Watahiniwa darasa la saba 2013; Watafaulu au watafaulishwa?

Mtihani unaendelea. Baadhi ya wadau wa elimu wana shaka na muda mdogo uliotolewa kutekeleza mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, ambao pamoja na mambo mengine  unasisitiza kupanda kwa  kiwango cha ufaulu kwa wahitimu wa darasa la saba  kuanzia mwaka huu. Picha ya maktaba

Muktasari:

  • Ili kutekeleza mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, maofisa elimu walikula kiapo cha kupandisha kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa mwaka huu kutoka asilimia 31 hadi 60

Desemba 20 mwaka huu, Serikali ilitangaza matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba wa mwaka 2012, yaliyooonyesha kufeli kwa idadi kubwa ya watahiniwa.

Ni kwa sababu hiyo, Serikali iliamua kuwapa fursa ya kuendelea na elimu ya sekondari hata watahiniwa waliopata alama chini ya 100 tofauti na utaratibu ulivyo.

 Kwa mujibu wa taratibu za mitihani ya darasa la saba, jumla ya alama zote ni 250 ambazo hugawanywa katika madaraja matano yaani ni A mpaka E.

Mchanganuo uko hivi: Daraja A huanzia alama 201 hadi 250, B inaanzia  151  hadi  200.  Daraja C ni 101 hadi 150 na D  inaanzia 51  hadi  100 . Chini ya alama 50 ni daraja E.

Kwa mtihani wa mwaka jana, asilimia 40 ya watahiniwa walipata daraja D, lakini bado wakachaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari.

Watahiniwa wapya 2013

Wakati kumbukumbu za matokeo hayo mabaya zikiwa bado katika vichwa vya Watanzania, kuanzia kesho hadi keshokutwa wanafunzi wa darasa la saba 868,030 wanatarajiwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu yao ya msingi mwaka huu.

Watoto hawa watakuwa zao la kwanza tangu Serikali izindue Mpango wa Maendeleo Makubwa Sasa, ambao katika upande wa elimu uzinduzi wake ulifanyika Agosti 15 mwaka huu.

Katika uzinduzi huo, maofisa elimu walikula kiapo cha kutekeleza mpango huo, ambao baadhi ya matokeo yake yanatakiwa kuanza kuonekana mwaka huu.

Moja ya matokeo ambayo maofisa elimu hao wameapa kuwa yataonekana kuanzia mwaka huu ni kupandisha ufaulu wa mtihani wa darasa la saba mwaka kutoka asilimia 31 mwaka jana mpaka 60 mwaka huu.

Pia wameapa kupandisha ufaulu wa mtihani wa kidato cha nne kutoka asilimia 43 mwaka jana mpaka asilimia 60 mwaka huu.

Katika malengo hayo pia, watendaji hao waliapa kufikisha ufaulu wa asilimia 70 kwa mwaka 2014  kutoka 60 za mwaka huu, na hatimaye ufaulu wa asilimia 80 au zaidi ifikapo mwaka 2015.

Wasemavyo wadau

Baadhi ya wadau wa elimu wana wasiwasi na  mafanikio ya haraka ya  mpango wa matokeo makubwa kama baadhi ya watu serikalini wanavyotaka kulazimisha kupatikana tena ndani ya muda mfupi wa utekelezaji wa mpango.

Mkuu wa shirika lisilokuwa la Kiserikali la Twaweza, Rakesh Rajani, anasema kuwa mpango ni mzuri ila unaweza kukwazwa na muda ulitolewa, hasa unapokuwa mchache.

“Kuwa na malengo ni muhimu kutawasaidia hata walimu kufanya kazi kwa malengo yaliyopo, ni vyema kwanza tungejua ni lini hiyo mikakati ilianza utekelezaji wake,” anasema.

Aidha, anashauri ili mambo yaweze kwenda vizuri, hatuna budi kuzingatia utaalamu zaidi badala ya kuingiza siasa hasa katika masuala yahusuyo utekelezaji wa mipango.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Profesa Tolly Mbwete ana shaka kama mpango huo unaweza kufanikiwa, kwani baadhi ya wadau muhimu akiwamo yeye hawakushirikishwa.

Anasema:  “Mimi kama  Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu kikubwa kuliko vyote nchini sijashirikishwa hata kidogo kwenye  mpango huu, sijui hata hayo matokeo makubwa yatatoka wapi kama wadau kama sisi hatujashiriki.

Anaongeza: “ Are they serious (wako makini?) Kweli hawa watu, hiyo big result now (matokeo makubwa sasa) itatoka wapi sijui. Wanasema ushirikishwaji kwenye mipango ni muhimu, lakini mimi sikushiki hata kidogo, waulize kama waliniita kwenye hata kikao kimoja.’’

Akizindua mpango huo, Waziri wa Elimu Dk Shukuru Kawambwa alisema kuwa utekelezaji wa mikakati katika sekta ya elimu ulianza tangu Aprili 17 mwaka huu.

Baadhi ya mambo ambayo anasema kuwa yameshatekelezwa ni pamoja na kukamilisha kitabu cha kiongozi cha usimamizi na uendeshaji wa shule za msingi na sekondari.

Jambo jingine analosema ni kuandaliwa kwa rasimu ya moduli ya ufundishaji wa stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu na kitabu cha mwalimu cha kufundishia (Teachers Hand Book) kwa masomo ya English, Biolojia, Kiswahili na Hisabati.

Pia anasema wizara imekusanya mitihani ya Taifa ya kidato cha nne na darasa la saba ya miaka ya nyuma (2008 – 2012) kutoka Baraza la Mitihani la Taifa. Mitihani hiyo imepelekwa kwa maofisa elimu kwa minajili ya kusambazwa shuleni.

Kwa mujibu wa Dk Kawambwa haya na mengineyo ndiyo yaliyokwishatekelezwa kuanzia Aprili. Kwa hali ilivyo matunda ya mikakati hii lazima yaanze kuonekana mwaka huu kupitia mtihani wa darasa la saba.

Kutoka Aprili hadi Septemba ni muda mfupi kutekeleza mikakati mizito ya kuinua ubora wa elimu, ikiwamo kukuza kiwango cha ufaulu. Baadhi ya watu wana wasiwasi kuwa huenda matokeo ya mwaka huu yakapikwa ili tu kuwaridhisha wabunifu wa mpango! Tusubiri tuone.