MAONI YA MHARIRI: Waziri Tizeba kutana na wadau wa mbolea

Waziri wa Kilimo na Mifugo, Dk Charles Tizeba 

Muktasari:

Serikali ya Awamu ya Tano tangu imeingia madarakani lengo lake kubwa ni kusaidia wananchi wa kipato cha chini, wakiwamo wakulima. 

Gazeti hili toleo la jana lilikuwa na habari iliyohusu malalamiko ya wadau wa kilimo kuhusu uamuzi wa Waziri wa Kilimo na Mifugo, Dk Charles Tizeba wa kupitisha kanuni mpya za uagizaji wa mbolea kwa mkupuo (bulk procurement) kupitia tangazo lake alilolitoa kwenye gazeti la Serikali namba GN 49 ya mwaka 2017.

Serikali ya Awamu ya Tano tangu imeingia madarakani lengo lake kubwa ni kusaidia wananchi wa kipato cha chini, wakiwamo wakulima.

Wakati kilimo kinatajwa kuchangia asilimia 50 ya pato ghafi la taifa, huku kikibeba zaidi ya asilimia 76 ya nguvu kazi nchini bado kumekuwa na malalamiko mengi kuhusiana na ukuaji wake.

Miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakizungumzwa na watendaji wa Serikali ni kumuwezesha mkulima kupata pembejeo kwa urahisi na kwa gharama nafuu.

Hata hivyo, pamoja na nia njema ya Serikali ikiwamo kuanzisha utaratibu wa uagizaji wa pamoja wa mbolea utakaompa nafuu mkulima, bado kuna kasoro zinazolalamikiwa hasa katika uandaaji wa kanuni.

Baadhi ya wakulima na mashirika yasiyo ya kiserikali wanasema waziri mwenye dhamana na kilimo na mifugo hakutenda haki kwa kutowashirikisha kikamilifu katika uandaaji wa kanuni hizo.

Wadau hao pia wanalalamika kwamba kupitishwa kwa kanuni hizo kumeifanya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea nchini (TFRA), inayosimamia soko la mbolea nayo kuwa mfanyabiashara.

Pia, wadau hao wanalalamika kuwa kanuni hizo zimejumuisha mahitaji yote ya mbolea kwa pamoja bila kujali tabia za ardhi kulingana na maeneo.

Wanasema mbolea siyo kitu kinachofanana kama mafuta, kuna tabia mbalimbali za ardhi kulingana na kanda nane zilizopo nchini, hivyo ushiriki wao wanadhani ungekuwa na tija katika kuboresha namna ya uagizaji kwa manufaa ya wakulima wote.

Pia, wanahoji iwapo kanuni zimezingatia maeneo ya uzalishaji wa mbolea duniani kama vile Afrika Kusini, Morocco na China na kama uagizaji huo wa pamoja umeangalia namna gani unafuu wa gharama kwa mkulima utakavyokuwa.

Malalamiko hayo yanatiwa nguvu na majibu ya Waziri Tizeba mwenyewe kwa gazeti hili yaliyohoji kama wadau hao waliambiwa (yeye waziri) amepitisha kanuni mbaya na kama wamezisoma.

Hoja zinazotolewa na wadau hao zinaonyesha mapungufu ya kutoshirikishwa katika uandaaji wa kanuni hizo, hivyo ni muhimu kwa wizara kuangalia upya namna wanavyoweza kukaa na wadau hao na kuwashirikisha kwa kuwa wao ndiyo wanahusika moja kwa moja na wakulima.

Tunachokiona hapa ni vema wizara husika ikapitia upya uamuzi wake kwa kuondoa kasoro ambazo zimeanza kulalamikiwa na wadau wa sekta ya kilimo.

Si mara ya kwanza kwa wadau wa masuala kadhaa kulalamika kutoshirikishwa katika uamuzi unaogusa masilahi yao.

Waziri anaweza kuwa amefanya uamuzi sahihi na wenye lengo zuri, lakini katika dunia ya sasa jambo la muhimu zaidi ni ushirikishwaji. Na faida ya kufanya hivyo huwa ni kupunguza malalamiko na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.

Hivyo, tunadhani bado kuna nafasi kwa Waziri Tizeba kukutana tena na wadau wa kilimo kujadili kanuni hizo ili zilete manufaa kwa pande zote.