Wimbi la madiwani Chadema kuhamia CCM ni njaa, ukata au?

Muktasari:

  • Licha ya kamba, wasemaji wengi wanalihusisha sakata la wimbi hili na mambo mengi kadha wa kadha. Wapo wanaojiuliza hivi, ni njaa inayosababisha haya, ni ile hali ya ukata uliokithiri na kuwagubika wananchi kila mahali au ni kule kurubuniwa tu? Ila jibu halijapatikana bado.

Wimbi la kuhama kwa madiwani wa Chama Cha Demokrasia (Chadema), kwenda CCM hivi karibuni limekuwa kubwa na kushika kasi kipindi hiki. Kiasi kwamba, sasa limewaachia maswali mengi yaliyokosa majibu wananchi wengi, huenda kuliko wakati mwingine katika awamu zilizotangulia.

Licha ya kamba, wasemaji wengi wanalihusisha sakata la wimbi hili na mambo mengi kadha wa kadha. Wapo wanaojiuliza hivi, ni njaa inayosababisha haya, ni ile hali ya ukata uliokithiri na kuwagubika wananchi kila mahali au ni kule kurubuniwa tu? Ila jibu halijapatikana bado.

Hivi karibuni, madiwani wa Chadema kutoka mikoa ya Iringa na Arusha, ndiyo miongoni mwa wahanga wakuu waliokumbwa na kimbunga hicho cha hama-hama na kuwaachia wananchi viulizo vingi bila kupata majibu ya msingi.

Kwa mfano, Julai 11 mwaka huu aliyekuwa diwani wa Kata ya Ngabobo (Chadema) Wilaya ya Meru mkoani Arusha, Solomon Laizer. Aliandika barua ya kujiuzulu udiwani na kujiunga na CCM.

Sababu kubwa ya diwani Laizer kama alivyonukuriwa na vyombo vya habari, ni kuunga mkono jitihada za utendaji wa Rais John Magufuli.

Sababu ambazo Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari, aliwahi kuzikanusha vikali kabisa. Ambapo yeye mbunge Nassari alisema kuwa, kujiuzulu kwa diwani huyo ni mwendelezo uleule wa michezo michafu inayochezwa na chama kikongwe cha CCM; akidai diwani huyo eti amenunuliwa.

Kimsingi, wananchi hatuwezi kuzikubali sababu hizi moja kwa moja kama zilivyotolewa na Nassari; lakini pia ni vigumu kuzikana na kukubaliana moja kwa moja na sababu za diwani Laizer, mpaka pale ushahidi utakapodhihirishwa bayana.

Akionyesha uhakika wa anachokiongelea, mbunge kijana Nassari alisema, tayari walipata taarifa za diwani huyo kushawishiwa kujiuzulu kwa ‘kitu kidogo’ na kwamba, eti aliwahi kufuatwa na viongozi wa wilaya na kada wa chama hicho. Ambaye inadaiwa ndiye aliyetumika kwenda kumshawishi diwani huyo.

“Baadaye alieleza hataondoka lakini naona wamefanikiwa kumshawishi, tunashangaa viongozi wa Serikali badala ya kufanya kazi za maendeleo wanafanya kazi za kushawishi madiwani wa upinzani kuhama,”alisema Nassari.

Nassari aliyasema hayo akisisitiza kuwa, Laizer ni diwani wa tano katika Halmashauri ya Meru kujiuzulu. Tena kwa kutoa sababu zilezile kama wengine kuwa, anamuunga mkono Rais Magufuli.

Madiwani watano mpaka sasa wa Chadema wanaodaiwa kujiuzulu, na kisha kujiunga na CCM ni pamoja na, Credo Kifukwe, aliyekuwa diwani wa Kata ya Murieti jijini Arusha.

Wakati wengine waliojiuzulu katika Jimbo la Arumeru Mashariki na kata zao, kama zilivyoainishwa kwenye mabano ni pamoja na, Anderson Sikawa (Leguruki), Emmanuel Mollel (Makiba), Greyson Isangya (Maroroni) na Josephine Mshiu (Viti Maalumu).

Wote hawa, walikihama Chadema na kwenda kujiunga na CCM kwa sababu zilezile zenye mwelekeo sawa.......kumuunga mkono Rais Magufuli. Hivi ndiyo siasa!

Lakini, wimbi hilo la kuhama kwa madiwani wa Chadema wanaohamia CCM, limeukumba Mkoa wa Iringa pia. Ambapo, Baraka Kimata,Theodora Mbata, Erick Muyungo na Raymond Kimata, wiki hii waliripotiwa kukihama Chadema rasmi na kujiunga na CCM; ikiwa ni miezi kadhaa tangu watangaze kujiuzulu; kwa kile walichosema kuwa walishindwa kuendana na tabia za ‘kidikteta’ za Mwenyekiti wao, Mchungaji Peter Msigwa, mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini.

Baadhi ya maneno waliyoyasema walipokuwa wakikaribishwa kwenye maisha mapya ni kama yafuatayo:

“Tutakitumikia ipasavyo CCM, kama tulivyokuwa tunakitumika Chadema. Na kuhakikisha kuwa CCM wanashinda chaguzi zote watakazo kuwa wanashiriki katika Manispaa ya Iringa,” walisema walipokuwa wakipokelewa.

Ni wazi na ni haki kabisa, kwa mwanachama yeyote na wa chama chochote kukihama chama alichoko kwa sababu zozote zile. Na ni haki ya kikatiba pia, kufanya hivyo na wala siyo dhambi wala kukiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; kwa kuwa kila mmoja anautumia uhuru wake kikatiba.

Isipokuwa, wasiwasi mkubwa madiwani hawa wanahama huku kukiwa na taarifa nyingi zilizozagaa za kurubuniwa kwa fedha.

Licha ya kwamba, suala hili na hasa linalowahusu madiwani wa kule Arusha, wanaodhaniwa kurubuniwa kwa fedha na baadhi ya viongozi wa Serikali; tayari lipo mikononi mwa vyombo vya uchunguzi kisheria; lakini nalo kama mengine linaleta maswali mengi kuliko majawabu.

Hasa kuwepo kwa ujumbe uliorekodiwa (clip) ukiwaonyesha baadhi ya viongozi wa Serikali na hasa, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexender Mnyeti, akipanga njama za kuwarubuni madiwani hao; huku akiwaahidi kuwapatia kazi na fedha mara baada ya wao kukubaliana na mpango ule.

Hilo sitalizungumzia sana. Isipokuwa, kama kashfa ile na ushahidi ule utakuwa na ukweli wowote; basi taifa litakuwa linakwenda kuangamia.

Kwa nini? Kwa sababu huu ni utaratibu mbaya, na ukiukwaji mkubwa wa matumizi mabaya ya madaraka; ombwe linalopigiwa kelele kubwa hapa nchini nyakati nyingi. Mara nyingi imedaiwa baadhi ya wateule wa rais, wamekuwa waraibu wa madaraka na kutumia visivyo.

Nikianza na upande wa viongozi wa Serikali waliopewa dhamana ya kuwatumikia wananchi. Ni mwiko na ni kosa la kiufundi, lisilopaswa kufumbiwa macho hata kidogo kwa kuzitumia vibaya ofisi za Serikali kuzibadilisha kwa sababu zao binafsi; kufanyia matendo yanayokinzana na utawala bora kiujumla.

Ikijulikana wazi. Viongozi wa Serikali, mara zote wanatakiwa wawe mfano kwa wanaowaongoza wakikemea vikali vitendo vya rushwa, ubadhilifu wa fedha za walipakodi, unyanyasaji kwa walio chini yao; na vitendo vingine vyovyote vinavyoonyesha kukinzana na utu kiujumla. Yaani wawe mstari wa mbele mara zote, wakiyavaa matendo mema.

Viongozi wa namna hiyo, hutofautiana kabisa na dhima pamoja na mipango ya nchi, hukinzana waziwazi pia na ilani za vyama vyao. Lakini wanakinzana pia na Katiba, inayokataza na kupinga vikali vitendo vya rushwa iwe kwa kiongozi yeyote au kwa raia.

Halikadhalika, baadhi ya nukuu za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, akikemea na kulaani vikali masuala na vitendo vya rushwa aliwahi kusema, “si kwamba enzi zetu rushwa ilikuwa haipo; hapana ilikuwepo isipokuwa tulikuwa wakali sana.....hatukumwachia hakimu kutoa adhabu,” anasema hayati Mwalimu Nyerere na kuongeza:

“Tukithibitisha kuwa ulikula au kupokea rushwa, ulikuwa ukienda jela na ukishatoka unatandikwa viboko 24. Viboko 12 wakati wa kuingia jela, na viboko 12 wakati wa kutoka ili ukamwonyeshe mkeo.”

Mwalimu Nyerere, alikuwa akiwahakikishia wananchi namna walivyokuwa wakiichukia rushwa tangu zamani enzi za utawala wake. Hivyo viongozi wanaotuongoza, wanatakiwa wamuenzi Mwalimu kwa vitendo na si kufanya maigizo.

0713/0765 937 378.

Adam Mwambapa