Friday, November 3, 2017

Zijue fursa za kujiongezea kipato kupitia mitandao

 

By Kelvin Mwita, Mwananchi

Wakati malalamiko ya changamoto zinazotokana na matumizi ya mitandao ya kijamii zikizidi kuongezeka hasa katika mmomonyoko wa maadili, bado kuna fursa nyingi katika mitandao hii ambazo hazitumiki ipasavyo.

Jamii hasa vijana wamekuwa wakitumia vibaya teknolojia hii kiasi cha Serikali na taasisi mbali mbali kutengeneza utaratibu na sheria za kudhibiti matumizi yake ili yasilete madhara makubwa kwa watumiaji au watu wengine wanaoweza kuathirika na matumizi ya watumiaji hao.

Hebu tuanze na maswali machache kwa wewe unaye soma makala haya; upo kwenye mitandao mingapi ya kijamii? Katika hiyo mitandao upo kwenye makundi (ma-group) mangapi? Je, yana msaada gani kwako?

Hivi karibuni nilijikuta kwenye kundi la mtandao wa kijamii la WhatsApp kwa kuunganishwa na mtu mwingine bila ridhaa yangu.

Nikamuuliza maswali machache tu; kwa nini umeniweka kwenye kundi hili na malengo ya kikundi ni nini?

Alinipa jibu moja tu; ‘just for fun’ akimaanisha ni la kujifurahisha. Makundi ya aina hii yako mengi kwenye mitandao ya kijamii.

Yanapoteza muda, yanaingiza gharama, yanasababisha uvivu na mara nyingi huchangia mmomonyoko wa maadili kwa sababu ya taarifa, picha na video zinazotumwa kwenye ma-group hayo.

Ni fursa zipi zinazoweza kutumika katika mitandao ya kijamii na ikasaidia kutengeneza ajira na kuongeza kipato?

Kutengeneza vikundi vya uzalishaji mali

Kukua kwa tatizo la ajira kuna hitaji mbinu mbadala za kukabiliana nazo ili kujikwamua kiuchumi.

Utengenezaji wa vikundi ni moja ya njia rahisi za kukabiliana na tatizo hilo. Changamoto kubwa ya kuunda vikundi hivi ni umbali wa kijiografia kati ya mtu na mtu lakini pia, ni ufinyu wa muda wa kukutana mara kwa mara kwa ajili ya mipango na mikakati ya vikundi.

Mitandao ya kijamii inatoa fursa ya kuunda vikundi ndani ya mitandao hiyo kusudi kuwawezesha watumiaji kujadiliana popote walipo.

INAENDELEA UK 24

Kimaro ni Mwenyekiti wa kikundi kinachoitwa Afrotan. Kikundi hiki kilianzishwa kwa lengo la kufanya shughuli za kilimo na ufugaji.

Kwa sababu ya changamoto ya muda na umbali, aliwashirikisha baadhi ya marafiki na kuamua kutengeneza kundi kwenye mtandao wa WhatsApp ambalo hutumika kwa ajili ya majadiliano juu ya mustakabali wa kikundi hicho.

Wakati kikundi kinaanza, wanachama walikubalina kuwe na gharama za kiingilio na michango ya mwezi kwa kuanza na wanachama sita, mwaka 2016 na sasa lina wanachama 15.

Kikundi kilianza na mradi wa kulima vitungu na kufuga sungura kwa kuajiri watu na wanachama kushiriki pale wanapopata muda.

Baadaye, wanachama walikubalina kutumia mtaji uliopo kwa ajili ya kukopeshana kwa riba ndogo ili kukuza mfuko na kuwawezesha wanachama kufanya shughuli mbalimbali ikiwamo ya ujasiriamali.

Mpaka sasa, kikundi kimeshatoa mikopo ya zaidi ya Sh14 milioni kwa wanachama wake.

Hii imewezeshwa kwa kiasi kikubwa na uwapo wa kundi la WhatsApp kwani wanachama wanaishi mikoa tofauti.

Kitu kama hiki kinaweza kufanywa na watu wengi na pengine kubadili matumizi ya makundi yaliyopo kwenye mitandao ya kijamii ili kuleta tija zaidi.

Hebu jiulize tena, makundi yako yanakusaidia nini?

Biashara na masoko

Kwa kuzingatia watumiaji wa mitandao ya kijamii ni wengi, hali hii inatoa fursa kwa watu wanaoamua kutangaza biashara zao. Watu hutumia akaunti zao za mitandao ya kijamii kutoa taarifa juu ya bidhaa na huduma wanazotoa kusudi kuwajulisha wateja wao kama njia ya kutafuta masoko ya biashara zao.

Urahisi na gharama ndogo ya kutangaza biashara hufanya matumizi ya mitandao ya kijamii kuwa ya ufanisi kwa ni huwafikia watu wengi ambao wanauwezo wa kuwasiliana nawe moja kwa moja kupitia mitandao hiyo ya kijamii.

Utafutaji wa masoko hufanyika pia kwenye makundi yanayotengenezwa kwenye mitandao hiyo.

Elimu ya ujasiriamali

Mitandao ya kijamii inatoa fursa ya kutoa elimu na taarifa zinazoweza kusaidia katika ujasiriamali na kutengeneza ajira kwa wengine.

Elimu ya ujasiriamali imekuwa ikifanyika kwenye mitandao ya kijamii kwa baadhi ya watu walioiona fursa hii.

Watu wenye maarifa au uzoefu wa biashara, huwafundisha wengine kupitia kurasa zao na makundi yanayoundwa kwenye mitandao ya kijamii.

Shughuli hii hufanyika bure na wakati mwingine kwa kiasi fulani cha ada. Sasa kama una ujuzi na unaweza kutumia ujuzi wako kwa kufundisha wengine, usitafute kisingizio kuwa hauna fedha za kukodisha darasa au ukumbi, waweza toa elimu kupitia mitandao ya kijamii.

Pia, mtandao kama wa YouTube, una mamilioni ya video zinazofundisha mambo mengi sana ikiwamo biashara na ujasirimali. Video hizi zinaweza kukupa maarifa zaidi na kukuhamasisha kuanza au kukuza biashara yako na hakuna malipo unayoyafanya kwa kuangalia.

Fursa za ajira

Kuwa na elimu ya matumizi ya mitandao ya kijamii, kunatoa fursa kwa vijana wengi. Wapo wanaofahamu nguvu ya mitandao ya kijamii katika kutafuta masoko, lakini hawana ujuzi wa kutumia mitandao hiyo. Hawa hugeuka fursa kwa wale wenye ujuzi wa kutosha, kwani huwalipa wenye ujuzi ili wawatengenezee na kuzisimamia kurasa za mitandao ya kijamii.

Shughuli hii mara nyingi haifanywi bure, bali kwa malipo kutokana na makubaliano yanayofikiwa.

Kama haujui, taasisi mbalimbali na watu wengi maarufu huwa hawana muda wa kusimamia kurasa zao za mitandao hiyo ya kijamii, lakini huwa na wasaidizi katika shughuli hiyo.

Pamoja na hilo, zipo kurasa za mitandao ya kijamii zenye wafuasi wengi kiasi cha watu binafsi na kampuni kuwalipa wenye kurasa hizo ili wawatangazie biashara zao.

Hii ni fursa pia ya kujipatia kipato kwa sababu shughuli hii haifanywi bure pia.

Angalizo

Mitandao ya kijamii pia imewacha madhara mengi katika uhusiano wa kibiashara, kwani wapo wanaotapeliwa na kupoteza fedha zao.

Hivyo, ni vyema kuwa muangalifu unapo amua kuanzisha uhusiano wowote wa kibiashara kupitia mitandao ya kijamii. Kama unataka kuanzisha kikundi cha biashara kwenye mitandao ya kijamii, zingatia kuwa na wanachama mnaofahamiana na kuaminiana pia.

Kelvin Mwita ni Mhadhiri Chuo Kikuu Mzumbe, 0659 081838, kelvnmwita@gmail.com, www.kelvinmwita.com

-->