Wengi hawafahamu namna ya kuepuka lehemu

Dk Shita Samwel

Muktasari:

Zipo aina mbili; lehemu mbaya (bad cholesterol) na lehemu nzuri (good cholesterol). Uwepo wa lehemu mbaya kwa kiwango kikubwa mwilini ndiyo chanzo cha kuharibika kwa mishipa ya damu hivyo kujitokeza kwa magonjwa yasiyoambukiza yakiwamo ya moyo na kiharusi

Lehemu au cholesterol ni aina ya mafuta yaliyopo mwilini ambayo yakizidi huwa na athari mwilini.

Zipo aina mbili; lehemu mbaya (bad cholesterol) na lehemu nzuri (good cholesterol). Uwepo wa lehemu mbaya kwa kiwango kikubwa mwilini ndiyo chanzo cha kuharibika kwa mishipa ya damu hivyo kujitokeza kwa magonjwa yasiyoambukiza yakiwamo ya moyo na kiharusi

Katika kufahamu namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza, kuna haja ya kuyatambua mambo ambayo tukiyafanya yatapunguza au kutuepusha na lehemu mbaya, ni miongoni mwa maradhi yanayotokana na mfumo wa maisha.

Kufanikisha kujiondoa kwenye hatari za kupata maambukizi haya, ni muhimu kubadili tabia hatarishi hasa ulaji holela holela wa vyakula vyenye kiasi kikubwa cha lehemu.

Uwapo wa soko huria na utandawazi umechangia kuibuka kwa vyakula mbalimbali vya kimagharibi ambavyo ulaji wake holela huweza kuchangia kuongezeka kwa lehemu mbaya mwilini.

Vyakula vya kuepukwa ni pamoja na nyama zenye mafuta mengi hasa nyekundu zitokanazo na mifugo kama vile ng’ombe, mbuzi na nguruwe. Ieleweke kuwa nguruwe si nyama nyeupe kama ambavyo watu wengi wamekuwa wakiamini kutokana na upotoshaji unaofanywa mtaani.

Huwa tunadhani kuwa kula au kununua vyakula katika migahawa mikubwa na supamaketi na nyama za kusindika ni jambo la kifahari bila kufahamu kuwa ndivyo vinavyoongeza hatari za kuongeza lehemu mwilini.

Takwimu zinaonyesha watu wengi ambao ni walaji zaidi wa migahawani ndio wanaopata magonjwa yatokanayo na lehemu kwani vyakula vilivyosindikwa ambavyo huuzwa zaidi huko vinaelezwa kuwa sababu.

Ni vizuri kuepuka vyakula hivyo kwani vina kiasi kikubwa cha lehemu. Vilevile ni vizuri kuepuka vyakula vya makopo hasa nyama, burger na piza.

Kula kwa wingi vyakula visivyo na lehemu ikiwamo mboga za majani, matunda, nafaka zenye nyuzilishe na zisizokobolewa, samaki, kuku bila ngozi yake na jamii ya kunde kama vile maharage kunde, mbaazi na choroko.

Inashauriwa kula zaidi samaki kwani kiasilia wana aina ya mafuta ambayo huweza kusaidia kufifisha lehemu. Vyakula vya kuchemsha, kubanika na kukausha ni vyakula ambavyo vinapunguza kiasi cha mafuta kilichopo ndani yake.

Epuka vyakula vya kukaangaa ambavyo hutumia mafuta mengi kuviandaa. Pika vyakula na mafuta ambayo hayana lehemu yaani yatokanayo na mimea ikiwamo ya alizeti, mawese na pamba.

Fanya mazoezi mepesi ikiwamo kutembea, kukimbia, kucheza mziki na kuogelea. Inashauriwa kufanya mazoezi mepesi angalau kwa dakika 30 mpaka 40 kwa siku na mara tano kwa wiki.

Mazoezi yanasaidia kupunguza mafuta mwilini kwani huchomwa kuipata nishati ya mwili inayotumika wakati wa mazoezi.

Fanya uchunguzi wa afya mara kwa mara angalau mara moja kila baada ya miezi sita kwani inasaidia kubaini kama una wingi wa lehemu mwilini. Faida ya ugunduzi wa mapema ni kujihami na kuchukua hatua kabla madhara makubwa hayajatokea.

Wanaotoka kwenye historia ya maradhi haya ni vizuri wakachukua tahadhari mapema kwa kujiepusha na vihatarishi vyote na kutumia njia zinazoshauriwa kukabili wingi wa lehemu.

Kwa ujumla, kubadili mfumo wa maisha hasa aina ya vyakula na kufanya mazoezi ni kinga madhubuti dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.