Friday, July 21, 2017

KUTOKA LONDON : Wanaume wanaozaa na wimbi la jinsia mseto uzunguniFreddy Macha

Freddy Macha 

By Freddy Macha

Maisha Ughaibuni huwa ya vioja na upya.Miaka mingi nimeelezea namna nilivyoonywa na maaskari nikiwa Ujerumani. Nilimrushia tofali mbwa aliyekuwa na tabia ya kujisaidia nje ya nyumba niliyoishi. Wanyama wanaofugwa Uzunguni hususan mbwa na paka, husajiliwa. Si kawaida hata kidogo kumkuta mbwa au paka koko asiye na mwenyewe.

Kinyume na Afrika, mbwa akikutwa anazagaa zagaa atatafutiwa askari achukuliwe kwa mhusika. Wahusika wanapotembea na mbwa huwa na mkanda shingoni. Mbwa akiwa mkali, akiacha kinyesi ovyo njiani, wajibu ni wa mmiliki wake.

Shingoni, paka na mbwa wana kidude chenye anuani na habari nyingine maalum zinazowekwa katika kompyuta ya kiserikali. Kama ambavyo wananchi tulivyoorodheshwa tunapoishi , tarehe za kuzaliwa nk.

Ni kawaida kabisa kukuta matangazo pembe za barabara, yakilia kupotea mnyama fulani. Zawadi hutolewa ukimwokota. Kila mtu atazingatia jambo kama hilo, linalofanana na mwanadamu kupoteana na ndugu zake.

Tukiendelea na mada hebu tudokeze kisa cha mwanaume kujifungua mtoto wiki jana. Kidesturi mahusiano ya jinsia moja yamekuwa kawaida jamii za Kizungu. Bado wapo wapinzani wachache kama mkuu wa Ujerumani Angela Merkel aliyepinga kupitishwa sheria ya ndoa za jinsia moja lakini akashindwa kwa kura serikalini. Mambo ya jinsia moja yameshatandaa. Ipo mikahawa, baa na mahoteli yao; pia vitengo maalum vya polisi vilivyoundwa na serikali kutetea. Ila jipya ni kuendelea kukua kwa watu wasiotaka kuitwa wanaume au wanawake. Sidhani neno hili limo kamusi za Kiswahili.

Leo hati mbalimbali za kitaifa zinakataza kuwagawa wananchi mafungu mawili tu. Unapojaza fomu sehemu nyingi unaulizwa wewe mwanamke, mwanaume au jinsia iitwayo “transgender” kwa kimombo.

Kwa vipi?

Wapo wanaozaliwa wakakua wakijisikia si sawa. Mfano mzuri ni wanaume wawili waliopata mimba karibuni. Wa kwanza, Hayden Cross, alizaliwa msichana, akadai akiwa mtoto alicheza na wavulana na kufanya mambo ya kiume zaidi. Alipofikia utu uzima ( ana miaka 21) alianza kutumia dawa za kumgeuza kabisa mwanaume. Sasa akataka kuzaa. Akanunua mbegu mtandaoni, akapostiwa kwake na kujipiga sindano mwenyewe.

Wapo wanaume wanaofanya biashara kuuza mbegu zao. Huwa hawataki watoto watakaozaliwa wawajue. Hayden ameshazaa mtoto wa kike na ingawa ana matiti na vitu vya kike, ameamua kuvisimamisha kwa sindano na dawa.

Swali linaloulizwa ni je mtoto akikua? Anasema atamweleza ukweli.

Mwenzake, Scott Parker ni mja mzito. Pia alizaliwa msichana akatumia dawa kujigeuza mwanaume.

Mambo haya ya wanadamu kujibatili Uzunguni yanapingwa na hasa wanadini.

Yamo vile vile katika vyakula.

Tanzania sasa hivi imeanza kuingiza ubatilishaji kutumia mtindo unaoitwa GM (“Genetically Modified”) kwa neno la kitaalamu. Maana yake ni mbegu za mmea hazikukuuzwa kiasilia. Ubatilishaji huu unaofanya nafaka na mimea kuwa kubwa au haraka, una mintaarafu kunufaisha wafanyabiashara unaathiri afya na hata kulemaza watoto. Unga unaotengenezwa Afrika Kusini (kwa GM) unaoitwa “Iwisa” unapendwa sana na Waafrika Majuu. Ila pamoja na kuishi Uzunguni wengi hawafahamu au kuzingatia athari za GM.

-->