Wasiwasi dhidi ya waangalizi wa uchaguzi barani Afrika

Waangalizi wa uchaguzi nchini Kenya wakijadiliana jambo jijini Nairobi. Kutoka ushoto ni Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry na Waziri Mkuu mstaafu wa Senegal, Aminata Toure Agosti 9, 2017. Picha ya Reuters

Muktasari:

Je, muhimu ni idadi ya kura alizopigiwa mgombea, hivyo akatangazwa kuwa mshindi, au kipaumbele kiwekwe juu ya mwenendo mzima wa uchaguzi - tangu pale wapigaji kura wanapoandikishwa, taratibu na kampeni za uchaguzi, upigaji, ukusanyaji na kuzihesabu kura au namna ya kuyatangaza matokeo

Katika uchaguzi mkuu wa Kenya wa Agosti 8 mwaka huu na ule wa marudio wa urais wa Septemba 26, nadharia mbili zinazopingana zilichomoza kuhusu matokeo ya chaguzi hizo.

Je, muhimu ni idadi ya kura alizopigiwa mgombea, hivyo akatangazwa kuwa mshindi, au kipaumbele kiwekwe juu ya mwenendo mzima wa uchaguzi - tangu pale wapigaji kura wanapoandikishwa, taratibu na kampeni za uchaguzi, upigaji, ukusanyaji na kuzihesabu kura au namna ya kuyatangaza matokeo.

Katika chaguzi zote hizo mbili Tume Huru ya Kenya ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imedhihirisha haijaimudu hata kidogo kazi iliyopewa ya kuzisimamia chaguzi hizo, licha ya mabilioni ya shilingi zilizotumika.

Baada ya uchaguzi wa marudio wa Septemba 26, mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati alisema asilimia 47 kati ya watu zaidi ya milioni 19 walioandikishwa kupiga kura ndio walishiriki katika zoezi hilo. Baada ya saa chache alidai kwamba asilimia 38 ya watu walio na haki ya kupiga kura ndiyo waliotumbukiza kura zao.

Kila kura kutoka katika wilaya za uchaguzi zilipojumlishwa mwishowe katika makao makuu mjini Nairobi, matokeo yalibadilika.

Huenda hii ilitokana na kuhesabiwa sivyo, kwa makosa, lakini pia isikatalike moja kwa moja kwamba jambo hilo huenda lilifanyika kwa makusudi.

Kilichojidhihirika wazi, hata hivyo, ni kwamba tume hiyo ya IEBC isingeachiliwa hata kidogo kusimamia uchaguzi wa Agosti 8, seuze tena kabisa ule wa marudio wa Septemba 26. Tume hiyo imejifanya kuwa kichekesho kwa Wakenya na kwa walimwengu pia. Lakini kulikuwa hakuna mbadala. IEBC ndiyo inayotakiwa na Katiba ya Kenya isimamie chaguzi za nchi hiyo, tangu za kaunti, bunge, Baraza la senati, magavana hadi ule wa rais wa nchi.

Idadi ya kura zilizopigwa na zile zinazodaiwa amepata Rais mteule, Uhuru Kenyatta zinabishiwa na wapinzani. Katika uchaguzi wa urais wa marudio watu walishuhudia namna vituo kadhaa vya uchaguzi vilivyobakia vitupu au kuwa na milolongo mifupi ya watu waliotaka kupiga kura, wacha kwamba sehemu kadhaa za nchi hakujafanywa uchaguzi kutokana na vurugu na watu walioususia uchaguzi na kuzifunga barabara za kupitia magari ya kusafirisha vifaa vya uchaguzi.

Wiki moja kabla ya kufanywa uchaguzi wa marudio, Chebukati alikiri kwamba asingeweza kuhakikisha kwamba uchaguzi huo ungekuwa wa kuaminika na salama. Lakini siku mbili kabla ya uchaguzi alibadilisha kauli yake na akasema kwamba ana matumaini uchaguzi huo ungekwenda vizuri. Kitu gani kilichomfanya afikie uamuzi huo hajakitaja.

Itakuwa maajabu pindi matokeo ya uchaguzi wa Septemba 26 hayatabishwa na mtu yeyote mbele ya Mahakama Kuu ya Katiba ya Kenya, seuze tena na upinzani.

Mambo yanatazamiwa yatakuwa kama vile baada ya uchaguzi wa Agosti 8, na huenda Mahakama Kuu ya Kikatiba ikaubatilisha tena uchaguzi wa Septemba 26, kwa hoja ya kutoendeshwa kwa mujibu wa katiba na sheria. Dosari ya uchaguzi wa Septemba 26 yanaonekana ni mengi zaidi kuliko yale ya Agosti Nane.

Muda mfupi kabla ya IEBC kutangaza matokeo ya Uchaguzi wa Agosti 8, waangalizi wa kigeni wa uchaguzi huo kwa haraka walianza kutoa taarifa wakidai uchaguzi huo ulikuwa safi kabisa, huru na wa haki, na kwamba ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta aliyekiongoza Chama cha Jubilee ulikuwa wa haki na bila dosari.

Walimtaka kiongozi wa Upinzani wa Muungano wa NASA, Raila Odinga akubali ameshindwa, ama sivyo, walimtuliza aende mahakamani kubisha, lakini si kuwaruhusu wafuasi wake waende kulalamika mabarabarani.

Odinga alihisi ameporwa ushindi alioudai ni wake kama ule wa chaguzi tatu za hapo kabla. Alikwenda mahakamani na akashinda, majaji wakiamuru uchaguzi mpya urudiwe. Hilo lilikuwa kofi kubwa lililopigwa juu ya mashavu ya waangalizi wa uchaguzi kutoka ng’ambo, hasa wale wa nchi za Ulaya Magharibi na wa Marekani (Kutoka Wakfu wa Jimmy Carter waliongozwa na waziri wa zamani wa mambo ya kigeni wa Marekani, John Kerry).

Katika Kenya, kama ilivyo katika nchi nyingi za Afrika, kuna desturi ya mgombea aliyeshindwa katika uchaguzi mara nyingi kulalamika kwamba ameibiwa ushindi, kwamba uchaguzi ulifanyika kwa udanganyifu.

Malalamiko hayo mara nyingi huwa yana sababu za kimsingi. Ndio maana kabla ya uchaguzi wa Agosti 8 huko Nairobi, Serikali ya Marekani na Umoja wa Ulaya ziliamua ziipatie Kenya kompyuta mpya za kuhesabia kura ili angalau kupunguza malalamiko ya udanganyifu katika zoezi la kupiga kura. Mfumo wa kuhesabu kura katika Kenya ni wa kielektroni, kinyume na ule wa kuhesabu kwa mkono tu, na ambao unapunguza wizi wa kura.

Hadi Euro nusu bilioni zilitumika kununulia kompyuta hizo, na sehemu kubwa ya fedha hizo zilirejea Ulaya kwani ni makampuni ya Ulaya yaliyopewa kandarasi za kuiuzia IEBC kompyuta hizo.

Hayo yalifanyika licha ya kwamba Kenya inayo makampuni yanayoanza kufanikiwa katika shughuli hiyo. Siku ya uchaguzi kompyuta hizo mpya zilianza kufanya kazi, bila ya shaka kwa furaha ya pia waangalizi wa nchi za Magharibi. Na haijawa pia mshangao kwa waangalizi hao wa Magharibi kutamka mara baada ya uchaguzi kwamba mambo yote yalienda salama na kwa haki.

Mahakama Kuu ya Katiba ya Kenya iliyamulika zaidi matokeo ya Uchaguzi wa Agosti Nane na ikagundua kwamba kompyuta hizo mpya zilitoa uwezekano wa kuchakachua zaidi matokeo.

Siku chache kabla ya kufanywa uchaguzi, mkuu wa kitengo cha mawasiliano ya kompyuta cha IEBC, Chris Msando aliuawa, hivyo kutumia data zake za siri katika kuchakachua zaidi matokeo ya uchaguzi. Kwanini hayo yote hayajatajwa katika ripoti za waangalizi wa nchi za Magharibi?

Jibu ni kwamba wao walitaka uchaguzi ufanyike kwa vyovyote vile bila ya kujali kasoro mbalimbali zilizochomoza ambazo zingewekea alama kubwa za kuuliza juu ya busara ya kufanyika uchaguzi huo wakati huo. Pale Mahakama Kuu ya Katiba ya Kenya ilipogundua kwamba uchaguzi wa Agosti 8 haujawa chochote kingine bali ni uchafuzi, hivyo inabidi ufanyike mpya mwingine, wakaguzi hao wa Magharibi walishangilia na kusifu kwamba tukio hilo ni la mara ya kwanza katika Afrika - ni ushindi wa demokrasia.

John Kerry alijitoa kimasomaso na kufikia karibu kukiri makosa aliyoyafanya ya harakaharaka kuupa uchaguzi huo hati safi kabisa na kuzikubali mbiombio hesabu zilizotolewa na IEBC kwa msaada wa kompyuta za nchi za Magharibi.

Raila Odinga alizikejeli nchi za Magharibi pale aliposema kwamba “ushindi” wa Uhuru Kenyatta ulikuwa wa “Vifaranga vya Kompyuta.” Waangalizi wa nchi za magharibi walisahau kwamba kompyuta hizo za nchi za Magharibi zilikuwa zinasimamiwa na Wakenya waliokuwamo ndani ya sekretariati ya IEBC.

Swali la msingi ni kwanini nchi za Magharibi zilizotuma waangalizi wao huko Nairobi hazijajiuliza kama lilikuwa wazo zuri kwa IEBC, iliyochafua uchaguzi wa mwanzo wa Agosti 8, iruhusiwe isimamie tena uchaguzi wa marudio, tena bila ya kuyasahihisha makosa yaliofanywa katika uchaguzi wa mwanzo, na bila ya kuwawajibisha maofisa waliosababisha uchafuzi katika uchaguzi wa mwanzo?

Nchi za Magharibi, licha ya kuyaona mbele ya macho yao, maajabu yote hayo, zilinyamaza kimya. Demokrasia inayozungumzwa na kushikiliwa katika nchi hizo za Magharibi, si ile ambayo Wazungu wanaitakia Afrika. La mwanzo kwa Wazungu hao ni kuitakia nchi ya Kiafrika “utulivu” pale utulivu huo utaendeleza pia maslahi yao ya kiuchumi au ya kijeshi. Pia cha mwanzo kwao ni “kuchochea vurugu” pale vurugu hizo zitasaidia pia, kwa muda fulani, kupeleka mbele maslahi yao ya kisiasa, kiuchumi na kijeshi.

Kwa nchi za Magharibi hivi sasa Kenya iliyo “tulivu” ndiyo kipaumbele, na jambo hilo ni zuri, lakini nchi hizo hazijali hata ikiwa demokrasia itapigwa teke, utarejea utawala wa kiimla au udikteta utakaowatenga watu wengi mbali na madaraka ya Serikali.

Uhuru Kenyatta ameshinda, amepata karibu asilimia 100 ya kura zilizopigwa katika uchaguzi wa marudio. Lakini ukweli ni kwamba Wakenya sasa wamegawanyika zaidi kuliko wakati wowote mwingine tangu nchi hiyo ilipopata uhuru mwaka 1963.

Raila Odinga aliyeshindwa amesema ataugeuza Umoja wake wa Nasa kuwa vuguvugu la kuukaidi utawala wa Kenyatta. Na magavana wa Mombasa na Kilifi, sehemu ya pwani ya Kenya ambao ni washirika wakubwa wa Raila Odinga, wamezusha suala la uwezekano sehemu yao ya Pwani ya Kenya kujitenge na Kenya kwa vile maslahi yao hayaangaliwi na Serikali kuu ya Jubilee huko Nairobi. Huo si mustakabali mzuri kwa Kenya.

Cha kusikitisha juu ya chaguzi za Kenya ni kwamba uamuzi anakuwa nao mtu anayekamata mwiko jikoni mbele ya sufuria la minofu ya nyama - naye ni rais wa nchi.

Yeye anahakikisha kwamba Tume ya Uchaguzi ina watu wanaomtii au anaoweza kuwatisha pale inapohitajika yeye aendelee kubakia madarakani. Hapo tena haijali nini watakachosema waangalizi wa uchaguzi kama ni wa ndani au wa nje.

Kwa vyovyote waangalizi wa nje hukaa katika nchi inayohusika kwa siku chache. Isitarajiwe kwamba wao ni wajuzi tosha wa siasa na mabishano yalio ndani ya jamii za Kiafrika. Ni makosa kutegemea ripoti zao kuwa ndiyo ukweli wote wa mwisho, asilimia 100, kama uchaguzi uliofanyika ulikuwa wa haki na sawa.

Swali jingine linazuka kwamba inakuwaje chaguzi za Afrika mara nyingi hujiwa na waangalizi wa kutoka Ulaya na Marekani na kinyume na hivyo si sana kusikika?

Karika jibu lake usiusahau ule msemo kwamba anayelipia muziki ndiye mwenye haki ya kuucheza muziki wenyewe. Chaguzi katika nchi nyingi za Afrika hugharimiwa pia na fedha za kutoka nchi wafadhili za Ulaya na Marekani.