Wimbi la wapinzani kukimbia vyama vyao linaiumiza CCM

Muktasari:

  • Tukio la mwanasiasa kuhama chama matokeo ya moja kwa moja ni faida kwa kile ambacho kinampokea na hasara ya kule alikoondoka. Chama cha siasa huhitaji wanachama, hivyo kinapovuna watu wapya hayo ni matokeo chanya na kinapoondokewa na watu hiyo ni hasi inayotafsirika kwa urahisi.

Mwanasiasa anapoondoka kwenye chama chake cha siasa na kujiunga na kingine ni furaha kwa kile ambacho kimempokea. Hivi sasa CCM ipo ndani ya furaha kwa mavuno ya wanachama wapya kutoka vyama vya upinzani.

Tukio la mwanasiasa kuhama chama matokeo ya moja kwa moja ni faida kwa kile ambacho kinampokea na hasara ya kule alikoondoka. Chama cha siasa huhitaji wanachama, hivyo kinapovuna watu wapya hayo ni matokeo chanya na kinapoondokewa na watu hiyo ni hasi inayotafsirika kwa urahisi.

Hivyo basi kwa tafsiri hiyohiyo, matokeo ya sasa ya wimbi la wanachama kukimbia vyama vyao na kukimbilia CCM na kuviacha vya upinzani ambavyo walikuwa wanachama na viongozi, ina faida mbili zenye kuonekana, hizo ndizo zinawapa furaha CCM.

Mosi, chama cha siasa kinahitaji watu, kwa hiyo mavuno ya wanachama wapya maana yake kinaongeza mtaji wa kisiasa. Siku zote mhimili wa chama si majengo, ofisi wala rasilimali nyingine, nguzo kuu yenye kukipa uhai katika nyakati zote ni watu. Rasilimali ya uhai wa chama ni watu.

Pili, chama cha siasa kinapovuna watu hasa viongozi hujiongezea nguvu na imani. Wanachama waliopo hupata nguvu na imani kuwa wapo kwenye chama sahihi ndiyo maana kinakimbiliwa. Watu wa vyama vingine hushawishika kukiona ni chama bora chenye kustahili kufuatwa.

Matokeo ya wanachama kuhama husababisha hasara kwa chama kinachoondokewa. Mosi, watu wapya ambao wangetamani kujiunga nacho hupatwa na wasiwasi, maana waliopo tu wanakimbia. Ile tafsiri ya siri ya mtungi aijuaye kata, husababisha waone wanaoondoka wanajua tamu na chungu kuliko wao wa nje.

Hasara ya pili ni kutetereka kwa imani na utulivu wa wanachama wanaokuwepo. Watajiuliza mbona wanakimbiwa? Huko kunakokimbilia kuna faida gani? Maswali hayo ndiyo husababisha mwanachama ajione pengine yupo sehemu ambayo si sahihi.

Hasara ya kisayansi

Pamoja na faida ambazo chama kinapata kwa kupokea wanachama wapya, vilevile hasara za kile kinachoondokewa, jicho la kisayansi linaweza kuichambua hasara ambazo chama cha siasa kinaweza kuzipata ingawa kitakuwa kinapokea watu wapya kwa wingi na kuonekana kinajijenga.

Jicho la kawaida linaweza kuiona CCM ya sasa kuwa ipo vizuri mno, lakini sayansi inaiona hasara ambayo si kila mtu huona. Hii inabeba maudhui ya aina ya wanachama ambao inawapokea na uwakilishi wao kwenye jamii. Ni kwa kuliona hilo ndiyo maana CCM inapaswa kuwa na tahadhari. Wimbi la wanachama ambao CCM inawapokea kwa sasa ni viongozi. Hivi karibuni ilimpokea Mbunge wa Kinondoni (CUF), Maulid Mtulia ambaye, kama wengine, alisema anahama upinzani na kujiunga na chama tawala ili kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli.

Mtulia amekuwa sehemu ya mkumbo wa kisiasa ambao umekuwa ukiwapeleka wapinzani wengi CCM katika siku za hivi karibuni. Kuanzia madiwani Arusha hadi viongozi wengine maarufu wanaosema wamevutwa na juhudi za Rais Magufuli.

Mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, viongozi waasisi wa ACT-Wazalendo, Profesa Kitila Mkumbo, Samson Mwigamba na Albert Msando, vilevile aliyekuwa Katibu ya Ngome ya Vijana (ACT-Wazalendo), Edna Sunga, walitimkia CCM kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli.

Ukiwatathmini hao wenye kuhama, unaweza kuuona ukweli kuwa ni tabaka la viongozi wa kisiasa ambao kwa kawaida huyatazama masilahi yao kivyao. Ndiyo maana Masha alihamia Chadema mwaka 2015 kumfuata aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa akiamini angeweza kushinda urais.

Hata hivi karibuni aliporejea CCM alisema sababu ni wapinzani kutokuwa na mipango ya kushika dola na akamwomba Rais kumtumia akitaka. Ukijumlisha na ile hoja ya wengi kuwa wanahamia CCM kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli, ndipo unaweza kuiona hasara ambayo CCM inaweza kuipata kutokana na wimbi la kupokea wapinzani.

Hasara ndani ya faida

Wanaohamia CCM wanawakilisha nini? Je, hicho ambacho wanakisema ndicho wananchi wote wanakiona? Mahitaji ya Watanzania kwa sasa ni yapi? Je, Watanzania wote wana furaha na namna uongozi wa Rais Magufuli unavyoshughulikia mambo?

Maswali hayo ndiyo ambayo CCM kama chama wanapaswa kujiuliza. Wasibweteke wala kuzidi kutumia nguvu nyingi katika kupokea wapinzani ili kuuonyesha umma kuwa Rais Magufuli anakubalika. Mwisho kabisa wenye kupiga kura ni mamilioni ya Watanzania ambao uchambuzi wao wa mambo si kama Masha, Kitila wala Mtulia.

CCM wanaweza kubweteka na kuwekeza nguvu nyingi kupokea wapinzani lakini chama kikawa kinachukiwa na mamilioni ya watu kwa sababu hakitimizi matarajio yao. Hivyo pamoja na kupokea wapinzani, chenyewe kama chama tawala kijikite kuisukuma Serikali kutimiza matarajio ya watu. Huo ndiyo mtaji mkuu.

Wimbi la wapinzani kuhama linaweza kuwafanya CCM waone upinzani unapepesuka au unaelekea kufa. Kwa hiyo wakazidisha siasa za urembo (cosmetic politics) badala ya kuwekeza kwenye matarajio ya watu. Hata sasa, CCM wajikite zaidi kwenye hali halisi ya maisha ya Watanzania. Wakizubaishwa na wapinzani wenye kuhama wanaweza kukutwa na fadhaa kama waliyokutana nayo chama cha Conservative cha Uingereza mwaka 1945 chini ya kiongozi aliyeonekana kupendwa sana, akiwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Winston Churchill. Conservative waliingia kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 1945 wakijiamini kupita kiasi. Churchill alionekana kukubalika mno, maana alipokuwa Waziri wa Jeshi la Maji, aliisaidia Uingereza kushinda Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia mwaka 1914-1918.

Matokeo hayo yakupe tafsiri kuwa wanasiasa waliona tofauti na wananchi. Wanasiasa waliangalia ushindi wa vita lakini wananchi waliangalia matarajio yao ya kimaisha. CCM ijifunze hili, wanaweza kuwekeza kwenye imani kwamba Rais Magufuli anapendwa sana lakini ikawa kinyume na maoni ya wananchi.

Hasara ya pili

CCM kama chama kinachoongoza Serikali kinahitaji fedha kuhudumia watu. Hatua ya madiwani na wabunge kuhama vyama vyao kwa namna moja au nyingine inaingilia matumizi ya fedha za umma, maana lazima kufanya uchaguzi kujaza nafasi.

Hivi karibuni mabilioni ya fedha yalitumika kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 43 ambazo zilikuwa wazi. Ndani ya hizo zimo zile ambazo madiwani wake waliachia ngazi kwa hoja ya kumuunga mkono Rais Magufuli na juhudi zake za kupambana na ufisadi.

Hivi sasa majimbo manne yapo wazi, Songea Mjini ambalo mbunge wake, Leonidas Gama (CCM) alifariki dunia. Longido la Onesmo Nangole (Chadema) aliyetenguliwa na Mahakama. Singida Kaskazini kwa Lazaro Nyalandu aliyejivua uachama CCM na kujiunga Chadema kisha Kinondoni kwa Mtulia.

Mabilioni ya fedha ambayo yatatumika kuandaa uchaguzi huo, yanapaswa kuwa chungu kwa CCM, maana yangeweza kutumika kufanikisha huduma kwa wananchi ambazo ndizo za msingi zaidi. Matokeo yake fedha nyingi zinatumika kugharamia uchaguzi.

Suala la Gama ni nguvu iliyo juu ya mamlaka za dunia, Mungu ndiye aliyeamua. Nangole ni matokeo ya kuwa na mfumo wa haki, kwamba ushindi haukuwa halali, hivyo Mahakama iliubatilisha, vilevile ya Nyalandu na Mtulia ni matunda ya demokrasia. Mtu hazuiwi kuhama, ila uchaguzi ni gharama kubwa.

Watu hawana umeme wa uhakika, maji hakuna, hospitalini dawa shida na wananchi hawana uwezo wa kumudu matibabu hata kwenye hospitali za Serikali, waliambiwa elimu bure lakini baadhi ya maeneo wazazi wameanza kuchangishwa fedha, halafu mabilioni yanatumika kuandaa uchaguzi. Hii ni hasara kwa Serikiali ya CCM.

Hasara ya tatu

CCM wanaingia kwenye mkumbo kuhusu hiki kinachoimbwa na kutamkwa kuwa “juhudi za Rais Magufuli”, wao wanajisahau kuwa ni taasisi ambayo ilikuwepo kabla ya Rais Magufuli na inapaswa kuendelea kuwepo hata baada yake.

CCM wanapaswa kutabasamu kupokea watu kwa sababu wanafuata chama na siyo mtu. Rais Magufuli ni binadamu. Ikitokea akisema anahama chama, kitabaki na mbeleko gani? Kama uchaguzi ujao asipogombea? CCM itabidi kujikusanya upya.

Chama chochote ambacho kinajikabidhi kwenye nguvu za mtu mmoja hasara yake ni kubwa mno. CCM hawapaswi kuunga mkono huu wimbo wa “juhudi za Rais Magufuli”, kama itawapendeza, wauimbe ule wimbo wa “CCM Mpya” ambao huimbwa na Katibu Itikadi na Uenezi CCM, Humphrey Polepole ambao una nafuu kwa chama.

Hivyo, kipindi hiki ambacho CCM wanavuna wanachama hasa viongozi kutoka upinzani, wazione faida katika chanya, wazifikirie hasara kwenye hasi. Wasibweteke na mkumbo wa mapenzi kwa Rais Magufuli, maana Conservative walipigwa mwereka na Churchill wao, wakumbuke mabilioni ya kurudia uchaguzi na hasara ya chama kutegemea mtu.