Wataalamu: Unyonyaji kidole huimarisha afya ya mtoto

Picha na Mtandao

Muktasari:

Kwa mtoto, kunyonya kidole ni namna ya kujifariji. Mtoto asipotosheka kila anaponyonya maziwa huanza kunyonya kidole ambacho humfanya apunguze njaa. Kisaikolojia; hujibembeleza na kujisikia salama.

Ni kawaida watoto wadogo kunyonya kidole kutokana na mahitaji ya kimwili na kisaikolojia. Mtoto huanza kunyonya kidole endapo hapati maziwa ya kutosha. Mara nyingine husababishwa na matatizo ya kihisia.

Kwa mtoto, kunyonya kidole ni namna ya kujifariji. Mtoto asipotosheka kila anaponyonya maziwa huanza kunyonya kidole ambacho humfanya apunguze njaa. Kisaikolojia; hujibembeleza na kujisikia salama.

Mara nyingi mtoto ataacha kunyonya kidole akiwa na umri kati ya miaka mitatu mpaka sita ingawa wengine huendelea hadi ukubwani.

Inasemekana kuwa tabia hii huanzia tumboni baada ya wiki 13 za ujauzito na huendelea mpaka mtoto anapozaliwa ingawa wazazi wengi hugundua hilo mtoto anapofikisha umri wa miezi miwili mpaka mitatu.

Zipo faida zilizothibitika za watoto kunyonya kidole. Nyingine zinaendelea kuchunguzwa. Baadhi ya watafiti wanadai unyonyaji huo huimarisha kinga ya mwili. Watafiti hao wanadai unyonyaji wa dole gumba na ung’ataji wa kucha husaidia kuzuia mzio (allergy).

Hasara

Kama ilivyo kwa masuala mengine yoyote, hili nalo lina hasara zake. Zipo zitokanazo na mtazamo na imani za jamii husika na zile za kimuonekano.

Kwenye jamii zilizopo, baadhi ya watu huamini mtoto anayenyonya kidole anajipunguzia uwezo wa kuzingatia masomo hivyo kuwa mjinga jambo ambalo kitaalamu halijathibitika.

Upo uwezekano wa mdomo hasa kuathirika. Inaelezwa kuwa ‘lips’ zinaweza kulegea kutokana na uzito wa kidole sambamba na mtoto kuchelewa kuwa na ufahamu kutokana hutumia muda mwingi kunyonya kidole. Wazazi wanashauri kuwa macho ili kunusuru hali hii.

Endapo mtoto ataendelea kunyonya hata akiwa na umri mkubwa kidogo inaweza kusababisha meno kutojipanga vizuri kwenye fizi. Madaktari wa kinywa wamehusisha mpangilio mbaya wa meno na kunyonya kidole hasa gumba kwani meno husukumwa kwenda mbele au kujipanga vibaya na hivyo kuathiri muonekano wa mhusika.

Daktari Bingwa wa Meno, Christopher Ruhinda wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) anathibitisha hili. “Ni kweli. Nguvu (presha) anayotumia mtoto kunyonya kidole inahartibu mpangilio wa meno. Mara nyingi yanatoka nje na mdomo hushindwa kufunga,” anasema Dk Ruhinda.

Kunyonya kidole siyo hatari ikiwa mtoto ataacha kabla ya miaka mitano. Kama mtoto atashindwa kuacha kunyonya kidole mpaka baada ya umri huo kuna uwezekanao mkubwa wa meno yake kutojipanga vizuri na kuota yakiwa yamebebana au kuwa na meno yasiyokutana.

Watoto wanaonyonya kidole baada ya miaka minne au mitano wana hatari ya kupata tatizo hili hivyo kuathiri muonekano wao wa sura na hata matatizo ya kuongea vizuri.

Hii huweza kutokea kutokana na kulegea kwa lips ambazo ni muhimu kwa matamshi ya baadhi ya maneno. Meno yaliyokosa nafasi au yenye nafasi kubwa nayo yana athari kwenyemmatamshi. Kutokana na kunyonya huko mtoto atapata tatizo la matamshi na viungo vya mdomo mfano ulimi kutoka nje wakati wa kuongea.

Inategemea na ukubwa wa athari. Kama mpangilio haujawa mkubwa sana mpangilio mbaya huweza kujirekebisha wenyewe iwapo mtoto ataacha kunyonya kidole. Kwa wale wanaopitiliza wanahitaji huduma za mtaalamu wa meno (orthodontist) kufanya marekebisho.

Ipo mifano kadhaa ya watu waliowahi kufanya upasuaji wa fizi ili kurekebisha mpangilio wa meno kuupata muonekano wanaouhitaji.

Cha kufanya

Inashauriwa kutomkataza mtoto kunyonya kidole akiwa chini ya miaka minne au mitano isipokuwa kama kuna tatizo linalojitokeza au mtoto akianza ghafla kufanya hivyo baada ya miezi 10 tangu azaliwe na ikiambatana na kuvuta nywele.

Ili kupunguza uwezekano huo, mama anayenyonyesha anapaswa kula vyakula vyenye lishe kamili vitakavyosaidia mwili kutengeneza maziwa ya kutosha kumnyonyesha na kumshibisha mtoto kila wakati hivyo kumuepusha kunyonya kidole.

Kwa mtoto anayenyonya, wazazi au walezi wanapaswa kumueleza kwa upole wakitumia lugha laini ikibidi kumuahidi zawadi nzuri ili akubali kuacha kunyonya kidole.

Kumuanzisha shule ni njia nyingine inayoweza kumsaidia mtoto kuacha kunyonya kidole. Shule kutamfanya aone aibu na kuacha hasa atakapokuwa anataniwa na wenzake anaosoma na kucheza nao.

Njia mbadala pia zinaweza zikatumika. Hizi zitamsaidia kuacha mapema zaidi. Kupaka pilipili vidole vyake ili akinyonya awashwe na ukali atakaokutana nao itamfanya asirudie tena kufanya hivyo ingawa kutakuwa na jukumu la kumbeleza kila atakapokuwa analia baada ya kunyonya kidole.

Kushiriki michezo inayoshughulisha mikono kwa muda mwingi ni njia nyingine ya kufanikisha suala hili. Unaweza ukampa midoli (wanasesere), au acheze na wenzake ili mradi viganja vyake viwe na shughuli ya kufanya na kumnyima nafasi ya kunyonya kidole.

Pia, unaweza kumnunulia nyonyo za plastiki ili umpe anyonye badala ya kidole. Hii itamfanya asipate muda wa kuzoea kunyonya kidole.

Kuwavalisha watoto mipira ya mikono au viganja (gloves) na kuwafanya washindwe kunyonya vidole.

Iwapo vyote hivyo vitashindikana basi mzazi au mlezi asisite kuwaona madaktari wa afya ya meno na kinywa kwa msaada zaidi.