UCHAMBUZI: Zifanyike tafiti halisi za hali ya uchumi nchini

Muktasari:

Hoteli za Mount Meru na Snow Crest sasa zinauzwa wakati biashara hiyo ikielezwa kwamba siyo nzuri. Shirika la ndege la Fastjet limetangaza azma ya kupunguza wafanyakazi wake ili kukabiliana na gharama za uendeshaji.

Kumekuwa na viashiria vingi vya kuyumba kwa uchumi hapa nchini. Watu mbalimbali wamekuwa wakitafsiri hali hiyo wakihusisha na utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano tangu ilipoingia madarakani, mwishoni mwa mwaka jana.

Hoteli za Mount Meru na Snow Crest sasa zinauzwa wakati biashara hiyo ikielezwa kwamba siyo nzuri. Shirika la ndege la Fastjet limetangaza azma ya kupunguza wafanyakazi wake ili kukabiliana na gharama za uendeshaji.

Kadhalika, wananchi wanalalamika kwamba hali ya maisha kwa sasa siyo nzuri. Fedha haipatikani mitaani, watu wanakosa kazi na wengine wanashindwa kuendesha biashara zao kwa kukosa wateja wa kutosha.

Mambo hayo yanaelezwa kusukumwa zaidi na mfumo mpya wa Serikali wa kubana matumizi. Hata hivyo, Serikali inasema fedha zilizokuwa zinaibwa sasa hazipo, kila mtu analazimika kufanya kazi ili apate fedha.

Nadharia hizo siyo za kupuuzwa. Zinahitajika tafiti mbalimbali kutafuta kiini na kisha kupata ufumbuzi wa kuporomoka kwa uchumi. Tukiendelea kuleta siasa kwenye suala la uchumi, basi tukubali kuwa Taifa maskini siku zote.

Ripoti ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ya mwaka jana ilieleza kwamba uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi ya asilimia saba. Wachumi walipongeza ukuaji huo, lakini baadhi ya wakosoaji walisema uchumi huo hauakisi maisha halisi ya Watanzania.

Hivi karibuni, tuliambiwa kwamba mizigo imepungua bandarini lakini mapato yameongezeka. Inawezekana ni kweli yameongezeka, lakini si jambo la kujivunia kama mizigo iliyokuwa inahudumiwa imepungua.

Huenda Bandari ya Dar es Salaam ingeweza kuhudumia mizigo mingi zaidi na kuiwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukusanya fedha nyingi zaidi. Kuishia kujivunia kuongezeka kwa mapato wakati watumiaji wa bandari wakipungua ni kujidanganya.

Natambua jitihada za uongozi wa Bandari ya Dar es Salaam kwenda kuzungumza na wafanyabiashara 100 ili wapitishe mizigo yao hapo. Hata hivyo, suala hili linahitaji kufanyiwa utafiti wa kina ili kupata suluhisho la kudumu.

Bandari ya Dar es Salaam ikiwa chanzo kikubwa cha mapato, inahitaji kujengewa mazingira ya kuvutia ili kuwashawishi wafanyabiashara wengi. Mfumo wa soko huria unataka kila upande unaohusika katika biashara unufaike na siyo upande mmoja tu.

Kuna haja ya kuwasikiliza wafanyabiashara ili wazungumzie kero wanazozipata katika Bandari ya Dar es Salaam na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ichukue hatua kutatua changamoto ambazo zitakuwa zimebainishwa na wafanyabiashara.

Siyo jambo jema kupuuza madai yao kwa sababu tukiacha wakaondoka wote, Serikali itakosa mapato ya kuiwezesha kutimiza malengo yake ya kujenga Taifa lenye uchumi wa kati kupitia viwanda.

Jitihada za Rais John Magufuli kujenga viwanda zinahitaji nguvu kubwa ya maendeleo ya sekta nyingine. Sekta ya usafirishaji ikitengenezwa vizuri itaisaidia Serikali kukusanya mapato ya kutosha kugharamia ujenzi wa viwanda.

Hata hivyo, Serikali haiwezi kupata jawabu la hali ya uchumi wa Taifa kama hakutafanyika utafiti wa kina na kubaini vyanzo halisi vya hali ngumu ya maisha ya Watanzania na baadhi ya kampuni kufungwa.

Nchi zilizoendelea zinatengeneza mipango yake baada ya kufanya tafiti za hali ya uchumi kwa wakati husika na kutabiri hali ya uchumi kwa miaka mitano itakayofuata.

Peter Elias ni mwandishi wa gazeti hili – 0763891422. [email protected]