Wapinzani wamejiweka katika mkondo wa maji

Muktasari:

Kusema ukweli ni msingi muhimu wa maadili hata katika siasa na ndiyo miongoni mwa miiko ya wana- CCM ni ule unaosema, “nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko.”

Maadili ya dini zetu – Uislamu na Ukristo na hata maadili ya mila zetu za asili na vilevile utamaduni wa Kitanzania – yote yanahimiza kusema ukweli. Hata maadili ya taaluma mbalimbali, mfano uandishi wa habari pia yanahimiza kusema ukweli.

Kusema ukweli ni msingi muhimu wa maadili hata katika siasa na ndiyo miongoni mwa miiko ya wana- CCM ni ule unaosema, “nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko.”

Hata hivyo, licha ya umuhimu huo wa kusema ukweli daima ni muhimu vilevile kutafuta namna sahihi ya kuusema na kufikisha ujumbe, hasa katika uchaguzi wa matumizi ya lugha. Hii inaitwa busara au hekima.

Katika Uislamu kuna aya moja ya Qur’an inaagiza Waislamu wawahubirie watu wengine wasiokuwa Waislamu kwa hekima na mawaidha mema, na wakati huohuo ikionya kuwa usitumie lugha chafu kwa miungu wanaoaminiwa na hao unaowahubiria, na wao watarudisha lugha chafu kwa Mungu wako ambaye ndiye Mungu wa kweli.

Hii ni kuonyesha umuhimu wa hekima inayojidhihirisha katika lugha nzuri unayotumia, katika kukosoa na kufikisha unachoamini, kuwa ni kweli. Na ndiyo maana katika Biblia Mithali 4: 6 - 7 imeandikwa; “Usimwache hekima naye atakuweka salama, mpende, naye atakulinda. Hekima ni bora kuliko vitu vyote, kwa hiyo jipatie hekima.”

Ukweli na matokeo hasi

Katika ukweli wako unaotaka kuusema, usipotumia lugha sahihi kutokana na mazingira husika, unaweza kupata matokeo hasi badala ya matokeo chanya unayoyatarajia. Katika hali ya sasa ya mazingira ya kisiasa, somo la njia sahihi ya kuufikisha ukweli linawahusu wapinzani wa Serikali, hususan wabunge wa CUF na Chadema.

Nasema hivi kwa sababu katika sakata la makinikia, vyama vya upinzani vimekuwa vikijididimiza vyenyewe kwa sababu ya namna mbaya wanayotumia kuufikisha ‘ukweli wao’ katika mazingira ambayo suala la makinikia limempandisha chati Rais John Magufuli na kuonekana shujaa mkuu.

Ukiwauliza Watanzania wengi hivi sasa watakujibu Rais Magufuli ni mzalendo, mpiganaji na hata ni masiha wa kisiasa ambaye amekuwa akisubiriwa muda mrefu kulikomboa Taifa. Haijalishi kama mtazamo huo ni kweli au uongo, muhimu ni kuwa wananchi wengi wanaamini hivyo na haya yanaeleza kuhusu mfanikio ya Rasi Magufuli kisiasa. Na hapa nikizungumzia mafanikio ya kisiasa ninamaanisha kuwa ni kupata uungwaji mkono kuliko wapinzani wako.

Rais Magufuli ‘smart’ kisiasa

Rais Magufuli kisiasa yuko vizuri na anajua jinsi ya kucheza na hisia za watu kupata uungwaji mkono, kiasi kwamba watu hadi wanaamua kufumbia macho changamoto nyinginezo za Serikali yake.

Katika jambo kubwa ambalo Magufuli amefanikiwa ni kuteka hisia za huruma za watu kwa kujiwasilisha kwao kama kiongozi mwenye uchungu na nchi yake na watu wake, na kama Mchamungu.

Pia, Rais Magufuli ameweza kujiwasilisha kama mtu aliyejitoa mhanga, aliye tayari kufa kwa ajili ya kutetea Taifa lake kuliko kuuza nafsi yake kwa mafisadi ambao wanahangaika kumhonga.

Katika hotuba zake, Rais Magufuli ameweza kuwatweza watu wakubwa walioonekana kuwa wana nguvu za kisiasa, hata wanaodaiwa kuwa ni marafiki zake, akitekeleza falsafa yake ya kutumbua majipu. Mambo haya yamemfanya apate umaarufu mkubwa miongoni mwa wananchi.

Baada ya taarifa ya pili ya tume ya wanasheria na wachumi iliyochunguza suala la makinikia, nimeona katika vyombo vya habari vikuu na mitandao ya kijamii watu waliojazibika na kuhamasika kumuunga mkono na kuahidi kuwa wapo nyuma yake. Kuna saikolojia moja ya wapigakura katika nchi zetu. Watu wanaamini umaskini wao unatokana na viongozi wanaoiba mali za umma. Kiongozi mkuu anapotengeza uadui na kada hiyo ya viongozi wanaoonekana walaji, kama Magufuli, anajijenga kisiasa kwa namna mbili.

Kwanza, watu wanaamini chanzo cha matatizo kinashughulikiwa na hivyo kupata matumaini kuwa mambo yatakuwa vizuri baadaye. Pili, wananchi wanahamisha fikra zao kutoka katika mambo yanayoonyesha kushindwa kwa Serikali kutoa huduma za msingi na badala yake wanawafikiria wale wanaodhaniwa kuwa maadui. Yaani wanawachepusha kutoka mambo ya msingi.

Wapinzani kujichimbia kaburi

Kutokana na kuchanga na kucheza karata zake vyema katika wiki chache zilizopita baada ya taarifa ya kwanza ya makinikia hadi ile ya pili, Rais Magufuli ameonekana ndiye nyota wa mchezo, huku wapinzani wakijichimbia kaburi la kisiasa, kwa kusema ‘ukweli’.

Kilele cha kujichimbia kaburi la kisiasa kilifikia pale Rais Magufuli alipotembelewa na Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation ambayo ni mmiliki mkubwa wa Kampuni ya Acacia Mining Limited, Profesa John L. Thornton, licha ya utabiri wa wapinzani kuwa sakata hili litasababisha Tanzania kushtakiwa na kuingia hasara kubwa.

Tangu mwanzo, wapinzani wamekuwa wakipinga hatua za Serikali kwa ujumla wakidai kuunda tume ni upuuzi mtupu, haitaleta maana wala tija yoyote kwa sababu zilikuwapo nyingine huko nyuma na hakukuwa na mabadiliko. Pia walidai makinikia ni sehemu ndogo ya matatizo mengi yaliyopo katika sekta ya madini.

pia, wapinzani wanasema sera ya kurekebisha sekta ya madini ni yao, na kwamba Magufuli hana mamlaka ya kimaadili ya kurekebisha matatizo hayo kwa sababu yeye mwenyewe amekuwa sehemu ya mfumo uliounda matatizo hayo.

Jambo la kushtusha zaidi kutoka kwa wapinzani ni lugha ya kejeli na kukatisha tamaa ambayo wanaitumia dhidi ya juhudi za Serikali, kiasi kwamba wanaonekana kama wanafurahia madini na malisiali nyingine kuvunwa bila Tanzania kupata inachostahili. Wanaombea hali iwe mbaya ili wapate umaarufu wa kisiasa na labda kuishinda CCM.

Lakini hata kama hilo ndiyo lengo, matokeo yake hayawezi kuwa mazuri kwa sababu watu wanaona wapinzani wanavyomkatisha tamaa Magufuli na kutoa hoja ambazo ungetegemea zitolewe na kampuni zinazotuhumiwa.

Haistaajabishi basi kuwa Rais na wana CCM wenzake wanaeneza kampeni dhidi ya wapinzani wakiwatuhumu kuwa ni mawakala wa wezi waliojiunga na wazungu dhidi ya Watanzania baada ya kuhongwa fedha.

Na huwezi kuwalaumu CCM kwa kutumia fursa hiyo kuwafitinisha wapinzani kwa wananchi kwa sababu lugha za wapinzani zinaashiria kale kaugonjwa maarufu ka - kupinga kila kitu, na kutotaka kuona na kutambua juhudi (hata kama ni ndogo) za Serikali za kujaribu kutatua matatizo lukuki katika sekta ya madini.

Tangu mwanzo wapinzani wamekuwa wakitoa hoja za kukosoa tume zilizoundwa na kuziita taarifa zao kuwa ni za uongo huku wakitoa hoja za kuelezea namna wawekezaji watakavyotushinda, jambo ambalo linashangaza wengi ukizingatia kuwa nchi ipo katika vita ya wazi ya kiuchumi.

Wachina wana msemo wao kuwa safari ya maili elfu moja huanza na hatua moja. Tuwe wa kweli, Magufuli kaanza. Kama alichofanya ni kidogo, basi tumpongeze kwa kuanza na kumshajiisha aendelee zaidi. Kusema kuwa kilichofanyika ni upuuzi, ni bure, hamna faida ni kukosa busara za kisiasa.

Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na anapatikana kupitia 0713420780