Wasomi: Uhuru, Raila darasa tosha

Muktasari:

  • Mahasimu hao wa kisiasa Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa muungano wa National Super Alliance (Nasa), Raila Odinga wamekutana baada ya takribani miezi minne ya taharuki ya kisiasa iliyotokea nchini mwao.

Wagombanao ndiyo wapatanao. Msemo huu ndiyo unavyoweza kutumika kuelezea tukio la Ijumaa Machi 9 nchini Kenya baada ya mahasimu wakuu wa kisiasa nchini humo kukutana na kufanya mazungumzo.

Mahasimu hao wa kisiasa Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa muungano wa National Super Alliance (Nasa), Raila Odinga wamekutana baada ya takribani miezi minne ya taharuki ya kisiasa iliyotokea nchini mwao.

Katika kipindi hicho Wakenya wameshuhudia matukio mbalimbali ikiwamo maandamano ya mara kwa mara ya kupinga uongozi wa Rais Kenyatta na pia tukio la kiongozi huyo wa upinzani kujiapisha kama rais wa wananchi wa nchi hiyo jambo ambalo lilielezwa ni kinyume cha sheria za nchi hiyo.

Tukio hilo la kukutana kwa mahasimu hao licha ya kuwashtua Wakenya, liliibua mjadala kote Afrika Mashariki na Afrika nzima, kwa jinsi mahasimu hao walivyokutana na kutoka kauli moja ya kujenga Kenya mpya.

Wanasiasa hao waliamua kukutana juzi mchana katika ofisi ya Rais iliyopo katika jengo la Harambee lililopo jijini Nairobi nchini Kenya na pamoja na mambo mengi waliweza kujadili mustakabali wa nchi hiyo huku Raila akitoa ya moyoni kwamba ulikuwa ni wakati wa kujitathimini kama nchi.

Baada ya mazungumzo hayo, Raila alivieleza vyombo vya habari kuwa wamekubaliana na ‘ndugu yake Kenyatta kwamba Kenya iwe taifa moja ili kuzima migawanyiko iliyopo.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema hiyo ni hatua nzuri katika kufuta tofauti zao zilizodumu kwa muda mrefu na hatimaye kujenga Kenya mpya kwa mustakabali wa nchi yao.

Ni wazi kuwa sasa Kenya imefungua ukurasa mpya katika demokrasia ya nchi hiyo baada ya kugundua kuwa anayeweza kujenga au kuibomoa nchi yao ni wao wenyewe.

Wachambuzi wazungumza

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji amewapongeza viongozi hao kwa kuonyesha alichokiita ukomavu wa hali ya juu kwa kubaini ukweli kwamba katika siasa mnaweza kupingana kwa hoja bila kupigana.

“Wote ni mashahidi muda si mrefu Raila alitangaza maandamano makubwa lakini pamoja na kuandamana Rais Kenyatta alionyesha uvumilivu wa kiwango cha juu na Serikali iliwahakikishia ulinzi lakini mwisho wa siku walifikisha ujumbe wao kwa amani.”

“Hawakuishia hapo, siku chache baadaye kiongozi huyo wa upinzani aliamua kujiapisha; Rais Kenyatta alikuwa na uwezo wa kufanya chochote. Yeye ni kama headmaster (mkuu wa shule) kila mtu anamtii, pengine leo tusingekuwa na Raila lakini alionyesha uvumilivu wa kiwango cha juu na kwamba si kila kitu anakijua ila kuna wengine waweza kujua zaidi yake na matokeo yake leo tunashuhudia haya maridhiano,” anasisitiza.

INAENDELEA UK 24

INATOKA UK 23

Dk Mashinji anasema kitendo hicho ni somo kubwa kwa nchi za Afrika na kimesababisha wananchi wa Kenya sasa kujiona ni wamoja na kwamba hawana sababu ya kupingana kama ilivyokuwa awali.

Dk Mashinji anasema somo hilo liwafikie viongozi wa nchi nyingine, ikiwamo Tanzania, kwamba kunapotokea migogoro njia sahihi ni kufanya mazungumzo.

“Kuna msemo unasema kuwa, “Ukitaka kwenda haraka nenda peke yako, lakini ukitaka kwenda mbali nenda na wenzako”. Huu usemi una maana sana bila kushirikiana kamwe hatuwezi kufika mbali,” anasisitiza na kuongeza kuwa Wakenya wanazizidi nchi nyingi kwa uvumilivu wa kisiasa.

Akizungumzia kitendo cha Raila kujiapisha, Dk Mashinji anasema kiongozi huyo alikuwa akijua wazi kwamba hawezi kuwa Rais, lakini alitaka kuvuta hisia za watu na kufikisha ujumbe kwa Serikali kwamba haiwatendei haki.

“Unajua Raila sasa ni mzee, kitendo kile kweli ni cha kichekesho lakini kilikuwa na umuhimu mkubwa kwa kipindi kile kwa kuwa alihakikisha ujumbe wake umefika na cha muhimu zaidi ni Serikali ilikuwa sikivu na ilielewa nini dhamira yake na mwisho wa siku wameweza kukaa pamoja kwa mustakabari wa watu wa Kenya,” anasema.

Vilevile Dk Mashinji anasema kitendo hicho kitoe funzo kwa viongozi wengine, hata hapa Tanzania ambao anasema wamejifungia ndani, wananchi hawaongei jambo linalosababisha kutopata mrejesho wa jambo wanalokifikiria.

“Serikali ingeruhusu watu watoe wanachokifikiria, wangepata ukweli wanakubalika kwa asilimia ngapi na kugundua wanapokosea badala ya kuacha hofu ikitawala huku wakiamini wanakubalika kwa asilimia 100.

“Hata Rais wa Marekani John Kennedy aliwahi kunukuliwa akisema kuwa kiongozi ukiona unakubalika kwa asilimia zaidi ya asilimia 75, ujue kuna shida kwani ukweli ni kwamba kuna 25 ya watu wanaweza kukuchukia bila sababu za msingi, anasema Mashinji.”

Anasema Kenya imetoa funzo kubwa, kwanza kwa kuwa na Katiba imara inayoweza kuruhusu matokeo ya uchaguzi kupingwa mahakamani, kuruhusu wananchi waseme wanachofikiria lakini pia watawala wameonyesha kuwa kuna uwezekano wa kuwa na tume ya maridhiano ambayo ikitumika vyema nchi itapita katika demokrasia ya kweli.

“Upinzani si uadui na mara zote wanasiasa watambue kuwa bila Yanga imara huwezi kuwa na Simba na bila ya kuwa na upinzani imara huwezi kuwa na CCM.”

Dk Mashinji anaungwa mkono na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Alexander Mkulilo anayesema kuwa licha ya nchi hiyo kuwa na mgawanyiko mkubwa wa ukabila na rasilimali ya ardhi, imeweza kuonyesha ukomavu katika siasa.

Dk Makulilo ambaye ni msomi wa sayansi ya siasa anasema ingawa kitendo hicho si cha kwanza kutokea katika nchi za Afrika, lakini viongozi hao wameweza kuweka mazingira ya kufuta tofauti zao ukizingatia kwamba walikuwa katika kipindi kigumu baada ya kumaliza uchaguzi mkuu mwaka jana.

“Ni tukio jema, hata Zanzibar mwaka 2010 viongozi wa chama tawala na upinzani waliwahi kukutana na kufanya maridhiano. Hii inaonyesha siasa siyo ugomvi bali ni kuongoza wananchi ili kufikia malengo kama nchi,” anasisitiza Dk Makulilo.

Kwa mtazamo wake Dk Shoo Innocent, mtaalamu wa Diplomasia na Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia anasema sababu kubwa ya viongozi hao kuamua kukutana ni baada ya nchi hiyo kuanza kuyumba kiuchumi.

“Unajua Kenya ndiyo ina uchumi mkubwa kwa nchi za Afrika Mashariki lakini kutokana na hali ya kisiasa ilivyo, sasa nchini humo takwimu zake za uchumi kwa mujibu wa Benki Kuu ya Kenya zinaonyesha uchumi kuporomoka kwani ilitarajiwa kupanda kutoka asilimia 5.5 lakini sasa umekuwa kwa asilimia 4.5 pekee,” anasema.

Anasema hali hiyo imewatisha sana viongozi hao kwani nchi inayofuata kwa karibu ni Tanzania ambayo inaonekana ina hali nzuri, rushwa imepungua kwa kushika nafasi ya pili ikiongozwa na Rwanda, lakini pia biashara ya utalii inaongezeka kwa kasi hivyo wakaona si vyema kuendelea kulumbana kwani wataendelea kuwapoteza wawekezaji.

“Unaweza kusema kilichofanyika Kenya ni Politica Game (mchezo wa kisiasa) wameona uchumi wao haukui kama walivyotarajia. Kenya wana ofisi nyingi za kimataifa kama Umoja wa Mataifa (UN), UNDP, UN Habitat, Tata na Volkswagen hivyo kuendelea kulumbana kutasababisha kuongoa huduma zao kwani hawawezi kukaa katika nchi ambayo haina utulivu na amani,” anasema.

Dk Innocent anasema kuwa nchi nyingi za Africa zinakosea kwa kushindwa kutoa kipaumbele kwa sekta binafsi na badala yake kufikiri Serikali pekee inaweza kufanya hivyo hata kunapokuwa na mgogoro wa siasa nchi inaamini inaweza kuweka mambo sawa.

“Ukiheshimu sekta binafsi huwezi kuacha hali yako ya kisiasa iende mrama. Haiwezekani Serikali ikafanya kila kitu, ni lazima iweke mazingira mazuri kwa kila mwekezaji wa ndani na nje kuwe na utulivu lakini pia kuwapo na sera ambazo zitasababisha uchumi ukue, hivyo wanasiasa wana nafasi kubwa katika kupingania hilo. Huwezi kuwa na migogoro kila siku ukategemea maendeleo,” anaonya.

Akijadilia hatua hiyo, Wakili wa Kujitegemea, Peter Mshikilwa anasema kuwa nchi hiyo imeonyesha ukomavu wa kidemokrasia na kwamba imetambua kuwa ili ukue ni lazima uwe na taasisi imara.

“Kenya imeonyesha mfano kwa kuwa na Katiba imara na kuweka maslahi ya wananchi mbele kuliko viongozi, mfano wameweza kwenda mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi wakati sisi Katiba yetu inasema matokeo yakishatangazwa hakuna chombo chochote chenye mamlaka ya kuhoji wala kubatilisha matokeo hayo.”

“Huo kwao ni mwanzo mzuri, ndiyo maana unaona demokrasia ya kweli inatamalaki, lakini pia kitendo cha kuwa na Tume ya maridhiano nayo ni hatua nyingine.”

Anawataka viongozi wa Afrika kuhakikisha wanapinga vikali siasa za uhasama kwani hazina nafasi badala yake wanatakiwa kutofautiana kimtazamo na mwisho wa siku wote wanakuwa kitu kimoja kama nchi.

“Hapa kwetu hali ni tofauti ukishakuwa mpinzani basi wewe unaonekana ni adui. Dhana hii haitatufikisha katika kutengeneza demokrasia ya kweli, lazima tubadilike,” anasisitiza Mshikilwa.

Vilevile Mhadhiri wa (UDSM), Dk Francis Michael anasema huwezi kupata maendeleo kama nchi haina amani na utulivu, hivyo viongozi hao wa Kenya wameliona hilo na kuamua kulifanyia kazi.

“Siasa zipo kwa ajili ya wananchi wote siyo kikundi fulani cha wananchi au viongozi wachache wanaojihusisha na mlengo mmoja, hivyo Raila na Rais Kenyatta wameona si busara kuendeleza migogoro ambayo haina tija kwa taifa lao.”

“Kenya ilishagawanyika na bado ina amani, hivyo kama tunataka kuwa na demokrasia ya kweli jambo la msingi kwa viongozi wahakikishe wanaangalia mustakabali wa wananchi wote badala ya maslahi ya makundi na viongozi binafsi,” anasisitiza.

Dk Michael ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uongozi anaongeza kuwa viongozi Afrika lazima watambue kwamba wapo madarakani kwa ajili ya watu wote na hata wapinzani ambao kwa wakati huo hawapo madarakani wana haki sawa na wananchi wengine.

“Suala kubwa ni ushirikiano kwa pande zote, tumejifunza kutoka Kenya, sasa kuna amani baada ya viongozi wake bila kujali kwamba wanatoka chama tawala au upinzani wameamua kukaa pamoja na kujadili mustakabali wa nchi yao kwa manufaa ya Wakenya wote.