Watanzania wanavyofanya kweli Marekani, watwaa ubingwa

Muktasari:

  • Kuchukua kwao ubingwa huo, kumeifanya timu ya Watanzania hao kupata nafasi ya moja kwa moja kwenda kushiriki mashindano ya mabingwa wa kanda mbalimbali nchini humo.

Wachezaji wa Kitanzania wanaocheza soka Marekani, Daud Aboud na Adolf Bitegeko wameiwezesha timu yao ya LCC Men’s Soccer kuchukua ubingwa wa ligi ya Golden Valley Conference.

Kuchukua kwao ubingwa huo, kumeifanya timu ya Watanzania hao kupata nafasi ya moja kwa moja kwenda kushiriki mashindano ya mabingwa wa kanda mbalimbali nchini humo.

Spoti Mikiki imefanya mawasiliano na vijana hao ambao wamezungumza mengi kuhusu namna walivyochukua ubingwa huo.

“Asante ila natanguliza shukrani zangu za dhati kabisa kwa Mungu ambaye amekuwa akitusaidia, pili Spoti Mikiki kwa kuwa pamoja na sisi kwenye kila hatua yetu, mmetuongezea uthamani mbele ya macho ya Watanzania.

“Hatuna uwezo wa kuwalipa ila mbarikiwe sana, furaha yangu ni kushinda, haikuwa kazi nyepesi lakini imewezekana,” anasema Daud ambaye awali alikuwa na Mtanzania mwingine, Ronald Mkaramba ambaye kwa sasa yuko TUMUT FC iliyoko Jimbo la Texas, Marekani.

“Daud nimekuja huku, nilimweleza sipendi kushindwa na niliwataka wachezaji wenzangu tushirikiane ili kwa pamoja tufanikishe kuwa mabingwa ndicho kilichotokea,” anasema Bitegeko aliyeanzia soka yake katika kituo cha vijana cha Azam kilichoko Chamazi.

Msimu ulivyoanza

“Dalili za kutwaa ubingwa zilianza kutokea, timu yetu ilikuwa imefanyiwa maboresho kwa kuongezwa wachezaji kadhaa ambao walikuwa wanaonekana wana uwezo, hapo ilikuwa bado hajafika Bitegeko.

“Kila timu ilikuwa inataka kuanza vizuri msimu hivyo ilibidi tufanye kazi ya ziada kupata matokeo ya ushindi kwenye michezo yetu ya mwanzoni mwa msimu,” anasema Daud.

Daud amefunga mabao saba na kutengeneza 10 huku Bitegeko ambaye hakuuanza msimu na timu hiyo akifunga mabao matano na kutengeneza mengine matatu.

Ushindani ulivyo

“Japo tumepoteza mchezo mmoja na kutoka sare mitatu, ila ushindani ulikuwa mkubwa sana, ujue kuna watu ukiwaambia tumepoteza mchezo mmoja pekee anaweza kudhani kuwa ligi ni nyepesi,” anasema Daud

“Ushindani ulikuwa wa pande mbili, wa kwanza ni ule wa timu yangu na hizo nyingine, pili ni mimi binafsi ambao ulikuwepo kuhakikisha napata nafasi ya kucheza mara kwa mara.

“Nilipofika nilikuta ligi inaendelea hivyo ilibidi nijitume sana ili niwe napata nafasi ya kucheza,nilicholenga nilifanikiwa hivyo kiujumla ushindani wa ndani ya timu umenijenga pili wa ligi umetufanya kuwa bora zaidi ndiyo maana tumekuwa mabingwa,” anasema Bitegeko.

Chachu ya ubingwa

“Kuna uwezo wa wachezaji binafsi, mbinu za makocha pamoja na muunganiko wetu wa uchezaji, matokeo ya yote hayo naamini yametufanya kuchukua ubingwa,” anasema Bitegeko ambaye ni mchezaji wa zamani wa Azam.

“Kilichotukwamisha msimu uliopita ndicho ambacho kocha wetu amekifanyia kazi, ninaamini sana kupitia mbinu vingine ni ziada japo vinaweza kuchangia kwa kiasi chake upatikani wa matokeo,” anasema Daud.

Mawakala wawanyemelea

“Kibaya au kizuri ni kwamba tupo chini ya LCC Men’s Soccer hivyo suala la kuchuliwa kwa kipindi hiki ni gumu kwa sababu tupo kwenye mafunzo, tukishahitimu tutakuwa huru kuuzwa au kutafuta timu za kujiunga nazo.

“Mfano, mimi nina madili matatu mpaka sasa lakini siwezi kwenda huko kwa sababu sijahitimu, mbali na kucheza kwetu soka nadhani unakumbuka kama hapa tunapata masomo ya kawaida hivyo sio rahisi kuondoka.

“Ukisema uondoke, ina maana unakuwa umekatisha masomo ambayo baadaye yanaweza kuja kuwa msaada hasa baada ya kumalizika maisha ya mpira, kiufupi mawakala wapo ambao wananisumbua,” anasema Daud.

Ishu za wachumba zikoje?

“Ha ha ha ha ha!! umenifanya nifurahi aisee, mimi ni mgeni labla mwenzangu Daud ambaye nimemkuta,kingine hata watu ninao fahamiana nao ni wachache na hakuna hata msichana mmoja ambaye nina mazoea naye,” anasema Bitegeko.

“Wasichana wapo wengi sana, kati ya vitu ambavyo huwa najiepusha navyo ni hao, najua ili kufikia malengo ninayoyataka ni lazima nijitunze, ngoja nikwambie jambo tangu nifike huku sijawahi kuwa na mahusiano ya kimpenzi na msichana yeyote.

“Nikiendekeza hapa hayo mambo inamaana nitakuwa nacheza na maisha yangu, wazazi,ndugu jamaa na marafiki wamekuwa wakinisisitizia kufanya kilichonileta huku, sisemi kama sintokuwa na msichana hapana ila mpaka muda sahihi utakapofika,” anasema Daud.

Ratiba za siku

“Saa 12 alfajiri huwa tunapata chai na saa 1 asubuhi tunakwenda kufanya mazoezi binafsi kisha tukitoka huko tunajiandaa kwa ajili ya kwenda darasani, mida ya mchana, kuanzia saa saba ni kwenda mazoezini na timu.

“Baada ya mazoezi na timu, tunaamua siku moja moja kwenda kufanya mazoezi ya gym, hayo ni mazoezi ambayo huchukua saa moja kisha tunarudi nyumbani kuendelea na ratiba ndogo ndogo,” anasema Bitegeko.

“Hiyo ndiyo ratiba yetu ilivyo, vingine vinaweza kuwa vya kawaida mfano kucheza game, kuangalia muvi lakini vyote hivyo hufanyika tukiwa nyumbani,” anasema Daud.