Weka mdomoni chakula kinakutosha, usizidishe

JULIETH KULANGWA

Muktasari:

  • Siku hiyo inapofika unaacha shughuli zako zote, kama ilibidi uhudhurie kikao au mkutano wa aina yoyote unaacha. Wakati mwingine unaomba ruhusa kazini ili ukakamilishe zoezi hilo. Muda unapofika fundi hatokei, ukipiga simu haipatikani.

Nadhani hili wengi wenu limewahi kuwakuta ingawa inaweza kuwa kwa namna tofauti. Kutokana na mabadiliko ya maisha na uvamizi wa sayansi na teknolojia kila kitu siku hizi kinaweza kufanyika mtandaoni.

Unawasiliana na fundi labda wa kukurekebishia kitu nyumbani, iwe ni nyaya za umeme, friji, televisheni au sakafu iliyopasuka. Mnakubaliana kuwa atafika Jumamosi kufanya ukarabati huo.

Siku hiyo inapofika unaacha shughuli zako zote, kama ilibidi uhudhurie kikao au mkutano wa aina yoyote unaacha. Wakati mwingine unaomba ruhusa kazini ili ukakamilishe zoezi hilo. Muda unapofika fundi hatokei, ukipiga simu haipatikani.

Au unahitaji huduma kwa ajili ya ofisi yako unamtafuta mtoa huduma. Unatangaza zabuni, mmoja anashinda  mnakubaliana na malipo ya awali unampa lakini baada ya muda hapokei simu, ananapopokea anakuwa na visingizio lukuki.

Kuna huduma unaitaka lakini unagundua kuwa ili uipate ni lazima ukasubiri katika foleni ndefu ya watu, iwe benki, hotelini au dukani.

Tatizo ni nini? Tatizo ni hawa wanaojiita wajasiriamali au wafanyabiashara hukubali wateja ambao hawawezi kuwahudumia kwa madai kuwa wanajaribu kuinyakua kila fursa inayokuja mbele yake.

Hii haina tofauti na mtu anayekula chakula kingi mdomoni kiasi cha kushindwa kuufunga wakati akitafuna na kuwachefua wenzake.

Fundi anaposhindwa kutokea kwa wakati, hata kama atakufanyia kazi nzuri ya namna gani huwezi kumtumia tena.

Siku hizi watu hawapendi kuhudhuria matamasha kwa sababu mwanamuziki anapanda jukwaani usiku wa manane akiwa amelewa . Hivi ni sahihi msanii kupanda jukwaani na kujishikashika maungo na suruali na kofia yake?

Nadhani msanii anaonekana vizuri zaidi katika video kwa kuwa anakuwa amevalia nadhifu, kichwa kipo safi hakina kilevi na anajituma tofauti na akiwa jukwaani.

Muigizaji wa filamu anaigiza ndani ya maigizo badala ya kuifanya kazi hiyo kwa umakini na kumfanya mtazamaji ahisi anatazama maisha halisi. Anaigiza kama vile ana kazi nyingine inayomwingizia kipato na kuipuuza hiyo.

Jua kuwa biashara au kazi yako inabidi uifanye kwa umakini na uangalifu wa hali ya juu. Kila mtu anapewa nafasi moja ya kuthibitisha kuwa anaweza kufanya kazi yake au biashara vizuri.

Unapoaminiwa iwe katika kazi au biashara inabidi ulipe deni hilo kwa kufanya vizuri. Kuna hoteli nzuri, wasanii, wafanyakazi ambao sasa wamesahaulika. Huduma mbovu huondoa uaminifu.