Wengi huishia hatua ya tatu kati ya tano za penzi

Muktasari:

  • Kila mmoja wetu hushangaa na kuchanganyikiwa akifikiria kwa nini mapenzi ambayo yanaonekana kunoga kiasi hiki yanaishia kwenye machungu na majuto kiasi hiki. Kwa nini muda mzuri tuliouwekeza kwenye mioyo ya wapenzi wetu unaishia kupotea kihasara namna hii?

“Inawezekana hakuwa wa kwangu”, “Yamkini Mungu hakupanga tuwe pamoja”, “Labda Mungu ameniepushia mengi”. Mara kwa mara wengi tumesikia sentensi zinazofanana na hizi hususani kwenye vinywa vya watu, marafiki au ndugu zetu ambao wamewahi kuachana, kutengana au kuvunja mahusiano.

Kila mmoja wetu hushangaa na kuchanganyikiwa akifikiria kwa nini mapenzi ambayo yanaonekana kunoga kiasi hiki yanaishia kwenye machungu na majuto kiasi hiki. Kwa nini muda mzuri tuliouwekeza kwenye mioyo ya wapenzi wetu unaishia kupotea kihasara namna hii?

Jambo hili huwatatiza wengi sana na yamkini wewe ni mmoja wao. Tafiti za kisaikolojia kwenye eneo la mahusiano pamoja na yale mengi tunayokutana nayo kwenye kuwashauri wapenzi na wanandoa wengi yametufanya kufikia hitimisho kwamba mapenzi huwa yana hatua zake na kwa bahati mbaya wapenzi wengi wanashindwa kuziendea hatua hizo moja baada ya nyingine badala yake wanaishia njiani, kama nilivyosema kwenye utangulizi kwamba wengi huishia hatua ya tatu. Fuatana nami katika makala hii uzielewe vizuri zaidi hatua hizi zitakazokusaidia sana.

Kuingia katika penzi

Hii ni hatua ya mwanzoni kabisa wakati umekutana na mtu ambaye unaona kama ni ndoto yako imekuwa dhahiri. Mtu uliyemtamani kwa muda mrefu sana. Hapa unajihisi mwenye furaha kuliko mtu yeyote yule. Hisia zako zote zinatawaliwa na mihemko ya kuwa na huyo unayemfia.

Kila wakati na kila sehemu unatamani kuwa na huyo. Unamwona na kumuhisi yeye kuwa vyote katika vyote kwenye maisha yako. Hata afanye kosa la aina gani wewe unaliona ni jema tena lenye kuvutia. Hata kama ni mchafu na mwenye harufu mbaya wewe hautoona hilo kamwe. Hii ndio hatua ambayo binti huambiwa kwamba huyo kijana anayekuchumbia ni mwizi au ana wanawake wengi na akajibu “kwani hata mimi si mwanamke?”

Wengine ukiwaambia mabaya ya kweli ya wapenzi wao wanakwambia Mungu atambadilisha. Hapa daima utamwamini huyo mpenzi wako katika kila asemalo hata kama unaambiwa uongo, na pia moyoni mwako unahisi kwamba huyo mtu ana uwezo wa kuzitimiza ahadi zote alizokwambia na kila matamanio na ndoto zako ana uwezo wa kukuletea.

Katika hatua hii hauko tayari kurudishwa nyuma na mtu yeyote, awe mzazi wako, ndugu yako wa damu, walimu wako, mchungaji au shehe wako au hata Mungu mwenyewe. Unachojua ni kimoja tu. Nampenda huyu, basi.

Kuwa wapenzi

Katika hatua hii mapenzi yamepevuka sana na ile mikutano ya hotelini, kwenye migahawa au kutembeleana mara kwa mara inabadilishwa kwa kuamua kuanza kuishi pamoja. Sasa hapa kama ni watu wa dini ndio watafunga ndoa za makanisani au misikitini, wengine bomani, wengine za mila n.k ili mradi waanze kuishi pamoja kama mke na mume. Kufahamiana kunazidi na unaanza kumjua mwenzako kwa kina zaidi hususani baadhi ya vitu ambavyo mwanzoni ulishindwa kuvijua kuhusu yeye. Uwepo wako unaanza kuwa na umuhimu mkubwa kwenye maisha ya mwenzako. Ndani yenu mnaanza kuhisi umoja na furaha ya kipekee. Kila kitu kikienda sawa, baada ya miezi au miaka michache kipindi hiki kinaweza kuwaleteeni mtoto ambaye anaweza kuiongeza furaha baina yenu. Hapa mwanamke anajihisi salama zaidi ya wakati akiwa hana mtoto na mwanaume anajiona ana jukumu la kuwalinda mama na mtoto. Hisia za kuyapenda majukumu huanza na ulazima wa kujibidisha huongezeka. Mara nyingi furaha na ule umoja inapoongezeka kila mmoja anahisi hakukosea kumpenda mwenzake na kwamba kila mmoja amekuja kwenye maisha ya mwenzake kwa sababu sahihi.

Machungu ya kuhisi ulikosea

Katika hali ya kushangaza kabisa, katika kipindi hiki upepo unaanza kubadilika na kama ni safari ya baharini basi mnaanza kuona mawimbi yakivuma kwenye chombo chenu. Ndani yako unaanza kuona yale matumaini uliyokuwa nayo kwenye hatua ya kwanza na ya pili yanaanza kuzama.

Kuna vitu zamani ulikuwa ukiviona vidogo tu kwenye tabia za mwenzako, ulikuwa ukiviona kama njiti, sikuhizi unaanza kuviona vikubwa kama misumari, na vinakuchoma kama moto. Vipindi vya hasira, kelele na kufokeana vinaanza kuingia kwenye mahusiano yenu.

Ila kwa mbali moyoni mwako au akilini mwako unaweza kuwaza labda iko siku hisi hisia zitaniisha ili nirudi kumpenda tena huyu mume au mke wangu. Katika kipindi hiki wengi wanatoa sentensi za “tuachane kama tumeshindwana”, “kama umenishindwa nirudishe kwetu”, “nikirudi nisikukute” n.k.

Kiukweli katika hali na upepo huu ndani yako unahisi kabisa kwamba ulikosea kumchagua yeye, na wengine wanajutia kabisa uamuzi wao wa kuamua kuoana na yeye. Zile hisia za kumpenda, kumlinda, kumfurahisha na kumtetea mpenzi wako zinaenda na maji mbali kabisa, tena hutaki kabisa kumsikia, unatamani hata asirudi nyumbani kwa jinsi anavyokuudhi.

Kama mwanzoni mlikuwa mnafurahia tendo la ndoa basi sasa ndio tendo hilo linaingia shubiri. Hutaki akuguse wala akusogelee. Kwa bahati mbaya vita hii na kutofautiana huku kunapozidi uwezekano wa michepuko huongezeka ambayo na hiyo huongeza vita na mchimbiko pale ambapo kunakugundulika.

Katika kipindi hiki kiu ya kuwa pamoja imekufa na kuzikwa kabisa, wengine wanatafuta maeneo ya kupumulia ilimradi asiwe nyumbani, wakushinda baa ndio anapotelea huko kabisa, wakushinda kazini ndio atakaa huko hadi usiku wa manane kama vile mfanyakazi bora kumbe ana maumivu, wakushinda makanisani basi ndiyo utadhani kaambiwa Yesu anarudi kesho kumbe anamkimbia mwenza wake. Yaani kushoto na kulia kote kunakuwa shubiri.