KUTOKA LONDON : Watanzania tunalalamika nchi mbaya lakini tunapendwa majuu

Muktasari:

  • Tunavyojua tangia 2008 mfumo wa uchumi duniani umeathirika, hivyo karibuni wamezuka matajiri wapya wa China, Urusi na Uarabuni wanaonunua si tu majumba bali kampuni kubwa Uingereza zikiwamo klabu mashuhuri za mpira kama Chelsea na Manchester City.
  • Ndani ya kasheshe hii karo za vyuo zilipandishwa 2010 na vijana wanaosoma sasa tayari wameshaanza kujilimbikizia madeni. Maskini na wageni wamesukumwa nje ya baadhi ya vitongoji na kati ya matatizo makubwa ni nyumba za kupanga.

Miezi ya karibuni nimefanya shughuli na wasamaria wema London. Wasamaria weupe kwa weusi.

Tunavyojua tangia 2008 mfumo wa uchumi duniani umeathirika, hivyo karibuni wamezuka matajiri wapya wa China, Urusi na Uarabuni wanaonunua si tu majumba bali kampuni kubwa Uingereza zikiwamo klabu mashuhuri za mpira kama Chelsea na Manchester City.

Ndani ya kasheshe hii karo za vyuo zilipandishwa 2010 na vijana wanaosoma sasa tayari wameshaanza kujilimbikizia madeni. Maskini na wageni wamesukumwa nje ya baadhi ya vitongoji na kati ya matatizo makubwa ni nyumba za kupanga.

Mbali na misaada wafadhili hawa hujaribu kuweka wananchi wanaodhalilika ndani ya orodha ya kupata kazi kwa kuwaongoza kuzisaka au kuwahimiza waende kuzifanya. Misaada hiyo haina maana kwamba wanaofadhilika (weusi kwa weupe) watakaa maisha yao yote wakipewa vitanda na msosi chee tu.

Sasa mbali na wahudumu waliomo katika mashirika haya wapo wananchi wanaojitolea, bila mishahara. Hawa huja mara moja kwa juma, wakipeana zamu, kupika, kusafisha nguo, kutoa ulinzi hata kuwa sikio kwa waathiriwa. Wapo waathirika waliotesana na wake au waume zao, vilema, walemavu wa akili, wasiosoma shule, waliobakwa au wenye shida za upweke. Wasamaria huwa sikio lao...

Sasa katika moja ya hizi shughuli niliongea na waliojitolea na kila mmoja wao alishtuka nilipoitaja Tanzania. Ndani ya miaka 20 niliyoishi Uingereza nimeshuhudia namna wimbi la jina la Tanzania linavyozidi kupepea. Zamani Kenya ilijulikana kwa utalii na Afrika Kusini ikafahamika kwa rabsha za ubaguzi wa rangi na mbali.

“Jambo gani linalokufanya uipende Tanzania vile?” Nilimuuliza mmoja wa kina mama mzawa wa Antigua. Kisiwa hiki kiko bahari ya Atlantiki, ghuba ya Caribbean. Si mbali na Jamaica, Martinique, Puerto Rico na Haiti.

“Naipenda sana Tanzania. Ndugu zangu wengi wamewahi kwenda kule. Mimi mwenyewe nilitembelea mbuga za wanyama na kufanya kazi ya kujitolea na wanawake wenye Ukimwi na watoto wa yatima. Nyinyi Watanzania mmetulizana sana. Halafu Tanzania ni nchi ya amani huisikii ikiwa na tafrani kama sehemu nyingine. Hebu nikuulize. Inakuwaje Afrika yote ina vurugu kila mahali na nyinyi hamna?”

Ili mradi alitaka kufahamu. Ikabidi alezwe kiini. TANU kugombea Uhuru kwa amani, Mwalimu Nyerere kuzingatia ujenzi wa nchi kwa kilimo vijijini. CCM kuendeleza fikra hizo. Uchaguzi wa kidemokrasia. Kupitia awamu kadhaa hadi sasa Rais John Magufuli.

“Huyo Magufuli sijawahi kumsikia. Nitaangalia YouTube nimwone. Ah....alishinda tuzo la kiongozi bora Afrika mwaka jana? Safi sana. Tanzania ni mfano mzuri. Nilipokuwa huko sikufaidi sana kuongea na wananchi. Nilitegemea wakalimani. Sasa hivi nahudhuria madarasa la Kiswahili kusudi nitakapokwenda tena niwasiliane na wananchi. Nyinyi Watanzania watu wazuri sana. Tanzania inatia moyo ...”

Mama akaendelea kusema muda wote tuliokuwa pale. Akaelezea mikakati yake. Kusaidia kinadada wenye Ukimwi na watoto yatima. Akasema yeye si tajiri, amestaafu (ana miaka sitini) lakini atajitolea kuendeleza Afrika, walikotoka mababu na mabibi zake.

Tovuti : www.freddymacha.com