Wanaume na roho ya kuona kwenye matatizo

Muktasari:

  • Aliyepanga akatembelewa na rafiki yake siku moja ili kumsaidia swahiba wake asiondoke na maumivu, alipovua viatu tu mlangoni akamwambia aingie navyo, kwa sababu wazee wa kazi wanaweza wakavichukua wakavitafutie miguu mingine.

Kuna wavulana wawili, mmoja ndiyo alikuwa anatoka nyumbani, kwenda kuanza maisha; kupanga chumba na kuishi kwa kujitegemea. Na mwingine alikuwa ni swahiba wa karibu wa huyu anayekwenda kuanza maisha ya kujitegemea.

Kupitia madalali, anayekwenda kuanza maisha akapata chumba maeneo ya hovyo mno, uchochoroni sana na usalama kiduchu. Yaani huko ukianika nguo inabidi ukae nje, uzisubirie hadi zikauke. Au Ukijaribu kupikia nje, hakikisha ukienda ndani kufuata chumvi unaingia na jiko lako, vinginevyo chumvi uliyoifuata inaweza kuwa ndiyo chakula chako kwa siku hiyo, yaani utakuta wezi wameshapitia sufuria, jiko na kila ulichokuwa unapika.

Aliyepanga akatembelewa na rafiki yake siku moja ili kumsaidia swahiba wake asiondoke na maumivu, alipovua viatu tu mlangoni akamwambia aingie navyo, kwa sababu wazee wa kazi wanaweza wakavichukua wakavitafutie miguu mingine.

Swahiba alipoingia ndani akaulizwa na mwenyeji wake, anapaonaje kwenye makazi mapya, akajibu ‘pametulia sana’ ingawa huenda nafsi na moyo wake haukuwa na uhakika na hilo la ‘kutulia sana’ hivyo muonekano wake ukashindwa kufanana na jibu.

Basi baada ya swali, swahiba wake akaanza kujihami kidogo, akaanza kumuelezea rafiki yake namna ambavyo atahama pindi tu kodi yake itakapofika ukomo na sababu kubwa ikiwa ni tabia ya wizi katika eneo hilo— tena akamtolea mfano jinsi ambavyo angeondoka peku kama angethubutu kuacha viatu nje. Ajabu ni kwamba kwa mwenzake hilo halikuwa tatizo, badala yake aliona fursa katika hilo.

“Hiyo nd’o safi mbona,” akamjibu na kuongeza: “Hiyo hata ukija na demu hapa, majirani zako hawawezi kujua kwa sababu si lazima viatu uingize ndani. Labda wamuone wakati anaingia.”

Wanaume karibu wote tuko na ushetani huu linapokuja suala la uzinzi tunaona fursa katika kila jambo. Kombe la Dunia litaanza mwezi wa sita na watu watalitumia kuwazunguka wenza wao, watasema wanakwenda kutazama mechi ya Brazil na Ureno.

Kuna wengine hata hizi mvua za mfululizo zinazonyesha wanazitumia kama fursa ya uzinzi. Kuna ambao wakiwa ofisini wanatuma meseji kwa wake zao kuwa kesho kuna kikao ofisini, na kutokana na mvua, akitokea nyumbani kama kawaida anaweza kuchelewa, hivyo bora atafute sehemu ya karibu, apumzike ili awahi kikao— wanaume tunajua kutembea na fursa.

Wengine kutokea ofisini wanapiga simu nyumbani kwamba hawataweza kurudi kwa sababu barabara zimemezwa na maji, hakuna gari zinazopita. Na wenye propaganda za namna hii huwa wanajipanga kweli kweli. Wanajua wanawake wa siku hizi wajanja, wanaweza wakaomba picha za barabara iliyojaa maji — kwa hiyo na wao wanakuwa wameshajipanga, hawashindwi kuwatumia wake zao meseji za mafuriko yaliyoziba njia ya mwaka jana.