Friday, February 17, 2017

UCHAMBUZI: Wasomi wawasaidie wananchi kuelewa mabadiliko

 

By Aziz Msuya, Mwananchi

Kila jamii duniani hupitia mabadiliko yanayochagizwa na mambo mengi zikiwamo sababu za kiuchumi, kijamii, kisiasa, kiutamaduni na kiafya.

Wakati huu unapowadia, jamii inasukumwa kuendana na mabadiliko haya na kunakuwa hakuna namna zaidi ya jamii husika kuakisi na kuyakubali mabadiliko hayo na siyo kupingana nayo.

Ukiangalia mlolongo wa matukio yanayotokea nchini kwa sasa utaona Tanzania inapitia mabadiliko ya kijamii ambayo hayatokei kwa bahati mbaya. Kwa bahati mbaya wasomi hawalielezi hili kinagaubaga ili jamii ielewe kwa nini inatokea na inachotakiwa kufanya.

Kwa mfano, tunashuhudia mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha ukame, kuongezeka kwa joto, upungufu wa mvua na mafuriko ambayo yanaelezwa kuwa ni ishara ya upungufu wa chakula siku zijazo.

Lakini, hali hii inapotokea jamii inatakiwa iandaliwe kubadili mfumo wa maisha na uzalishaji hasa kilimo na ufugaji na kuyageukia mazao yanayostahimili ukame jambo litakalomaanisha kubadili chakula walichokizoea, mpaka hali hiyo itakapokoma.

Kutokana na mahitaji ya hali ya hewa, wananchi wanaweza kulima mtama au mihogo badala ya mahindi ili kukabiliana na ukame uliosababisha upungufu wa mvua, hivyo kubadili chakula kutoka mahindi mpaka mtama au mihogo. Haya ni mabadiliko yasiyoepukika na kung’ang’ania kulima mahindi kutakua hakuna tija.

Mto Ruaha kwa sasa umekauka, hauna maji, hali ambayo haijawahi kutokea. Maana yake ni kwamba kuna athari kwenye ikolojia ya viumbe ambao wanategemea maji ya mto huu. Hali ni mbaya.

Kuna ongezeko la watu kusikoendana na rasilimali zilizopo hasa maeneo ya mjini ikiwamo makazi, matokeo yake ni mabadiliko ya mfumo wa maisha kutokana na kuongezeka kwa watu wasio na makazi, familia nzima au watu wengi kulala kwenye chumba kimoja, hivyo kuporomosha maadili.

Wataalamu wetu hawazungumzii hatari iliyopo kwenye ongezeko kubwa la watu, ukilinganisha na rasilimali zilizopo na matokeo yake vijana wengi kujiingiza kwenye ulevi na utumiaji wa dawa za kulevya, hali ikiwa mbaya mvurugano hujitokeza kwenye jamii.

Suala la uchumi lina nafasi kubwa katika mabadiliko ya kijamii, kwani nchi isipoimarika kiuchumi na kuwa na uwezo wa kuhudumia wananchi hasa kutoa ajira kwa vijana na huduma za kijamii kunaweza kusababisha uvunjifu wa amani, uporaji, wizi na ubakaji.

Kutokea kwa mabadiliko kama haya huchagizwa na ongezeko kubwa la watu isiyohimilika na kuacha idadi kubwa ya vijana ikiwa haina shughuli za kiuchumi za kufanya ili kukidhi mahitaji yao.

Kunapokuwa na idadi kubwa ya vijana wasio na kazi ni rahisi kwao kushawishika kutumia au kusafirisha dawa za kulevya, wimbi ambalo likiachwa liwe kubwa linaweza kusababisha mambo yasiyovumilika katika jamii.

Jamii inapokosa morali ni lazima kuna mabadiliko katika eneo husika, na wataalamu wa masuala mbalimbali pamoja na watunga sera wanapaswa kuchukua hatua ili kuirudisha kwenye mstari.

Tunashuhudia na tutaendelea kushuhudia mabadiliko ambayo yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na mwenendo wa kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni. Jambo la msingi kwa wasomi na wanazuoni ni kuwaandaa Watanzania kukabiliana na mabadiliko haya, kadri yatakavyokuwa yanajiri ikiwamo kushauri njia bora na sahihi ya kukabiliana nayo ili kutoleta madhara.

Aziz Msuya ni mwandishi wa gazeti hili aliyepo mkoa wa Morogoro (0716069926)

-->