UCHAMBUZI: Watendaji wamsaidie RC Makonda kufikia malengo

Mkoa wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

Muktasari:

Nimekuwa nikifuatilia juhudi zako tangu ukiwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, umekuwa na kiu ya kuona maendeleo yakipatikana jijini Dar es Salaam chini ya uongozi wako.

Kwanza ninapenda kukupongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa juhudi na shauku ya kutaka kuliboresha jiji kwa mikakati madhubuti unayoionyesha.

Nimekuwa nikifuatilia juhudi zako tangu ukiwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, umekuwa na kiu ya kuona maendeleo yakipatikana jijini Dar es Salaam chini ya uongozi wako.

Naamini jitihada zako za kutaka kuiboresha Wilaya ya Kinondoni, ndizo zilizomfanya Rais John Magufuli akuongezee majukumu baada ya kuona namna unavyochapa kazi na kuwa na kiu ya maendeleo.

Kwa muda sasa tangu Rais Magufuli akuteue umetoa mikakati ambayo itasaidia kuleta mabadiliko, lakini hatujui kikwazo kinachokwamisha jitahada hizo ni nini. Ni watendaji jiji au manispaa?

Kwa mfano, suala la ombaomba lilikuwa wazo zuri na lenye tija kwa kuwaondoa na kuwarudisha makwao, lakini kwa kipindi kifupi tumewaona tena wakirandaranda mjini.

Juni 13, 2016 ulikuja na mkakati juu ya wahamaji wapate barua za kumtambulisha mwananchi ambaye anahamia au anahama kwenda mtaa mwingine. Jambo hili lilikuwa zuri kwani lingepunguza uharifu unaoendelea hapa jijini.

Vilevile, mkakati wa kuwatengea wamachinga maeneo mapya ya biashara ulitoa agizo kwa Wakurungenzi wa Manispaa watenge maeneo kwa ajili ya biashara hizo, lakini mpaka naandika uchambuzi huu sijaona utekelezaji wowote na kama upo basi taarifa hazijafika kwa wananchi wengi.

Mkakati mwingine ulikuwa kwa wamiliki wa nyumba zilizochakaa wazipake rangi, lengo lako ni kulifanya jiji lionekane safi kuanzia mazingira ya nyumbani hadi kwenye barabara. Mkakati huu ulikuwa mzuri kwani ulilenga kuliweka jiji kuwa la kuvutia kwa wageni wanaokuja kutalii.

Pia, suala la usafi ulikuwa ni mkakati mzuri kupitia kaulimbiu yako ya ‘Naona Aibu’ yenye kulifanya jiji kuwa safi na mazingira yake yakiwa safi. Moja ya kauli zako ulisema “Hatuwezi kuwa wasafi wa mioyo kama tunaishi kwenye mazingira machafu kila mtu na aseme naona aibu. Ukipanda kwenye daladala ukaona uchafu sema naona aibu. Ukiwa mtaani kwako sema naona aibu.”

Lengo lilikuwa ni kuliweka jiji katika mazingira mazuri na yenye kuvutia.

Katika kuhakikisha kampeni hiyo inafanikiwa, ulitangaza kuanzisha mashindano kwa kila mtaa, ambapo mitaa yote ya jiji la Dar es Salaam itashindanishwa kwa usafi na mtaa utakaoibuka mshindi utapata zawadi ya kitita cha Sh5 milioni.

Nakumbuka Machi 15, 2016 siku mkiapishwa Ikulu, Rais Magufuli alitoa maagizo kwenu kuwa mtekeleze wajibu wenu bila kuwa na hofu yoyote kutoka kwa watu ikiwa ni pamoja na kuwashughulikia watendaji wote watakaonekana kuwa wazembe kwenye sekta zao.

Ni jukumu la watendaji wakuu wa jiji na manispaa kutekeleza mikakati hii, kwani itakuwa jambo la kushangaza kuona mikakati mizuri inakosa utekelezaji na kushindwa kufikia malengo ya mtoa mikakati.

Sina uhakika kama kuna mtendaji yeyote wa jiji na mji anayekwamisha utendaji wako uliotukuka, kama yupo basi atakuwa hapendi maendeleo.

Hivyo, ni muhimu ukaitisha mdahalo na wakazi, wakuu wa jiji na mji ili kupitia mdahalo huo uweze kuibua mbinu mbalimbali ambazo utaweza kuzitumia pamoja na wakuu wengine ili kuboresha jiji letu.

Naamini wakazi wa jiji hili hawafurahishwi na hali jinsi ilivyo kwa sasa na wangependa iwe nzuri zaidi kupitia mikakati yako niliyoitaja hapo juu iwapo utawaalika kwenye mdahalo watakupa ushirikiano mzuri.

Mchambuzi ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam anayesomea Shahada ya Kiswahili