Yanga ilipopigwa 7-0 ndani ya siku 12

Muktasari:

  • Yanga ilikuwa na kazi ya kumalizia viporo vyake, mechi za Ligi Kuu baada ya kuwa na majukumu ya kimataifa, michuano ya klabu Afrika.

Achana na matokeo ya jana ya Ligi Kuu Bara kati ya Mtibwa Sugar na Yanga kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Yanga ilikuwa na kazi ya kumalizia viporo vyake, mechi za Ligi Kuu baada ya kuwa na majukumu ya kimataifa, michuano ya klabu Afrika.

Achana na hayo, kikubwa ni hili la Yanga kupoteza mechi tatu mfululizo, mbili za Ligi Kuu na moja ya klabu Afrika, ni kwamba kuna eneo Yanga mambo hayaendi sawasawa.

Yanga inapambana na Rayon Sports keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, ikiwa ni mchezo wake wa pili wa michuano hiyo ya klabu Afrika. Yanga ina kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha inashinda mchezo huo.

UDHAIFU

Benchi la ufundi la Yanga lina kazi ya kurekebisha udhaifu wa safu yake ya ulinzi kabla ya mchezo huo muhimu wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Safu ya ulinzi ya Yanga imejikuta ikiruhusu mabao saba katika mechi tatu ilizocheza ndani ya siku 12.

Mabao hayo saba ambayo Yanga imefungwa katika mechi dhidi ya Simba, USM Alger pamoja na Prisons yameifanya timu hiyo kuandika rekodi mbovu ya kufungwa idadi kubwa zaidi ya mabao ndani ya siku chache kuliko nyakati nyingine zote tangu klabu hiyo ilipoanzishwa.

Baada ya kukosa ubingwa wa Ligi Kuu ambao umechukuliwa na Simba, mashindano pekee yaliyobaki kwa Yanga ni Kombe la Shirikisho Afrika na wamepangwa kundi D sambamba na timu za Rayon Sports, Gor Mahia na USM Alger.

Yanga inayoshika mkia kwenye Kundi D ikiwa haina pointi, inatakiwa kuibuka na ushindi dhidi ya Rayon Sports kwenye mchezo wake unaofuata kwenye kundi hilo ili ifufue matumaini ya kufuzu hatua ya robo fainali.

Hata hivyo wakati Yanga wakipewa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi dhidi ya Rayon, hofu kubwa kwa wawakilishi hao wa Tanzania kwenye mashindano hayo ni safu yake ya ulinzi ambayo imeruhusu idadi hiyo ya mabao saba ndani ya kipindi kisichozidi wiki mbili.

NGOME KUKOSA UMAKINI

Nuksi kwa Yanga ilianzia Aprili 29 ambapo Yanga ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kipigo ambacho sio tu kiliwaongeza kasi wapinzani wao kwenye mbio za ubingwa bali pia kilihitimisha rekodi nzuri ambayo Yanga walikuwa nayo ya kufunga bao katika mechi tano mfululizo dhidi ya Simba kwenye Ligi Kuu.

Baada ya kupoteza dhidi ya Simba, safu ya ulinzi ya Yanga iliendelea kuonyesha udhaifu wake baada ya kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne katika mchezo wa ugenini wa Kombe la Shirikisho dhidi ya USM Alger uliochezwa Jumapili iliyopita ambapo ilifungwa mabao 4-0.

Siku nne baada ya mchezo dhidi ya USM Algers, safu ya ulinzi ya Yanga ilijikuta inaendeleza unyonge wake baada ya timu hiyo kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa juzi, Mei 10.

WASHAMBULIAJI YANGA

Wakati safu ya ulinzi ya Yanga ikionekana kushindwa kuhimili vishindo vya timu pinzani, ile ya ushambuliaji nayo imeweka rekodi mbovu ya kucheza mechi tatu mfululizo bila kufunga bao.

Kukosekana kwa wachezaji wake kama Ibrahim Ajib, Obrey Chirwa, Amiss Tambwe na Donald Ngoma ambao walisajili mahsusi kwa ajili ya kutupia, kumesababisha timu hiyo kuwategemea wachezaji wasiokuwa na uzoefu sana, Pius Buswita, Yusuf Mhilu ambao hawana uzoefu wa kutosha na mikikimikiki ya Ligi Kuu na mechi za kimataifa. Ushindi dhidi ya Rayon Sports utaiondoa Yanga mkiani mwa Kundi D na kuisogeza ama kileleni, kwenye nafasi ya pili au ya tatu kutegemea na matokeo ya mechi kati ya Gor Mahia na USM Alger ambayo nayo itachezwa siku hiyohiyo ya Julai 19 jijini Nairobi.

Baada ya mchezo dhidi ya Rayon ambao itachezwa keshokutwa, Yanga itasubiri hadi Julai 18 ambako itakuwa Kenya kukabiliana na Gor Mahia kabla ya kurudiana nao tena jijini siku 11 baadaye.

Ikimalizana na Gor Mahia, itaendelea kubakia jijini ambako itawakaribisha USM Alger kwenye mchezo utakaochezwa Agosti 19 na baada ya hapo itaenda Rwanda kufunga hesabu dhidi ya Rayon Sports.

KAULI YA NSAJIGWA

Kocha msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa anasema pamoja na kupoteza mechi zake hasa ya USM Alger bado wana nafasi ya kufanya vizuri kwa mechi za kimataifa.

“Yanga ilipoteza mechi zake ikiwemo kipigo kibaya cha mabao 4-0 ikiwemo ya USM Alger lakini nafasi kwetu bado ipo, tuna mechi nyingine tano za kufanya vizuri, kwa hiyo isiwe ishu sana ya kukata tamaa,” alisema alipozungumza na mtandao wa Goal.com

NYIKA AKUBALI

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Hussein Nyika alisema kuwa Yanga kutofanya vizuri katika kipindi hiki ni kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kupoteza ubingwa wa Ligi Kuu.

“Tunakubali mwaka huu kiujumla si mzuri kwetu, timu haifanyi vyema sana lakini tutajipanga vizuri zaidi msimu ujao kwani asiyekubali kushindwa si mshindani,” anasema Nyuika kwa kifupi.

KESSY ALONGA

Beki wa Yanga, Hassan Kessy alisema kilichoiangusha timu yao katika kipindi cha hivi karibuni ni kuwakosa wachezaji wake tegemeo wa kikosi cha kwanza kutokana na majeruhi na matatizo mengine. Ukiondoa mechi dhidi ya Simba, hizo zilizofuata hatukuwa na kikosi kilichokamilika na hata hao waliocheza bado wengine walikuwa na majeruhi.

Mbali na hilo lakini pia kuna suala la uchovu ambao umetokana na kucheza idadi kubwa ya mechi mfululizo. Naamini tutakaa sawa na tutafanyia kazi makosa yetu na mechi dhidi ya Rayon Sports tutafanya vizuri,” anasema Kessy aliyesajiliwa Yanga akitokea Simba.