Yajue makundi matano ya watu hatari kazini

Muktasari:

  • Mfanyakazi anapojichukulia kama ‘jeshi la mtu mmoja’ linalojitosheleza kila idara, anajiweka kwenye hatari ya kufanya kazi kwenye mazingira magumu.

Tunaweza kukubaliana kwamba mafanikio anayoyapata mtu kazini kwake, mara nyingi yanategemea vile anavyoweza kutengeneza mazingira mazuri ya kupata ushirikiano wa karibu miongoni mwa wafanyakazi wenzake.

Mfanyakazi anapojichukulia kama ‘jeshi la mtu mmoja’ linalojitosheleza kila idara, anajiweka kwenye hatari ya kufanya kazi kwenye mazingira magumu.

Pamoja na juhudi unazoweza kuzifanya katika kuhakikisha unashirikiana vizuri na wenzako kazini, zipo nyakati ambazo watu wanaokuzunguka wanaweza kuwa kikwazo cha kupiga hatua kwenda mbele.

Mara nyingi watu hawa huwa na tabia zinazochukuliwa kama za kawaida lakini zenye nguvu kubwa ya kumharibia mtu si tu mtazamo wake kazini, lakini pia hata utendaji wake wa kazi.

Makala haya yanaangazia makundi matano ya watu unaohitaji kukaa nao mbali kwenye eneo la kazi kuepuka kuhatarisha ufanisi wako.

‘Mwanaharakati’

Huyu ni mfanyakazi anayetafuta sifa nyepesi kwa kujipa kazi ya ‘kutetea’ haki za watu. Sifa yake kubwa ni ujasiri alionao wa kuwakosoa viongozi wake hadharani.

Ingawa kuna mazingira ambayo namna pekee ya kufikisha ujumbe inaweza kuwa ni ‘kumlipua’ bosi hadharani, lakini inapokuwa ndiyo tabia ya mtu kusubiri mikusanyiko ya wafanyakazi ‘kulipua’ mambo, hapo lazima kunakuwa na tatizo.

Lakini pia, ‘mwanaharakati’ ana tabia ya kufanya kampeni za chinichini kupingana na wakubwa zake kazini. Kinachomsumbua ni kiu ya kutaka kutumia matatizo ya kampuni kujipatia umaarufu.

Mara nyingi watu wa namna hii hawafiki mbali kwa sababu mbili. Kwanza, hutumia uanaharakati kuficha upungufu wao binafsi wa kikazi. Ili kujiweka kwenye mazingira salama, hutumia kichaka cha kuwabomoa wengine.

Lakini pia hawafiki mbali kwa sababu faida ya kuonekana wajuaji kwa muda mfupi, huwagharimu baadaye. Hujenga chuki isiyo ya lazima na wakubwa wa kazi na hivyo hujinyonga kwa mikono yao wenyewe.

Wakati mwingine wanaofanya uanaharakati maofisini ni watu wenye historia za siasa za vyuoni.

Wanafikiri kuwasema wakubwa mbele za watu kunasaidia kurekebisha hali ya mambo.

Pamoja na umuhimu wa kudai haki, kuna haja ya kujifunza kufuata utaratibu unaokubalika.

Hata katika mazingira ambayo taratibu rasmi hazionekani kuleta majibu, tafuta suluhu kwa njia zinazoheshimu utu na heshima ya unaowadai haki.

Maneno mengi

Hawa ni watu ambao ukiwasikiliza kwa haraka haraka utaamini ‘wanajua’ kila kitu.

Watakueleza kwa undani mambo usiyoyategemea lakini kwa kawaida huwa hawafanyii kazi kile wanachokisema.

‘Maneno mengi’ wanapenda sana kuongea vikaoni hata kama hakuna ulazima wowote wa kuongea. Hupenda kuchangia kila hoja muhimu ni kushibisha njaa ya kutambulika wanayokuwanayo.

Hawa ndio watu wanaoweza kukufuata ofisini muda wa kazi na kukaa wakizungumza kitu kisicho na dharura yoyote.

Wakati mwingine unaweza kuwaonesha ishara kwamba unahitaji kuendelea na kazi lakini wasielewe. Muhimu kwako ni kuongea.

Mtu wa namna hii ni hatari kwa sababu kubwa mbili.

Kwanza, anaweza kukujengea taswira ya maisha asiyoyaishi ukajikta unaiga kisichokuwepo.

Pili, ukimpa nafasi kubwa anaweza kupoteza muda wako kusikiliza mambo yasiyoongeza tija kwenye kazi yako.

Mlalamikaji

Si kazi rahisi kumridhisha mtu mlalamishi. Huyu ni mtu anayejiona ana haki ya kupata zaidi ya kile anachostahili.

Mara nyingi si mtu anayejituma sana lakini anatamani kuona watu wengine wakijituma kwa faida yake.

Hawa huwa wepesi kuwalaumu wengine mambo yanapokwenda mrama. Ukiongea naye kwa dakika mbili, atakwambia nani amemwonea, nani hamtakii mema, nani ni kikwazo kwake. Hata siku moja hawezi kukwambia yeye amechangia nini kwenye matatizo aliyonayo.

Mtu mlalamishi mara nyingi huwa hana majibu ya kile anachokilalamikia. Ukimwuuliza tufanye nini kurekebisha hali anayoinung’unikia, ataishia kutoa majibu ya jumla, “mfumo”, “Serikali”, “Kampuni” bila kusema ni kwa namna gani.

Ukimpa nafasi mtu wa namna hii, utajiingiza kwenye tabia ya uvivu hatua kwa hatua.

Utaanza kutarajia zaidi kwa wengine kuliko kuwajibika na utataka ufanyiwe kuliko unayotimiza wajibu wako. Huwezi kufanikiwa kwa mtindo huu.

Anayependa kukosoa

Huyu anaona mapungufu kwa karibu kila kitu na kila mtu.

Ni vigumu kumridhisha kwa sababu hana tabia ya kuona jema la mtu na akalikubali.

Hawa si walipuaji, kazi yao kubwa ni kukatisha tamaa watu. Ukikaa nae dakika mbili ameshakwambia ubaya wa kampuni, taasisi au mtu anayeonekana kufanya kazi kwa bidii.

Bila shaka unawafahamu watu wanaoweza kukwambia kwa nini mshahara mnaolipwa na kampuni hautoshi na kwamba kuna mahali wanalipa zaidi lakini ajabu hawaachi kazi.

Tabia ya mtu kulalamika mara nyingi hutokana na kukata tamaa kunakofanya wasiishi na uchungu usioisha.

Hawa ni watu wanaofanya kazi wasizozipenda na hawana namna ya kutimiza ndoto zao.

‘Jembe sifa’

Huyu ni mtu anayechapa sana kazi kwa lengo la kuonekana kwa wakubwa kazini. Mara nyingi ni mtu anayeonekana kujiamini sana kwa nje lakini ndani yake ana wasiwasi na usalama wake.

Huwa anakuwa na tabia ya kujikomba kwa bosi, mara nyingine kwa kuwasema vibaya wafanyakazi wenzake.

Katika mazingira ambayo bosi mwenyewe naye hajiamini, watu wa namna hii wana nafasi kubwa ya kuaminika sana kazini.

Tabia ya kupenda sifa huenda sambamba na tabia ya kushindana na watu ambao wakati mwingine hata hawashindani naye.

Mtu mshindani haridhiki kufanya vizuri bali hutaka kufanya vizuri kuliko wengine wote.

Unapokuwa karibu na mtu wa namna hii atakuharibia kazi kwa sababu si tu atakunyong’onyeza bila sababu, lakini pia atakufanya ujisikie huwezi, huna thamani unayofikiri unayo na utajiona dhalili.

Ambatana na watu wanaojituma kufanya kazi kwa bidii, lakini wasio na muda wa kusubiri sifa ili wafanye kile wanachokifanya.

Tafuta watu wasio na sababu ya kujilinganisha na wewe.

Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Blogu: http://bwaya.blogspot.com , 0754870815