Wapiga kura kiduchu, tatizo linaloweza kukomeshwa

Muktasari:

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kumekuwa na mwitiko mdogo wa wananchi wanaojitokeza kupiga kura katika chaguzi ndogo, ukilingananisha na idadi ya watu walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapigakura.

Katika siku za karibuni Watanzania wameendelea kushuhudia idadi ndogo ya wapigakura ikijitokeza katika uchaguzi, hususan chaguzi ndogo wa wabunge na madiwani unaofanyika kwa nyakati tofauti katika sehemu mbalimbali nchini.

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kumekuwa na mwitiko mdogo wa wananchi wanaojitokeza kupiga kura katika chaguzi ndogo, ukilingananisha na idadi ya watu walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapigakura.

Hali hiyohiyo imejitokeza safari hii katika uchaguzi mdogo wa ubunge katika majimbo ya Kinondoni na Siha Februari 17, ambako wagombea wa CCM, Maulid Mtulia- Kinondoni na Dk Godwin Mollel-Siha waliibuka washindi. Katika Jimbo la Kinondoni kati ya wapigakura 264,055 waliojiandikisha ni 45,454 pekee ndiyo waliojitokeza kupiga kura. Hii ni sawa na asilimia 17.2.

Hali ilikuwa tofauti kidogo kwa Siha ambako kati ya watu 55,313 waliojiandikisha waliojitokeza ni 32,277, sawa na asilimia 42.1.

Kutokana na hali hiyo, hata kura alizopata mshindi wa uchaguzi katika Jimbo la Kinondoni, Mtulia, zilipungua kutoka 70,337 mwaka 2015 hadi kura 30,247.

Idadi hiyo ya kura za Mtulia ni chini ya nusu ya zile alizopata katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 wakati huo akiwa CUF na kuungwa mkono na vyama vya Ukawa, dhidi ya kura za mpinzani wake wa CCM wakati huo, Idd Azzan aliyepata kura 65,964.

Kwa upande wa Siha, Dk Mollel wa CCM alitangazwa mshindi baada ya kupata kura 25,611 ikiwa ni zaidi ya kura 2,865 ya kura 22,746 alizopata akiwa Chadema mwaka 2015.

Hali hii ni wakati huu pekee, Machi 16, 2014 katika uchaguzi mdogo wa Kalenga mkoani Iringa kati ya watu 71,964 waliojiandikisha kupiga kura, waliojitokeza ni 29,541 (asilimia 41); Vivyo hivyo ikawa katika uchaguzi mdogo wa Chalinze mkoani Pwani ambako kati ya watu 92,000 walioandikishwa 24,422 ndio waliopiga kura, sawa na asilimia 26.5.

Si chaguzi ndogo pekee zinazoathiriwa na idadi ndogo ya wapigakura, pia uchaguzi mkuu wa rais, wakati mwingine unakumbwa na hali hiyo. Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 watu milioni nane pekee walipiga kura kati ya milioni 21 waliojiandikisha.

Katika uchaguzi Mkuu uliopita mwaka 2015, kati ya wapiga kura milioni 23.2 walioandikishwa, waliojitokeza kupiga kura walikuwa milioni 15.

Hali hiyo inaelezwa na wadau wa masuala ya siasa kuwa ni tatizo la Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na wanapendekeza namna ya kuondokana nalo.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, wadau hao wanasema wananchi wengi wanakosa imani na Tume hiyo na kukata tamaa, hivyo kushauri tume hiyo kujenga mazingira ya kuaminika kwa kuongeza uwazi na kutoa uamuzi usiopendelea chama chochote.

Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CUF, Abdul Kambaya anasema kinachojitokeza ni wananchi kukata tamaa hasa kwa matendo yanayotokea kabla na baada ya uchaguzi.

“Ikifika wakati wananchi wanasema hata ukienda kupiga kura mshindi anajulikana, huwezi kuwaona wapigakura wakijitokeza, haiwezekani uchaguzi wa kata 43 CCM ishinde zote, majimbo matatu ishinde yote, majimbo mawili ishinde yote,” alisema.

Anasema ili kurejesha imani ya wapigakura ni lazima kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi ambayo wananchi watakuwa na matumaini nayo.

“Tukiwa na Tume Huru, wananchi wakawa na imani kwamba wanayemchagua ndiye mshindi, vurugu hazitakuwapo,” anasema.

Mwanasiasa hiyo anasema pia mikutano ya hadhara ya kisiasa ikiruhusiwa kama inavyotaka sheria ya vyama vya siasa, itatoa fursa kuwapa wananchi elimu wapiga kura ili waweze kutambua thamani ya kura zao.

Dhana hiyo inaungwa mkono na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Damian Shumbusho ambaye mwaka 2012 alifanya utafiti kujua kwa nini wananchi wengi hawajitokezi kupiga kura na kushauri mambo ya kufanya, ikiwamo kutoa elimu ya mpiga kura ikaeleweka.

Anasema mwananchi asipotambua thamani ya kura yake kwa kiongozi anayekwenda kumchagua anaweza asijitokeze kupiga kura. Anasema, “Jukumu la kutoa elimu kwa mpiga inapaswa kutolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi na si kuviachia vyama vya siasa. Pia, itolewe mapema badala ya kusubiri siku 20 kabla ya kupiga kura.

Shumbusho anaungwa mkono na msomi mwenzake wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Benson Bana ambaye pia amewahi kufanya utafiti kupitia taasisi ya kuangalia uchaguzi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Temco) kuhusu tatizo hilo na kubaini sababu kadhaa.

Mara tu baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Temco ilitoa taarifa yake ikieleza kuwa mwitikio wa wapiga kura ulikuwa wa chini kwa kiasi cha kushtusha ikilinganishwa na chaguzi zilizopita hasa kutokana na wapiga kura kuchoka, vikwazo vya kisheria kuhusiana na vituo vya kupigia kura, upotevu wa kadi za kupigia kura na pengine kuuza na kununua kadi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, waangalizi wa Temco walidadisi sababu za viwango vya upigaji kura kuwa chini hivyo na kujumuisha sababu hizo katika mafungu matano.

Mosi, ile kanuni kwamba kila mtu atapiga kura katika kituo alichojiandikisha inawanyima wahamahamaji fursa ya kupiga kura. Kwa mfano, katika sehemu za wafugaji, wapigakura walioandikishwa wanaweza kuwa mbali na vituo vyao siku ya uchaguzi wakitafuta malisho ya wanyama wao, na hawaruhusiwi kupiga kura katika vituo vilivyo karibu na pale walipo.

Pili, watu wengi wanatembea na kadi za kupigia kura mifukoni wakizitumia kama kitambulisho katika shughuli nyingi. Kwa hiyo zinaweza kupotea au kuharibika haraka.

Tatu, watu kutokuyakuta majina yao katika orodha ya wapiga kura iliyobandikwa kituoni. Wale ambao hawakupata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa maofisa wa uchaguzi waliondoka na kurudi nyumbani bila kupiga kura.

Nne, kukosekana elimu ya uraia na ya wapigakura inayotosheleza. Licha ya Tume za uchaguzi kutoa elimu ya wapigakura zikisaidiwa na vyama vya wananchi na vyombo vinginevyo, nchi ni kubwa (hasa Bara) na si rahisi kuwafikishia watu wote elimu hiyo.

Tano, ununuzi wa kadi za wapigakura ili kupunguza kura za wapinzani. Hili si jambo jipya, lakini lilifanyika kwa kiwango cha juu. Huko nyuma utaratibu ulikuwa kununua na kuziharibu; lakini kwa sababu sasa zinatumika kama kitambulisho kwenye shughuli nyingi, utaratibu unaokubalika ni kuzichukua na kuziweka kadi hadi uchaguzi upite. Wale wanaokubali kuzitoa kadi zao wanalipwa kiasi wanachokubaliana na wale wanaozichukua.

Kabla ya uchaguzi huo, Aprili 2014 aliyekuwa Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva alisema pamaoja na sababu nyingine, mojawapo ni kutoboreshwa kwa daftari la wapigakura.

Sababu nyingine alisema ni za kiuchumi. “Hali ngumu ya kiuchumi inaweza kusababisha watu washindwe kwenda kupiga kura na badala yake wanaenda kufanya shughuli zao za kujipatia kipato.”

Alisema namna ya kuondokana na hilo ni kutoa elimu kwa wananchi ili waelewe kwamba kutojitokeza kupiga kura wanapoteza haki zao za kuchagua viongozi wanaowataka.

Hadi sasa NEC inasema mwitikio wa wapigakura wakati wa uchaguzi mdogo hutofautiana na wakati wa uchaguzi mkuu, kama anavyosema naibu uratibu uendeshaji uchaguzi wa NEC, Irene Kadushi.

Kadushi anasema kitendo cha watu kuhama chama kimoja na kisha kuruhusiwa kugombea nafasi ileile katika chama kingine nacho kimechangia kujitokeza idadi ndogo ya wapigakura kwenye uchaguzi mdogo wa Februari 17.

Bosi huyo wa uchaguzi wa NEC anasema muundo wa Tume hiyo unachangia wananchi kuwa na mtazamo kuwa wateule wa Serikali wanaosimamia uchaguzi ngazi za chini wanakipendelea chama tawala.

“Hii imepelekea sisi kuomba tupatiwe ofisi kwenye kanda mbalimbali hapa nchini, jambo litasaidia pia katika utunzaji wa vifaa vyetu vya kazi.

Pia, anasema Tume hiyo inataka iwe na uwezo wa kuajiri wafanyakazi hasa wasimamizi wa uchaguzi, hali itakayoiongezea kuaminika kwake kwa wadau.

“Kikubwa ni watu waongeze uaminifu wao kwa Tume ambayo imekuwa ikifanya kazi kubwa, kwani hata nchi ambazo tume zake zinaonekana ziko huru na haki bado zinalalamikiwa kwa mambo kadha wa kadha.”

Kuhusu uhuru wa Tume, Kadushi anasema, “Miaka ya nyuma tulikuwa na changamoto ya fedha katika kutoa elimu ya mpigakura lakini tatizo hilo limepatiwa ufumbuzi wa kutosha na sasa elimu ya mpigakura ni endelevu.”

Je, Serikali inaingilia Tume ya Uchaguzi? Akijibu madai hayo, Kadushi anasema, “Hakuna taasisi yoyote inayoiingilia NEC katika utendaji wake ikiwemo Serikali ambayo jukumu lake huishia kwenye kuipatia Tume fedha kwa ajili ya shughuli zake.”