Yasiyotakiwa kufanywa wakati wa kampeni za uchaguzi- (3)

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi huo, huu ni wakati wa kampeni za uchaguzi ambapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imepewa mamlaka kisheria kuratibu kampeni na kuvisimamia vyama vya siasa kuheshimu maadili ya uchaguzi.

Kutokana na uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani uliotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) katika Jimbo la Dimani na kata 20 za Tanzania Bara, ni vyema kutumia fursa hii kutoa elimu ya baadhi ya mambo ya msingi ya kuzingatia.

Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi huo, huu ni wakati wa kampeni za uchaguzi ambapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imepewa mamlaka kisheria kuratibu kampeni na kuvisimamia vyama vya siasa kuheshimu maadili ya uchaguzi.

Tume kwa kushauriana na vyama vya siasa na Serikali pia huandaa maadili ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani kwa kwa kuzingatia kifungu cha 124A cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343.

Maadili ya uchaguzi ni makubaliano ya pamoja baina ya vyama vya siasa, Serikali na Tume ya Taifa ya Uchaguzi yanayoeleza mambo yanayotakiwa kufanywa au kuzingatiwa na yasiyotakiwa kufanywa katika mchakato wa uchaguzi.

Lengo la maadili hayo ni kuweka uwanja sawa wa ushindani na kuwawezesha wananchi kupata nafasi ya kusikiliza sera za wagombea wa vyama vya siasa wakati wote wa kampeni za uchaguzi.

Vyama vya siasa na kila mgombea anapaswa kusaini maadili hayo katika fomu namba 10 na kutosaini maadili hayo chama au mgombea hataruhusiwa kushiriki katika uchaguzi.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, vyama vya vyote vya siasa vilivyoshiriki kwenye uchaguzi huo vilikubaliana maadili ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani wa mwaka huo na kusaini tamko la kukubali kufuata maadili hayo Julai 27, 2015.

Tamko hilo linasema hivi: “(Chini ya Kifungu cha 124 A cha Sheria ya Uchaguzi Na. 1 ya mwaka 1985 (sura ya 343). Sisi vyama vya siasa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa pamoja tumekubaliana kuwa na uchaguzi huru, wa haki, uwazi, na wa kuaminika.

Na kwamba amani, ustawi wa nchi, usalama wa raia, uhuru wa vyama vya siasa na utii wa sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi ndiyo msingi wa uchaguzi ulio huru, haki na wenye kuzingatia ushiriki wa makundi yote ya jamii katika uchaguzi.

Tunakubaliana kuwajibika kuyatekeleza maadili haya yanayotokana na kifungu cha 124A cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi ya mwaka 1985, (sura 343).

Tutafanya jitihada za wazi kuhakikisha maadili haya yanajulikana na kuheshimiwa na wagombea na wanachama wote wa Vyama vya Siasa.”

Kwa mujibu wa kifungu cha 2 (2) cha Maadili hayo, viongozi wa vyama vya siasa na wagombea wanatakiwa kuzingatia kuwa hawatakiwi kufanya fujo au kusababisha vurugu ya aina yoyote katika mkutano wa chama kingine wakati wa kampeni.

Hawatakiwi kutumia lugha ya matusi, kashfa, kejeli, udhalilishaji na vitisho au lugha inayochochea uvunjaji wa amani au kuashiria ubaguzi wa kijinsia, ulemavu au maumbile kwenye mikutano ya kampeni.

Silaha

Mtu yeyote haruhusiwi kuwa na au kubeba silaha yoyote ikiwa ni pamoja na silaha za jadi au zana yoyote inayoweza kumdhuru mtu katika mkutano wa kampeni au mkusanyiko wowote wa kisiasa.

Hairuhusiwi kuwa na au kubeba sanamu, kinyago au kitu chochote ambacho kinaonesha kudhalilisha, kukebehi au kufedhehesha chama kingine cha siasa au kiongozi wake au Serikali katika mkutano au mkusanyiko wowote wa kisiasa.

Viongozi wa vyama vya siasa, wagombea wao hawaruhusiwi kutumia vipaza sauti vya aina yoyote ile kwa shughuli za kisiasa vyakati za usiku kuanzia saa 2:00 usiku hadi saa 12:00 asubuhi.

Viongozi wa vyama vya siasa, wagombea wao hawaruhusiwi kuchafua, kubandua au kuharibu matangazo ya kampeni ya vyama vingine vya siasa na matangazo ya uchaguzi yanayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Vyama vya siasa visibandike mabango ya kampeni, matangazo au mchoro wowote kweye nyumba, majengo au vyombo vya usafiri vya watu binafsi au taasisi mbalimnali bila idhini ya wamiliki husika.

Kukosoana kati ya vyama na wagombea kunapofanyika ni lazima kujikita katika sera, programu na kazi zao walizofanya.Ukosoaji wa vyama vingine au wagombea wengine kwa kuhuma zisizothibitishwa ni lazima ziepukwe.

Vyama vya siasa au wagombea hawaruhusiwi kuomba kura kwa misingi ya kidini, ukabila, jinsia au rangi.

Vyama vyote vya siasa vikubali na kuheshimu uamuzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi yanayofanywa kwa mujibu wa Sheria za Uchaguzi. Hii ni pamoja na matokeo ya uchaguzi na wasimamizi wa uchaguzi.

Pale ambapo mtu hataridhika na matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi au wasimamizi wa uchaguzi, ana haki ya kupeleka malalamiko ya uchaguzi Mahakamani kwa mujibu wa sheria za uchaguzi.

Vyama vyote vya siasa, wagombea, wanachama au wafuasi hawaruhusiwi kutoa rushwa au shukrani ili kumshawishi mtu kusimama kama mgombea au kujitoa ugombea wake hawatakiwi kuwazuia watu kuhudhuria mikutano ya hadhara ya vyama vingine.

Kwa mujibu wa maadili haya, adhabu mbalimbali zinaweza kutolewa iwapo chama au mgombea atakiuka maadili hayo ikiwemo kusimamishwa kufanya kampeni au kulipa faini.

Mwandishi ni Ofisa Habari wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Kwa maswali na maoni tuma kwenda [email protected] au sms 0766496589.