Wanaokiuka sheria Zanzibar waadhibiwe

Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein

Muktasari:

  • Alisema vyombo vya ulinzi na hasa Jeshi la Polisi halipendi kuonea watu, lakini halina subira na watu wanaovuja sheria.
  • Huu ni ushauri mzuri wa mzazi kwa vijana na hasa akiwa kiongozi wa nchi kwa sababu sheria lazima zilindwe na kuheshimiwa. Kwa kufanya hivyo, kisingizio cha kuvunja sheria kinaondolewa.

Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein hivi karibuni amekuwa akiwatahadharisha watu wa Zanzibar hasa vijana juu ya hatari na athari za kutoheshimu sheria. Wakati akiwa Pemba alikutana na wananchi kwenye sherehe za kuadhimisha miaka 52 ya Mapinduzi na kuwaonya wanaovunja sheria kwamba mwisho wa siku watajikuta wamejiingiza katika matatizo.

Alisema vyombo vya ulinzi na hasa Jeshi la Polisi halipendi kuonea watu, lakini halina subira na watu wanaovuja sheria.

Huu ni ushauri mzuri wa mzazi kwa vijana na hasa akiwa kiongozi wa nchi kwa sababu sheria lazima zilindwe na kuheshimiwa. Kwa kufanya hivyo, kisingizio cha kuvunja sheria kinaondolewa.

Kama raia wanaiona sheria ni mbaya na haitendi haki kinachotakiwa ni kuilalamikia na kujenga hoja za kutaka ifanyiwe marekebisho.

Hata hivyo, tusisahau kwamba suala la kuheshimu sheria za nchi linamhusu kila raia na mgeni na huwa hazitarajiwi kubagua kati ya mkubwa na mdogo, tajiri na maskini au mapenzi ya mtu kwa chama cha siasa au klabu ya soka.

Tatizo lililopo Zanzibar na ambalo linaonekana kufumbiwa macho au kutopewa uzito unaostahili ni usimimizi wa sheria zilizopo.

Mwenendo huu umesababisha baadhi ya watu kuhisi kama vile Zanzibar wapo watu walio juu ya sheria na wana haki ya kuwapanda wenzao vichwani na kufanya watakalo.

Siyo mara moja wala mbili au tatu zimesikika taarifa za watu wakiwa katika baraza zao za mazungumzo kuvamiwa na kupigwa bila ya sababu.

Wapo walioumia na kutibiwa hospitali na katika matukio yote hayo hakuna hata mtu mmoja aliyekamatwa na kuwajibishwa kisheria kwa vitendo hivyo vya uhalifu.

Orodha ya matukio ya aina hii ni ndefu. Baadhi ya baraza zimevunjwa kwa kisingizio cha kutengeneza bustani wakati nyingine zilizopo karibu na hizo hazikuguswa.

Hapa inadaiwa pametumika utashi wa kisiasa na siyo sheria za nchi. Sote tunakumbuka matukio kadha ya waandishi wa habari wa Zanzibar kutishwa na hata kupigwa.

Vilevile, kituo kimoja cha redio kilichopo mjini Unguja kilivamiwa na hao tunaoambiwa ni wahuni na kutiwa moto, lakini hatujasikia waliofanya uhalifu huo kukamatwa.

Panapokuwapo hali kama hii mtu hubaki akijiuliza, hizi sheria za Zanzibar zinatakiwa ziheshimiwe na kikundi tu cha watu fulani na ni ruhusa kuvujwa na wengine?

Kama alivyosema Rais sheria lazima ziheshimiwe, lakini ulazima huo uwe kwa kila mtu na asiwapo mtu au kikundi cha watu kuonekana kuwa juu ya sheria.

Vilevile, ni muhimu kwa sheria kuonekana zinafanya kazi zilizosababisha zikatungwa kwa wanaotuhumiwa kuzivunja kuwajibishwa kwa haraka ipasavyo na Mahakama.

Hapa kwanza tukumbuke kwamba mtu anabaki kuwa mtuhumiwa, yeyote yule hastahiki kuhukumiwa na kutiwa adabu kama ni mhalifu mpaka anapotiwa hatiani na Mahakama.

Kwa hivyo, dhamana kwa mtuhumiwa kwa mashtaka mbalimbali isipokuwa machache, huwa haki ya mshtakiwa.

Masharti ya dhamana

Baadhi ya nyakati hutolewa masharti ya dhamana ambayo ni sawa na kumwambia mshtakiwa hana haki ya kupata dhamana.

Kwa mfano, tunasikia wenye haki ya kuweka dhamana ni watumishi wa Serikal. Kwa maana hiyo watu wa Zanzibar wamegawanywa katika mafungu, moja la watumishi wa Serikali na fungu la pili ni wale ambao hawafanyi kazi serikalini.

Hii siyo haki hata kidogo na haitoi sura ya mfumo mzuri wa sheria na utawala bora. Yamekuwapo malalamiko ya kuwapo kesi za kubuni na baadhi ya watu kusota mahabusu kwa miaka huku tukisikia upelelezi haujakamilka au upo mbioni kukamilishwa.

Hali hii inatia dosari utawala bora na waungwana wa masuala ya sheria wanakemea mwenendo huu kwa kutuaambia, “justice delayed is justice denied”, yaani haki ikikawia kutolewa ni sawa na kutotolewa kabisa.

Ili sheria zifanye kazi iliyokusudiwa na wananchi kuwa na imani na mfumo wa sheria ni lazima haki ionekane inatendeka na hakuna uonevu unaofanywa kutoka kwa mtu yeyote ndani na nje ya Mahakama.

Mtindo wa watu kuwa na ujasiri na kuamua kufunika nyuso zao kisha kupiga watu ovyo ni kinyume cha sheria na haukubaliki.

Maelezo kwamba wanaofanya hivyo ni wahuni na kwa hivyo watu wawapuuze hata pale migongo yao inapogeuzwa ngoma au nyumba zao kutiwa moto hayana mantiki na hayakubaliki.

Katika Kisiwa cha Pemba ulitokea uharibifu mkubwa wa nyumba kutiwa moto, mashamba ya watu kuvamiwa na mikarafuu mingi kukatwa.

Suala ni nani hasa waliohusika?

Mengi yanasemwa juu ya matukio hayo na kilichoshuhudiwa ni ukimya kama vile yaliyotokea ni mambo madogo.

Hawa wanasema hivi na wale wanasema vile na baadhi ya shutuma zinazosikika ni nzito na hazifai kupuuzwa.

Ni vizuri ili kuisafisha hali ya hewa na ukweli wa suala hili kujulikana ni vema ikaundwa tume huru, siyo ya Wazanzibari, kuutafuta ukweli pekee ili kuchunguza ni nani alihusika.

Kwa kufanya hivyo ndiyo kila mtu atakuwa na imani kwamba sheria za Zanzibar hazimbagui wala kumwonea mtu na yeyote anayezivunja hafumbiwi macho kwa kisingizio hiki au kile.

Wakati tunaadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi ambayo lengo lake ni kuweka hali za wananchi sawa na kuondoa ubaguzi au uonevu wa aina yoyote, ni vizuri kufanya tathmini juu ya namna sheria zinavyofanya kazi Visiwani.

Tathmini hiyo iwe na wigo mpana na isimalizie wenye sheria, bali hata namna ajira na nafasi za masomo zinavyotolewa na Serikali.

Jambo jingine ni suala la utoaji wa vitambulisho vya Mzanzibari. Hili linahitaji kuangaliwa kwa undani na kuwa na hadidu rejea zitazosaida kuondoa malalamiko juu ya utoaji wa vitambulisho.

Miongoni mwa mambo yanayotaka kuangaliwa kwa undani ni kwa nini mpaka leo maelfu ya watu ambao wao na wazazi wao wamezaliwa Visiwani na hawajawahi kutoka nje ya Zanzbar wananyimwa vitambulisho hivi?

Linaloshangaza ni watu waliohamia Zanzibar miaka ya karibuni na hawana makaburi ya wazazi wao Visiwani wanatamba na kuwa na vitambulisho na kuwa Wazanzibari zaidi kuliko wenzao waliozaliwa na kukulia.

Serikali ilikiri kwamba wapo watu wengi waliopewa vitambulisho kinyume cha sheria, lakini hatujasikia hata mmoja wao au waliovitoa kuwajibishwa kisheria.

Wakati umefika kwa kila jambo kuliangalia kwa pande zote mbili za sarafu na ikiwezekana hata kwenye ukingo wa sarafu badala ya kukurupuka kwa mmoja kumlaumu mwingine.

Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii. Anapatikana kwa baruapepe: [email protected] na [email protected]