MBALAMWEZI YA KISWAHILI : Wanaodai fasihi simulizi imekufa wanapotosha

Muktasari:

  • Sayansi na teknolojia imekuwa ikikua na kusambaa hatua kwa hatua kote duniani mpaka wakati huu ambapo inaonekana kufikia upeo.

Fasihi simulizi ni tawi la fasihi ambalo huwasilishwa kwa hadhira kwa njia ya masimulizi ya mdomo. Hadithi, nyimbo, semi na sanaa za maonyesho ni tanzu za tawi hili la fasihi. Aidha, aina hii ya fasihi imekuwapo tangu karne nyingi zilizopita. Sayansi na teknolojia imekuwa ikikua na kusambaa hatua kwa hatua kote duniani mpaka wakati huu ambapo inaonekana kufikia upeo.

Baada ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia kujipambanua katika zana anuwai, kumekuwapo na mtazamo kwamba fasihi simulizi imekufa. Hoja inayotolewa ni kwamba, matumizi ya televisheni, redio na vyombo vingine yameingilia kati na kuwateka fanani na hadhira wa fasihi simulizi. Wanaoshikilia hivyo wanaona hakuna tena umuhimu wa fasihi simulizi katika jamii. Jambo kubwa linalorejelewa hapa ni kwamba; kwa wakati huu ambapo kuna vyombo vingi vya kimawasiliano kama simu, redio, televisheni, pia kuwapo kwa mitandao mbalimbali; watu ambao ndio fanani na hadhira (wa fasihi simulizi), wamekuwa wakijishghulisha zaidi na mitandao na vyombo hivyo na kuipa kumbo fasihi hususan simulizi.

Suala hilo halipaswi kutufanya tutoe hukumu kwamba fasihi simulizi imekufa au imepitwa na wakati. Wala hatupaswi kuifananisha fasihi simulizi na vyombo vya kimawasiliano. Laiti kungalikuwa na tawi jingine la fasihi limeibuka likachukua nafasi ya fasihi simulizi, pengine tungaliweza kunena hivyo. Ukweli ni kwamba, fasihi itabaki kuwa fasihi na vyombo vya kimawasiliano ni nyenzo za kurahisisha mawasiliano hayo.

Aghalabu wasemao fasihi simulizi imekufa au kupitwa na wakati huurejelea utanzu wa hadithi pekee. Hao hushikilia kuwa, kwa wakati huu hadithi hazisimuliwi tena na wala hakuna fanani wa kusimulia hadithi kama ilivyokuwa miongo kadhaa iliyopita. Kwa hakika, mawazo hayo ni potofu. Ikumbukwe kwamba hadithi si utanzu pekee wa fasihi simulizi. Hata hivyo, si kweli kwamba haditi hazisimuliwi tena. Katika baadhi ya jamii, hadithi husimuliwa na akina babu na akina bibi kama ilivyokuwa hapo zamani.

Aidha, nyimbo, semi na sanaa za maonyesho ni tanzu zinazotumika kwa kiwango kikubwa kama ilivyokuwa zamani au zaidi.

Wanafunzi wengi wanapoulizwa swali linalohusiana na fasihi kufa au kupitwa na wakati, wamekuwa wakilivamia swali hilo na hivyo kupoteza alama zote.

Hii ni kwa sababu wengi wanapojibu swali hilo hujiegemeza kuzungumzia utanzu wa hadithi pekee wakisahau kwamba kuna tanzu nyingine. Mbaya zaidi hata huo utanzu wa hadithi unaoshambuliwa kuwa umekufa; haujafa bali bado unaishi.

Mpendwa mfuatiliaji wa safu hii, fasihi simulizi inayatawala maisha yetu ya kila siku. Ukisikia wimbo unaimbwa iwe kanisani, kilioni, katika siasa na matukio mengine; hiyo ni fasihi simulizi.

Ukisikia ngoma inapigwa, ni fasihi simulizi. Ukiona maigizo, ni fasihi simulizi.

Kwa hiyo, mtazamo kwamba fasihi simulizi imepitwa na wakati hauna mashiko.

Hoja ya msingi ni kwamba, maendeleo ya sayansi na teknolojia yameiathiri fasihi simulizi. Kwa kusababisha upungufu wa fanani na hadhira.

Aidha, yamewafanya baadhi ya watu kupoteza mapenzi katika fasihi simulizi kutokana na muda mwingi kujihusisha na televisheni na mitandao.

Lakini kwa upande mwingine, vyombo hivyo vimekuwa nyenzo muhimu ya kusambaza fasihi simulizi kwa hadhira pana kwa wakati mmoja.

Mathalani, katika televisheni, babu anaposimulia hadithi kwa watoto wa shule, kila aliyetyuni kwa wakati huo, atasikia visa vitamu vya ngano zinazosimuliwa na fanani huyo na kupata ujumbe maridhawa.