MAONI, KIPIMO: Zari, Diamond wanatoa udaku, kampuni za simu zinazidi kutajirika

Muktasari:

Ni kama vile wao hawana maisha wameshamaliza sasa wameamua kuyaangalia ya wengine. Diamond na Zari wameitambua fursa hiyo na kila watazamaji wanapoishiwa cha kuzungumza huwapa kipya.

Waswahili wanasema wapiganapo tembo ziumiazo nyasi. Ukifuatilia kwenye mitandao watu wanavyovutana kuhusu uhusiano wa Diamond na Zari ni burudani ya kipekee kuwahi kutokea nchini kwetu.

Ni kama vile wao hawana maisha wameshamaliza sasa wameamua kuyaangalia ya wengine. Diamond na Zari wameitambua fursa hiyo na kila watazamaji wanapoishiwa cha kuzungumza huwapa kipya.

Baada ya kuona mtandao umekaukiwa habari, Diamond aliliamsha dude na mitandao ikaitikia. Wakati wakijadili hiki, anabandua anabandika kingine.

Lakini, mwisho wa siku anayenufaika hapa ni kampuni ya simu ambazo nadhani ukifanyika utafiti katika siku ambazo Diamond anakuwa amelianzisha dude, basi vifurushi vya intaneti huwa vinanunulika sana. Kwa mfano juzi baada ya kuposti picha akimdhihaki Zari, na baadaye mwanamke huyo kujibu mashambulizi.

Ilikuwa ukifungua grupu lolote la Whatsapp unakutana na screen shot ya posti hiyo. Huko Instagram, facebook na kwingine ndio usiseme. Binafsi naamini ndicho hasa Diamond alichokitaka kitokee kwa sababu ndiyo aina ya maisha aliyojichagulia.

Jiulize ni data kiasi gani ilitumika katika kipindi cha saa 24, bila shaka wahusika wanachekelea huko kwa kinachotokea.

Kwa akili ya kawaida isingewezekana kuamini posti ile ilikuwa ya kweli, kwani hata wakati anatuma alikuwa tayari amefika Afrika Kusini na huenda wakati anaandika walikuwa wapo pamoja. Dimaond ananufaika katika kiki hizi lakini mitandao ya simu inanufaika zaidi.

Siku hizi kuna msemo kuwa ni heri ukose damu lakini sio kifurushi cha data kwenye simu, ndio maana mtu badala ya kununua panadol aponye maumivu ya kichwa, ananunua bando aandike posti katika mtandao ili aombewe.

Ukweli wa uhusiano wa Zari na Diamond wanaujua wenyewe na hiki kinachoonekana nje ni sinema tu ambazo Wabongo wamekubali kuzifuatilia. Ingekuwa jamii inayojua kufanya yao na kuachana na watu, Diamond angekazana katika muziki.

Mashabiki wamekubali kucheza ngoma yake na sasa wanafilisika katika kununua vifurushi ili waperuzi udaku au warushiane matusi katika mitandao.

Ushabiki wa timu Kiba na Diamond unakufa taratibu, Diamond anazidi kuwa mbunifu na mitandao ya simu inachekelea kwa sababu pamoja na malalamiko ya hali ya uchumi kuwa ngumu, makampuni hayo yanaendelea kuchekelea.

Diamond endelea kumwaga ubuyu kampuni zinachekelea zikihesabu bukubuku za bando kutoka kwa Watanzania wasiotaka kupitwa na udaku.