Zijue Faida za kuingia ubia kwenye biashara mbalimbali

Muktasari:

  • Wote walikuwa wakimiliki maduka ya kuuza nguo yaliyokuwa na gharama kubwa za uendeshaji.

Mwaka jana haukuwa mzuri kibiashara kwa marafiki wa karibu; Mushi na Brian ambao walikuwa wakifanya biashara zinazofanana katika maeneno tofauti mjini Moshi.

Wote walikuwa wakimiliki maduka ya kuuza nguo yaliyokuwa na gharama kubwa za uendeshaji.

Gharama za uendeshaji zilikuwa zikiongezeka na faida ilikuwa ikipungua kila mwezi. Marafiki hawa walishauriana na kuamua kufunga biashara zao.

Je unadhani hilo lilikuwa suluhisho?

Jibu ni rahisi, hilo halikuwa suluhishi, bali moja ya njia ambayo Mushi na Brian wangeitumia ni kuunganisha mitaji yao ili biashara iendelee.

kuna methali ya Kiswahili isemayo kidole kimoja hakivunji chawa.

Kuanzisha na kufanya biashara kimekuwa siyo kitu rahisi kwa watu wengi kutokana na changamoto nyingi ikiwamo ya ushindani na gharama za uanzishaji na uendeshaji.

Watu wengi ukiwauliza kwa nini hawajaamua kuanzisha biashara ziwasaidie kutatua tatizo la ajira au kuwaongezea kipato kingine, sababu kubwa wanasema ni mtaji mdogo au kukosa mtaji wa biashara.

Ubia ni moja ya njia nzuri za kukabiliana na changamoto kama hizi.

Ubia ni mapatano ya kibiashara yanayohusisha zaidi ya mtu mmoja kwa kuchanga mtaji, rasilimali na nguvukazi kisha kugawana faida au hasara ya biashara hiyo.

Wabia huchanga mtaji au rasilimali kwa viwango sawa au vinavotofautiana na faida hugawanywa kulingana na mchango wa kila mbia.

Urasimu mdogo katika uanzishwaji wake

Moja ya mambo yanayokatisha tamaa katika kuanzisha biashara ni urasimu hasa katika mchakato wa usajiri.

Ukilinganisha na uanzishwaji wa kampuni, ubia hauna mahitaji mengi ya kisheria katika uanzishwaji wake. Hii inatoa fursa kwa watu wa kawaida kumiliki biashara kwa pamoja.

Kugawana gharama za uanzishaji na uendeshaji wa biashara.

Methali ya umoja ni nguvu inaelezea vizuri faida ya ubia katika biashara.

Gharama za kuanzisha biashara mara nyingi siyo rahisi kuzimudu kwa watu wengi, lakini ubia unatoa fursa kwa kila mbia kuchangia mtaji kutokana na makubaliano na kufanya upatikanaji wa rasilimali kuwa rahisi zaidi. Uendeshaji wa biashara pia una gharama zake nyingi kama kodi na ushuru, matangazo, malipo kwa wafanyakazi na mengineyo.

Kugawana kwa gharama hizi kwa wabia kunapunguza mzigo mkubwa wa gharama ambao mtu mmoja angeubeba peke yake.

Mchango wa mawazo na ujuzi kutoka kwa watu tofauti

Uwapo wa mtu zaidi ya mmoja kwenye biashara kunaongeza uwezekano wa kupata mawazo ya kibishara yaliyobora zaidi.

Kwa kuzingatia ukweli kwamba binadamu tumetofautiana na tumezidiana maarifa, uzoefu, uwezo wa kufikiria, ubunifu na mambo mengine mengi, wabia katika biashara wanaongeza uwezekano wa kufanya maamuzi bora na yenye tija kwenye mustakabali wa biashara zao.

Mgawanyo wa athari ya kushindwa kwa biashara

Biashara yoyote ile ina vihatarishi vyake. Si biashara zote ambazo hufanikiwa hivyo kunauwezekano wa kushindwa kuendelea. Endapo hili litatokea madhara au athari zake hugawanywa kwa wabia pia hivyo maumivu yake sio makubwa kama biashara hiyo ingefanywa na mtu mmoja.

Ulipaji wa kodi hautozwi kwenye biashara yenyewe

Katika ubia kodi hulipwa kama ilivo kawaida kwa Mamlaka ya Mapato (TRA) lakini utaratibu wa malipo ni wa tofauti ukilinganisha na ule unaofanywa na makampuni.

Wakati kampuni linalipa kodi kutokana na faida inayopata, kwenye ubia kila mbia hulipa kodi kutokana na gawiwo alilolipata kutokana na faida iliyopatikana kwenye ubia huo.

Hii inamaanisha kuwa kiwango cha kodi kitatofautina kwa kila mbia kutokana na faida aliyoipata ambayo nayo hutokana na kiwango cha mchango (hisa) katika ubia huo.

Urahisi katika utunzaji wa kumbukumbu za kifedha

Mahitaji katika uandishi na utunzaji wa kumbukumbu za kifedha unaohitajika katika makampuni ni mkubwa zaidi kwenye makampuni.

Katika ubia mchakazo hauhitaji urasimu mrefu na mgumu kwani mahesabu yanaweza kuandaliwa na wabia kwa mfumo ulio rahisi kuumudu.

Pamoja na ukweli kwamba ubia unafaida zake lakini pia una changamoto kadhaa zinakabili aina hii ya biashara.

Mbia anaweza kushtakiwa kama mtu binafsi kutokana na anachofanya hata kama kinahusiana na biashara.

Hii inamaanisha mbia mmoja anaweza kushitakiwa mahakamani na wengine kuachwa kwa sababu ya tuhma zozote zile.

Endapo biashara itafirisika au kuwa na madeni gharama zinaweza muathiri mbia moja kwa moja kwa kutakiwa kuzilipa gharama hizo.

Hii inaweza kupelekea hata kupigwa mnada kwa mali za mbia au wabia kulingana na kiwango cha umiliki katika biashara yao.

Biashara ya aina hii pia inaweza kuyumba na kumuathiri mbia moja kwa moja endapo mmoja wa wabia ataamua kujitoa au kupoteza maisha.

Angalizo

Mara nyingi mfumo huu kibiashara ili uweze kufanikiwa unahitaji watu wanaofahamiana na kuaminiana kwani kosa la mbia mmoja linaweza kuathiri biashara na kumuathiri mbia mwingine moja kwa moja.

Ubia unahitaji watu wenye moyo wa kujitoa na kuipenda biashara yao ili kuweza kuweka jitihada za kutosha kwenye kuifanya istawi na kuzidi kuendelea.

Uwazi katika kufanya maamuzi pia ni moja ya vitu muhimu katika mafanikio ya ubia kwani endapo mmoja ya wabia atahisi kuwa anatengwa au hashirikishwi kwenye maamuzi inaweza kumvunja moyo na kupunguza umoja na ushirikiano vitu ambavyo ni muhimu sana katika kufanikisha biashara ya aina hii.

Ikumbukwe kuwa aina hii ya biashara inahiataji usimamizi wa karibu sana hivyo wabia wanatakiwa wawe na kiwango cha juu cha nidhamu ya kibiashara na kuwa tayari kufanya ufuatiliaji wa karibu.

Kelvin Mwita ni Mhadhiri Chuo Kikuu Mzumbe, 0659081838, [email protected], www.kelvinmwita.com