SHERIA BIASHARA : Zifahamu haki, wajibu wa kila mwanahisa

Muktasari:

  • Wajibu wa mwanahisa unaanza hata kabla hajanunua hisa za kampuni aipendayo. Kwa wakati huu wajibu wake unakuwa ni kutokukurupuka kununua hisa. Atafute taarifa za kutosha kuhusiana na kampuni anayotaka kununua hisa hizo.

Ni muhimu kila mwanahisa kufahamu wajibu wake ili apate nguvu za kudai na kuzisimamia haki zake. Ili ufanikiwe, mwekezaji mwenye malengo ni lazima atambue haki na wajibu wake kwa mujibu wa sheria.

Wajibu wa mwanahisa unaanza hata kabla hajanunua hisa za kampuni aipendayo. Kwa wakati huu wajibu wake unakuwa ni kutokukurupuka kununua hisa. Atafute taarifa za kutosha kuhusiana na kampuni anayotaka kununua hisa hizo.

Anaweza kuhudhuria semina mbalimbali za uwekezaji kwenye hisa, kusoma vitabu na kutumia taarifa zilizopo kwenye magazeti, majarida, mitandao ya kijamii na tovuti.

Ukishanunua hisa za kampuni haina maana unapaswa kulala na kuamka kusubiri gawio au kupanda kwa bei ya hisa zako. Unao wajibu kuiwezesha kampuni hiyo kupata faida.

Sheria ya Kampuni ya mwaka 2002 inabainisha wajibu na haki anazopaswa kuzifahamu kila mwanahisa.

Wajibu ni huo ni pamoja na kuendelea kufanya utafiti na kupata taarifa za kutosha za kampuni uliyowekeza. Hii humsaidia kuifahamu vyema kampuni hiyo na kuwa na uhakika wa uwekezaji wake.

Kuhudhuria vikao vya wanahisa ambavyo hufanyika mara mbili au zaidi kwa mwaka. Kutunza cheti na taarifa nyingine muhimu za umiliki wa hisa zake pia.

Mwanahisa anapaswa kulinda maslahi ya kampuni aliyowekeza pamoja na kufuatilia utendaji wa bodi ya wakurugenzi na viongozi wake. Upo pia wajibu wa kutotumia vibaya taarifa za ndani za kampuni kwa maslahi binafsi yatakayoiingiza kampuni kwenye matatizo ya kibiashara.

Zipo kampuni zinazotoa mafunzo kwa wanahisa wake ikiwamo namna ya kutambua fursa za uuzaji na ununuzi wa hisa, mirathi na mambo mengineyo yenye faida kwa wanahisa.

Ni muhimu kuhudhuria mafunzo hayo kupanua ufahamu wa wanahisa.

Kutimiza wajibu kunakupa uhalali na nguvu za kutosha kudai haki zako za kupewa nakala ya cheti cha umiliki wa hisa ulizonunua, taarifa za utendaji wa kampuni na ripoti ya mapato, matumizi, rasilimali na madeni ya kampuni.

Nyingine ni kushiriki kupitisha uamuzi wa kuboresha utendaji wa kampuni kama vile kuwawajibisha au kuwaondoa madarakani wakurugenzi wa bodi ya kampuni au uongozi wa kampuni.

Ni haki yako kupata gawio la faida iliyopatikana kila mwaka endapo bodi itaridhia. Kuendelea

Hata hivyo inashauriwa, ili kupata faida unapotaka kuuza hisa zako, ni vyema ukafanya hivyo bei inapopanda. Pia, unayo haki ya kutumia gawio lako vile upendavyo.

Unaweza ukaamua kutoendelea kuwa mwanahisa wa kampuni husika kwa kuuza hisa zako zote kupitia mawakala wa soko kwa bei na gharama za wakati huo.

Hii inaweza kuwa kwa lengo la kupata fedha na kuzitumia maeneo mengine au utendaji mbovu wa kampuni husika.

Mwanahisa na mwekezaji wa kampuni husika unayo mamlaka makubwa yanayotokana na umiliki wa hisa zako. Japokuwa katika baadhi ya kampuni anayemiliki hisa nyingi zaidi ndiye mwenye mamlaka makubwa zaidi kufanya uamuzi, hiyo haiondoi haki yako ya msingi kama mwanahisa.

Tambua wajibu wako na uutimize, kisha utambue kwa makini zaidi haki zako na uzisimamie. Wajibu wako ni haki kwa kampuni uliyowekeza na haki zako ni wajibu kwa kampuni.

Ni wajibu mwanahisa kutoruhusu mgongano wala migogoro ya aina yoyote. Mwanahisa makini, mwenye maono ya kufanikiwa zaidi na mwenye uchungu na fedha zake anatambua wajibu na haki zake.