Wasichana wengi hawana taarifa sahihi kuhusu hedhi

Miaka ya nyuma haikuwa rahisi kusikia mtu akizungumzia suala la hedhi hadharani.

Hata hivyo, bado baadhi ya jamii inaamini suala hilo ni siri na ni aibu kutaja neno hedhi mbele za watu hasa wanaume.

Usiri wa hedhi ndiyo unaoendelea kuwafanya wasichana wengi kuwa gizani.

Water and Sanitation Network (Tawasanet), inasema asilimia 82 ya wasichana nchini hawana taarifa sahihi kuhusiana na mabadiliko ya miili yao na namna sahihi ya kukabiliana na changamoto kipindi cha hedhi, hali inayosababisha baadhi yao kushindwa kuhudhuria masomo shuleni.

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) unasema hakuna namna nyingine ya kuwasaidia wanafunzi wa kike zaidi ya kuvunja ukimya kuhusu heshi.

May 28 kila mwaka, Tanzania huungana na mataifa mengine kuandimisha siku ya hedhi kwasababu suala hilo siyo siri tena.

Mkurgenzi wa TGNP, Lilian Liundi anasema hedhi inapaswa kujadiliwa kuanzia ngazi ya familia kwa sababu, isipokuwa hivyo linaweza kuzorotesha maendeleo ya mtoto wa kike kielimu.

Kutokana na ukweli huo, TGNP wameamua kuvunja ukimya kwa kuanzisha ‘kijiwe’ maalumu ili kuwawezesha watoto wa kike shuleni kujadili juu ya hedhi salama.

“Hiki ni kijiwe ambacho wanawake watu wazima, wa kati na wanafunzi wa kike wanakutana pamoja kujadili kuhusu hedhi. Wasichana lazima waambiwe ukweli kuhusu mabadiliko ya miili yao, hii itaongeza mahudhurio shuleni na itapunguza mimba za utotoni,” anasema Bibi Kijiwe, Rehema Mwateba.

TGNP imeanzisha kijiwe hicho baada ya kubaini wapo watoto wengi wa kike wanaoshindwa kupata taarifa kuhusu afya ya uzazi na hedhi salama kutokana na kuwapo kwa baadhi ya mila na desturi kandamizi.

Katika kijiwe kilichowakutanisha wanafunzi wa kike kutoka shule mbalimbali Jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Meneja wa Idara ya Ujenzi wa Nguvu ya Pamoja wa TGNP, Grace Kisetu alisema wasichana wanatakiwa kuwa huru kujadili masuala yanayohusu afya zao.

“Watoto wetu wakati mwingine wanakutana na vitu ambavyo kwa sababu ya mila na desturi wanashindwa kuvisema, tumeamua kuanzisha hiki kijiwe kusudi tukae nao na kuwasaidia kusudi wasione haya, waweze kusema na kuzungumzia masua haya,” anasema Kisetu.

Anasema mjadala kuhusu hedhi salama utaiamsha jamii inayodhani ni siri kuzungumzia hedhi wakati wasichana wanaumia kwa kutowekewa mazingira salama kwa ajili ya jambo hilo.

Simulizi za wanafunzi kuhusu hedhi

“Mama yangu aliniambia mtu yeyote hatakiwa kujua kama nipo kwenye hedhi ni bora niseme kichwa kinauma kama nitasikia maumivu makali kuliko kusema ukweli kwa kuwa naweza kulongwa,” anasema mmoja wa wasichana waliohudhuria mafunzo hayo.

Anasema mama yake alimwambia ikiwa ataweka wazi suala hilo kwa watu, wanaweza kumfanya asizae wakati atakapokuja kuwa mtu mzima baada ya kumaliza masomo yake.

“Kwa hiyo naogopa sana, ikitokea naumwa tumbo huwa sisemi kwa yeyote, ni bora niwaamie kichwa kinaniuma,” anasema msichana huyo jina linahifadhiwa.

Msichana mwingine anasema kutokana na hali ngumu ya wazazi wake, wakati anapokuwa kwenye hedhi huwa inamlazimu asiende shule kwa kukosa pedi.

“Kuna wakati vitambaa ninavyotumia huwa vinavuja, tangu siku niliyoaibika shuleni mpaka leo nikiwa kwenye hedhi kama sina pedi siendi kabisa shuleni hadi ninapomaliza baada ya siku tatu au nne,” anasema binti huyo.

Mkurugenzi wa TGNP, Lilian Liundi anasema kisa cha mwanafunzi mmoja wa kike kuzomewa na wenzake kwa sababu ya kuchafua nguo kutokana na hedhi kilimfanya asiende shule kwa zaidi ya wiki mbili akiona aibu.

“Huyu msichana alitakiwa kujibu swali darasani, lakini kila mwalimu alipomtaka asimame hakusimama, baadaye alivutwa akilazimishwa kufanya hivyo ndipo wenzake wakaona kumbe sketi yake ilikuwa imechafuka,” anasema.

Liundi anasema lazima suala la hedhi lizungumzwe kwa uwazi ili jamii itambue umuhimu wa jambo lenyewe.

Mwaka jana wakati akifundisha, Ofisa Sera kutoka Tawasanet, Darius Mhawi anasema hedhi huathiri wasichana wanapokuwa shuleni kwa kuwafanya wawe na hofu au aibu ya kuchafuka, wengine hupata maumivu ya tumbo na kichwa huku baadhi wakiwa na hisia za kunyanyaswa na wenzao hasa wavulana.

Mwalimu wa Shule ya Msingi Makumbusho, Ester Chaduo anakiri kuwa mazingira ya shule yasiyo rafiki kwa wasichana yanaweza kuwa sababu ya kupunguza mahudhurio yao wakati wa hedhi.

Taasisi ya uangalizi ya Haki za Binadamu ya Human Right Watch (HRW) katika ripoti yake ya mwaka 2017 kuhusu hali ya utoaji wa elimu ya sekondari nchini, inasema mazingira ya shule nyingi si rafiki kwa mwanafunzi wa kike hasa akiwa kwenye hedhi.

Mwalimu Chaduo anasema wameanzisha utaratibu wa kuwasaidia wanafunzi wa kike kupata elimu juu ya afya zao kwa kukaribisha wadau wanaozungumzia jambo hilo pamoja na kugawa bure taulo za kike kwa wale wasio na uwezo.

“Tuna chumba cha faragha ambacho wasichana wakiwa kwenye siku za hedhi wanaweza kujisitiri huko, huwa tunazungumza nao na hili limekuwa likiwajengea ujasiri zaidi,” anasema.

Nini kifanyike

Mhawi anasema ili kuondoa changamoto za hedhi ni muhimu kuwe na mtalaa wa elimu unaozungumzia jambo hilo shuleni, jamii kuvunja ukimya na watu wa rika zote waweze kujadili bila aibu.

Anasema ipo haja ya kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa vifaa vya hedhi kwa bei nafuu itakayomuwezesha kila mmoja kuimudu.

Hivi karibuni, Mbunge wa Viti Maalum Upendo Pendeza aliandaa hoja binafsi ambayo hata hivyo haikupenya bungeni akishinikiza Serikali kuandaa bajeti maalumu kwa ajili ya kuwasaidia wasichana vifaa vya kujisitiri wakati wa hedhi.

Takwimu zinaonyesha baadhi ya wasichana hukosa masomo kwa siku tatu hadi nne kwa sababu ya kukosa vifaa hivyo.

Mwatebe anasema pia wazazi wanatakiwa kuvunja ukimya kwa kukaa na watoto kujadili suala la hedhi bila kuoneana aibu.