Wapinzani: tutapambana mpaka dakika ya mwisho

Muktasari:

  • Harakati za kudai kurejeshwa mfumo wa vyama vingi zilipamba moto mwaka 1991 na kusababisha kubadilishwa kwa Katiba ili kurejesha mfumo huo ambao ulikuwa umefutwa Januari 14, 1963 kwa Azimio la Halmashauri Kuu ya Tanu.

Tanzania ilirejea katika mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992, kipindi ambacho kilikuwa muhimu na cha mafanikio kwa wanaharakati wa mageuzi.

Harakati za kudai kurejeshwa mfumo wa vyama vingi zilipamba moto mwaka 1991 na kusababisha kubadilishwa kwa Katiba ili kurejesha mfumo huo ambao ulikuwa umefutwa Januari 14, 1963 kwa Azimio la Halmashauri Kuu ya Tanu.

Hapo ndipo ukawa mwanzo wa kuanzishwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa yenye jukumu la kusajili vyama hivyo na kuhakikisha vinafuata sheria.

Matukio ya hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na vyama vya upinzani kutopata fursa ya kufanya siasa wakati wote bila kujali vikwazo na changamoto zilizopo kumeviibua vyama hivyo na kuanza kuhoji wapi Taifa linaelekea.

Hoja ya vyama hivyo imejikita katika tamko la Serikali kupiga marufuku shughuli za vyama vya siasa ikiwamo mikutano ya hadhara na maandamano.

Wakati suala hilo likivitesa vyama hivyo, viongozi walioshika nafasi kubwa za ubunge na udiwani wanatangaza kujivua nyadhifa zao na kuhamia chama wanachoona kinawafaa, huku vyama vya upinzani vikiathirika zaidi na wimbi hilo.

Wapo waliojiunga ama na CCM, NCCR-Mageuzi, CUF au Chadema. Lazaro Nyalandu, aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini alijiuzulu na kujivua nyadhifa zake zote ndani ya CCM na kubainisha kwamba ameamua kuhamia upinzani ili kuongeza nguvu ya kupigania demokrasia, kupambana na ukiukwaji wa haki za binadamu, dhuluma na kupigania Katiba Mpya.

Wakati Nyalandu akiibua madai hayo, waliohamia CCM kutoka vyama vya upinzani wanasema wanamuunga mkono Rais John Magufuli kwa maelezo kuwa anatekeleza aliyoyaahidi kwa wananchi sambamba na madai ya hoja ya ufisadi kukosa nguvu.

INAENDELEA UK 26

INATOKA UK 25

Uamuzi wa Nyalandu ni kama ulizima mtikisiko uliotokea mkoani Arusha baada ya baadhi ya madiwani wa Chadema kujivua nyadhifa zao na kumuunga mkono Rais Magufuli.

Madiwani waliojiengua ni Solomon Laizer (Ngabobo), Credo Kifukwe (Murieti), Anderson Sikawa (Leguruki), Emmanuel Mollel (Makiba), Greyson Isangya (Maroroni) na Josephine Mshiu (viti maalumu).

Wengine waliotimka Chadema ni waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha ambaye alihama CCM mwaka 2015 wakati wa wimbi lililomfuata aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.

Aliyekuwa mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chadema (Bavicha), Petrobras Katambi na wanachama wa zamani wa ACT Wazalendo, Albert Msando, Samson Mwigamba na Profesa Kitila Mkumbo nao walikihama chama hicho na kujiunga na CCM.

Pia, katika wimbi hilo yupo kada wa Chadema, David Kafulila alikihama chama hicho na kutangaza kujiunga na CCM na kufuatiwa na aliyekuwa mbunge wa Kinondoni kwa tiketi ya CUF, Maulid Mtulia, mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira na aliyekuwa mbunge wa Siha, Dk Godwin Mollel.

Madai ya siasa za ushindani

Wapo wanaosema mazingira ya kufanya siasa yamebadilika katika kipindi hiki cha wabunge kuvihama vyama vyao jambo ambalo Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Danda Juju analipinga na kubainisha kuwa wakati huu ulipaswa kuwa na siasa za ushindani kutokana na kufanyika chaguzi tano zinazovihusisha vyama vingi.

Huku akisisitiza kuwa mapambano ni lazima yaendelee na kwamba vyama vya upinzani havitokata tamaa hadi dakika ya mwisho Juju anasema, “ninayoyashuhudia sasa ni dhamira ya dhati kuwa Serikali inataka kunyonga upinzani kitu ambacho ni kibaya.

“Kuna matukio ya wabunge na wanasiasa kuwekwa ndani kitu ambacho hatujazoea kukiona siku za nyuma.”

Taasisi za Serikali

Anasema wakati umefika kwa vyama vya siasa, Tume ya Uchaguzi (NEC), Msajili wa Vyama vya Siasa, taasisi za haki za binadamu wadau wa maendeleo na wawakilishi kutoka serikalini kukutana na kuzungumzia hali iliyopo sasa katika uwanja wa kufanya siasa na kuminywa kwa demokrasia.

“Ukitazama kwa umakini utaona jinsi ambavyo Bunge limenyamazishwa. Mfano, Msajili wa Vyama vya Siasa jukumu lake ni kuvikagua, kuvisimamia vyama vya siasa na kuhakikisha vinatekeleza majukumu yake ya msingi ya kikatiba, ila wakati huo huo anashindwa kukemea vyama hivyo vikizuiwa kufanya siasa,” anasema Juju.

Akiwagusia wakurugenzi wa halmashauri, Juju anasema viongozi hao wamekuwa wakisimamia chaguzi mbalimbali wakati ikijulikana kuwa ni makada wa CCM, jambo alilodai kuwa haliwezi kuleta usawa katika chaguzi husika.

“Hawa ni wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM unadhani wanaweza kutenda haki kweli katika kusimamia uchaguzi. Kama hatutokemea mambo yanayoendelea sasa hakika uchaguzi mkuu ujao tusitegemee miujiza,” anasema.

Anafafanua kuwa iwapo mihimili yote ya Dola itashindwa kusikiliza kilio cha vyama vya upinzani na kuwakamata viongozi wake, wanachama wa vyama hivyo wataendelea kudai haki yao ya kikatiba.

“Madhara yake ni wapinzani kususia uchaguzi na kushtaki kinachoendelea katika jumuiya ya madola. Hii itaifanya nchi yetu kuingia katika orodha ya nchi zilizodhoofika kwa sababu ya kuminya demokrasia,” anasema.

“Ili Tanzania iendelee kuwa na amani lazima Serikali ikubali demokrasia ya kweli yenye misingi ya kuheshimu katiba na kanuni.”

Anasema ni jambo la kushangaza kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kukiagiza chama kuorodhesha idadi ya wanachama wake, wakati huohuo akichochea mgogoro na kutolea mfano mvutano wa uongozi unaokikabili Chama cha Wananchi (CUF).

“Anashindwaje kuzingatia na kusimamia Katiba ya nchi, sheria ya vyama vya siasa na sheria ya Jeshi la Polisi zinazotoa haki kwa vyama vya siasa kufanya shughuli zake,” anasema.

Anasisitiza, “daraja likivunjika mbinu za kuvuka daraja lazima uzipate ukiwa katika daraja husika. Tuna harakati tunapanga ila hatuwezi kusema kila kitu.”

Katibu Mkuu wa Chama cha National League for Democracy (NLD), Tozi Matwange anasema, “kuzuia mikutano ya hadhara ni kukiuka haki za binadamu na kuvunja Katiba ya nchi inayoruhusu mfumo wa vyama vingi.”

Akizungumzia kauli ya kuzuia mikutano ya hadhara mpaka mwaka 2020 huku wanaoruhusiwa kufanya mikutano wakiwa ni wabunge na madiwani katika maeneo yao anasema, “mfano mimi nina diwani mmoja tu nchi nzima ina maana nifanye siasa katika kata tu si sawa.

Lawama kwa CCM

“Ni ajabu maana CCM kinaendelea kufanya siasa kupitia mwenyekiti wake, mawaziri, wabunge na wakuu wa mikoa. Sisi wengine tumefungwa kamba. Huo ni ukiukwaji wa haki za binadamu na kuvunja mfumo wa vyama vingi.”

Anasema licha ya kuwepo kwa jambo hilo, wapinzani wataendelea kupiga kelele kwa kile anachofafanua kuwa Serikali ni ya watu, ipo siku itawasikia.

“Ipo siku watatuelewa tu na kuacha mfumo wa vyama vingi kufanya kazi kama inavyopaswa iwe. Ni hatari sana kwa CCM kwenda pekeyake bila upinzani. Tunazuiwa kwa sasa lakini uchaguzi ukikaribia watatuachia na hapo ndipo tutakapoweka mambo hadharani, wananchi watatuelewa maana watajua hatukusema kwa sababu tulizuiwa,” anasema.

Akizungumzia wabunge wa upinzani kuhamia CCM, Katibu Mkuu huyo wa NLD anasema ni jambo la kawaida kwa maelezo kuwa baadhi ya waasisi wa vyama vya upinzani wamefariki dunia, lakini vyama hivyo bado vipo mpaka sasa.

“Upinzani haupo kwa wabunge na vyama, upinzani upo kwa watu. Wananchi wasipate shida tuendelee kuwa pamoja kupigania mabadiliko,” anasema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi (CUF), Julius Mtatiro anagusia msimamo uliotolewa na vyama vinavyounda Ukawa kuhusu uchaguzi wa kata 43, kwamba haukuwa huru na haki na uliambatana na vitendo vya kuminya vyama vya upinzani.

Uchaguzi wa marudio wa kata

Katika uchaguzi huo, CCM kilishinda katika kata 42 huku upinzani ikiambulia kata moja tu, jambo ambalo liliwakutanisha viongozi wakuu vyama vinavyounda Ukawa; NLD, Chadema, NCCR-Mageuzi na CUF kujadili na kutoa tamko la pamoja, likiwemo la kususia uchaguzi mdogo wa ubunge wa Januari 13, mwakani iwapo changamoto zilizojitokeza katika uchaguzi huo hazijafanyiwa kazi.

“Tulipokaa Ukawa tulijadili matatizo yaliyojitokeza katika kata 43. Tunajua Tume ya Uchaguzi imekuwa ikipendelea chama kimoja ila uchaguzi wa kata hizo ulikuwa tofauti sana na chaguzi nyingine. Huu tuliminywa zaidi,” anasema Mtatiro.

“Wapinzani tumeshinda kata zaidi ya 10 ila washindi hawakutangazwa, mawakala wa upinzani walinyimwa fomu za kuwatambulisha kuwa ni mawakala ambazo zinatolewa na wasimamizi wa uchaguzi. Kumetokea mazingira ambayo hatukuyazoea.”

Mtatiro ambaye katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 aligombea ubunge katika jimbo la Segerea anasena, “kushiriki kwetu katika uchaguzi wa Januari 13 inategemea Serikali na Tume ya Uchaguzi watatusikia kwa namna gani maana tumetaka tukae na kujadiliana kuhusu kilichotokea katika uchaguzi wa kata 43.”

“Ikiwa hawatatusikiliza na wakaendelea na uchaguzi huu kwa kutupuuza maana yake wanatuambia tuchukue hatua zaidi ambazo tutazichukua. Ila hatua ya sasa msimamo ni kutoshiriki huo uchaguzi. Baadaye tutafanya uamuzi mwingine maana wataalam wetu wanaendelea na vikao na watafikia muafaka.”