. Taasisi ya kimataifa ya Endangered Species International (ESI) inayosimamia utunzaji wa viumbe vya habari inapendekeza suala hilo pia.

ESI inaamini endapo wananchi duniani kote watafahamishwa na kuepuka kununua samaki hao biashara hiyo itakufa na wavuvi kulazimika kufuata taratibu zinazopendekezwa kuendesha shughuli zao.

Mtaalamu wa afya na lishe, Sweetbert Shayo wa Hospitali Penisula jijini Dar es Salaam anasema ulaji wa samaki waliovuliwa kwa baruti unasababisha saratani na matatizo ya figo kutokana na kemikali zenye sumu zinazokuwamo kwenye baruti zinazotumika.

Maradhi hayo huweza kutokea kwa sababu mwili wa samaki hufyonza sumu iliyopo kwenye bomu baada ya kulipuka kupita kwenye mapafu au mwilini. Athari za sumu hiyo hutegemea imetengenezwa kwa mchanganyiko wa vitu gani.

Yapo mabomu yanayotengezwa kwa mchanganyiko wenye mbolea ya chumvichumvi, mafuta ya taa, baruti, na dongo au waterexplosive gel. Habari mbaya ni kwamba kemikali hizi huwa hazipotezi ubora wake hata baada ya samaki kupikwa kutokana na muda mfupi unaotumika kufanya hivyo.

Ingawa madhara ya samaki hawa hutokea baada ya muda mrefu, ulaji wa mara kwa mara humuweka mtumiaji kwenye hatari kubwa ya kupata maradhi ya saratani na figo.

Kumtambua wa baruti

Wavuvi, maofisa uvuvi wanawafahamu samaki waliovumiliwa kwa baruti na zipo dalili ambazo zinaweza kumsaidia mteja kufahamu kabla hajanunua samaki kwa matumizi ya familia yake. Inaelezwa mwili wa samaki huyo huwa umelegea, mifupa au miiba yake imetengana na nyama na hutokwa na damu katika matundu yote ya mwili wake.

Dalili nyingine ni mishipa ya damu iliyoko katika matamvua kupasuka, hivyo huvilia damu, utumbo wake kusagika na kutawanyika, bandama kupasuka na mwili kuacha tundu ukibonyezwa kwa kidole.

Athari

Licha ya madhara ya afya kwa mlaji, zipo athari za mazingira, ekolojia na uchumi wa wavuvi na taifa kwa ujumla. Watalaamu wa masuala ya uvuvi wanasema mabomu haya huathiri mazalia na malisho ya samaki.

Mabomu haya yakipigwa kwenye matumbao hufanya maisha ya samaki na viumbe vingine wa majini kukosa sehemu salama ya kuishi jambo linalowafanya wakose chakula cha uhakika na kutozaana, hivyo idadi yao kupungua kadri siku zinavyoenda huku uvuvi ukikithiri.

Baada ya mazalia hayo kuteketezwa, huchukua takriban miaka 100 kujengwa upya. Pamoja na hili, bomu huua samaki wadogo wasiofaa kwa matumizi, huharibu mayai yalikuwapo na kusababisha mmomonyoko wa fukwe kutokana na kukosekana kwa vizuizi vya mawimbi.

Madhara ya muda mrefu ni kukosekana kwa uendelevu wa sekta ya uvuvi kutakakosababishwa na kupungua kwa samaki. Hili likitokea, idadi ya wavuvi itapungua na kitoweo hicho pia.

Uwezekano wa kufungwa kwa viwanda vya kusindika samaki ni mkubwa, hivyo kuongeza upungufu wa ajira na kurudisha nyuma vita dhidi ya umaskini.

Mkurugenzi wa Shirika la Uhifadhi Wanyamapori na Mazingira Duniani (WWF) Tanzania, Amani Ngusaru anasema kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kuwa msatari wa mbele katika ulinzi wa rasilimali za bahari ili ziwe na manufaa endelevu kwa vizazi vijavyo.

“Waliotutangulia walikuwa makini na rasilimali hizi ndiyo maana nasi tuna nufaika nazo hivyo basi tunapaswa kuwa na matumizi endelevu ili kizazi kijacho kinufaike,” anasema Ngusaru na kuhadharisha endapo hatua stahiki zisipochukuliwa nchi itabakia na bahari yenye maji pekee.

Ofisa Mwandamizi wa Wizara ya Uvivi Upendo Hamidu anasema: “Serikali inashirikiana na wananchi wanaopiga vita uvuvi wa baruti lakini bado kuna changamoto kwani wanaofanya uvuvi huo siyo wavuvi wadogo.”

Hata hivyo, anasema kuna kamati ya vyombo vya ulinzi na usalama imeundwa na inafanya kazi kiintelijensia ambayo huenda ikapunguza tatizo hilo.