Watoto wasioona mbali hawawezi kuandika licha ya kufundishwa

Muktasari:

Kwa kawaida jicho hufanya kazi ya kupitisha mwanga wenye taswira na kuupeleka kwenye ubongo ili iweze kutafsiriwa na muhusika kutambua kitu anachokitazama.

Kutoona karibu hyperopia au farsightedness ni miongoni mwa matatizo ya macho yanayowakabili wengi. Watu wenye tatizo hili hutofautiana kiwango chao cha kutoona karibu.

Kwa kawaida jicho hufanya kazi ya kupitisha mwanga wenye taswira na kuupeleka kwenye ubongo ili iweze kutafsiriwa na muhusika kutambua kitu anachokitazama.

Ili zoezi hili liweze kufanyika ni lazima jicho lipokee mwanga wenye taswira na kuuelekeza sehemu husika ndani ya jicho ili usafirishwe kupitia mshipa maalum wa fahamu kwenda kwenye ubongo kwa ajili ya kutafsiriwa na kukamilisha utambuzi wa kinachotazamwa.

Sehemu kuu mbili ambazo hufanya kazi ya kuhakikisha mwanga unaelekezwa katika njia sahihi ndani ni cornea; sehemu ya mbele ya jicho inayo ruhusu mwanga kupita na kuingia ndani, na lensi (lens) ambayo ipo sehemu ya mbele ila ndani ya jicho (karibu na cornea).

Mwanga wa taswira unayoitazama huingia jichoni kupitia cornea ambayo huuelekeza kupenya kwenye lensi ambayo huwa na uwezo wa kubadilika umbo kulingana na taswira ilipo kuhakikisha mwanga unapelekwa kwenye retina.

Baada ya mwanga huu kufika kwenye retina, yenyewe huchukua taswira iliyoletwa na kuipeleka kwenye ubongo kupitia mshipa wa fahamu unaoitwa Optic. Ikifika kwenye ubongo, hutafsiriwa kabla hujatambua unachokiangalia.

Sehemu ya mbele ya jicho inayoruhusu mwanga yaani cornea na lensi zikiwa hazina tatizo lolote basi mtu huweza kuona vitu vyote vile anavyovitazama bila kujali viko karibu au mbali.

Ikitokea hitilafu yoyote kwenye sehemu hizi mbili basi inakuwa vigumu kwa taswira kuelekezwa kwenye retina na mtu kutambua anachokitazama.

Zipo sababu ambazo huchangai mtu kushindwa kuona vitu kwa usahihi hasa vilivyo jirani. Miongoni mwa sababu hizo ni cornea kuwa bapa badala yenye mbinuko kidogo hivyo kukosa uwezo wa kuuelekeza mwanga kwenye lensi kisha retina.

Nyingine ni kuwa na macho madogo kwani lensi hushindwa kuuelekeza mwanga wa taswira kutua kwenye retina kutokana na udogo wa jicho au macho yote mawili.

Tatizo hili huwakumba zaidi watu wenye matatizo ya macho hasa wenye tatizo la kushindwa kuona vitu vilivyo mbali yaani ‘shortsightedness.’ Wengine wanarithi kutoka kwa wazazi wao au wazee ambao uwezekano wa kupata tatizo hili ni mkubwa kwao.

Dalili

Kuna baadhi ya dalili zikijitokeza ni ishara ya tatizo la macho hivyo unahitaji kuchukua hatua za haraka kuzishughulikia. Kama unatumia nguvu nyingi kutambua kitu unachokiona jirani yako ukilinganisha na vilivyo mbali nawe unapaswa kutafakari.

Hali hii ya kutumia nguvu kubwa kuona vitu hivyo husababisha kichwa kikuume kwa muda mrefu unapotaza vitu vilivyo karibu sana kama vile unaposoma kitabu.

Wengine huhisi kuchoka sana baada ya kutazama vitu vilivyo karibu yao au kushindwa kuona vitu vilivyo karibu sawasawa. Macho kuuma na kukunja sura au kufinya macho ili uweze kuona vizuri vitu vilivyo karibu yako nayo ni dalili ya tatizo hili.

Kwa watoto hali inaweza kuwa tofauti kidogo na watu wazima. Wao wanaweza wakapata makengeza kutokana na changamoto ya kushindwa kuona vitu vilivyo karibu yao.

Kwa wanafunzi, wapo wanaoshindwa kuandika hata baada ya juhudi za kufundisha kufanyika.

Kwa wale wenye dalili hizi au wenye matatizo kila wanapojaribu kutazama vitu vilivyo karibu yao, ni vyema wakaenda kumuona daktari wa macho kwa ajili ya kufanya vipimo na kujua chanzo cha tatizo linalowakabili.

Matibabu

Watoto wadogo huweza kutibiwa tatizo hili kirahisi na kwa muda mfupi kwa kurekebisha chanzo cha kushindwa kuona vitu vya karibu tofauti na mtu mzima.

Watu wazima hupewa miwani maalumu ambayo huwasaidia kuweza kuelekeza mwanga kwenye sehemu ya mbele ya jicho vizuri na kurahisisha kazi ya cornea na lensi kuelekeza mwanga wenye taswira uweze kutua kwenye retina vizuri.

Ikibidi, mgonjwa hufanyiwa upasuaji wa kurekebisha lensi kwa wenye tatizo hilo. Kwa bahati mbaya upasuaji huu bado si salama sana hivyo watu wachache wasioona karibu hutibiwa kwa njia hii.

Kwa kawaida uvaaji wa miwani huwa hauna tatizo lolote kama tu vipimo vilifanyika vizuri na ukubwa wake ukajulikana na mgonjwa akapewa miwani inayoweza kusaidia kwa kiwango kinachohitajika.

Changamoto nyingi huonekana kwa wale wanaopimwa (au wasiopimwa) na kupewa miwani ambazo hazitatui tatizo kama inavyopaswa kuwa. Inawezekana miwani ikasababisha mwanga wenye taswira usitue kwenye retina hivyo kuendelea kusababisha tatizo.

Kinga

Kwa bahati mbaya hakuna njia ya moja kwa moja ya kujikinga na tatizo hili bali kuhakikisha unapima macho yako mara ili kugundua tatizo baada ya kuhisi moja au zaidi ya dalili zilizobainishwa kila unapojaribu kutazama vitu hasa vilivyo jirani nawe.

Ukiwahi matibabu husaidia kujikinga na madhara yanayoweza kujitokeza kwa kutotibiwa.

Kwa wenye maradhi ya muda mrefu kama vile kisukari, ni muhimu kuwa makini na macho kwani huweza kuathiri sehemu nyingine za mwili na (kisukari cha macho) husababisha upofu kwa mgonjwa lakini madhara yake yanaweza kupunguzwa matibabu yakianza mapema.