Zijue kanuni muhimu za ufugaji wa kuku

Wafugaji  wengi nchini hujihusisha na ufugaji wa kuku kwa lengo la kujipatia chakula na kipato.

Kipato hicho hutokana na mauzo ya mazao yatokanayo na ufugaji wa kuku kama vile mayai, nyama na mbolea

Pamoja na faida hizo, lakini wafugaji wengi wamekuwa hawafuati kanuni na mifumo sahihi kwa ajili ya ufugaji wa kuku.

Mifumo ya ufugaji wa kuku?

Kuna aina tofauiti za mifumo ya ufugaji wa kuku. Kwa  Tanzania, inayotumika ni  mfumo huria, nusu huria na shadidi. Huria ni kuwaacha kuku nje wakijitafutia chakula na kurudi bandani jioni. Nusu huria ni kuwafuga bandani na kisha kuwatoa nje baadhi ya nyakati, wakati shadidi ni kumfuga kuku ndani ya banda.

Kanuni zinazoongoza ufugaji wa kuku

Ufugaji wa kuku utakuwa endelevu na wenye tija kwa mfugaji endapo

atafuata kanuni maalumu kama  kuwa na banda bora kwa ajili ya

ufugaji wa kuku, uchaguzi wa mbegu bora ya kuku, matunzo  ikiwa ni pamoja na kulisha kuku kulingana na hatua mbalimbali za ukuaji.

Kanuni nyingine ni udhibiti wa magonjwa ya kuku kwa wakati na kutunza kumbukumbu kwa kila hatua.

Banda la kuku na sifa zake

Kuku wanahitaji kuwa na banda bora. Hii itasaidia wasipate madhara ya

aina yoyote kama vile kushambuliwa na wanyama au magonjwa ya kuambukiza.

Sifa za banda la kuku ni pamoja na kuwa  imara, lenye uwezo wa kuwahifadhi kuku dhidi ya hali ya hewa hatarishi. Banda liwe na mwanga, hewa na nafasi ya kutosha inayoruhusu usafi kufanyika kwa urahisi. Jenga banda sehemu yenye mwinuko isiyotuamisha maji. Banda liwe sehemu isiyo na upepo mkali na iwe mbali kidogo na nyumba ya kuishi. Hakikisha banda lina vichanja kwa ajili ya kuku kupumzika na kulala. Banda liwe na sehemu ya kuwekea chakula, maji, kutagia, kuatamia na sehemu ya kulelea vifaranga. Hakikisha banda lina nafasi ya kutosha kulingana na idadi ya kuku. Weka vyombo vya chakula na maji kwenye banda kwa mpangilio. Ni muhimu kuhakikisha kuwa kwenye mazingira ya joto, banda lina ukuta mfupi na sehemu kubwa iwe wazi yenye wavu. Kwenye mazingira ya baridi, banda liwe na ukuta mrefu unaokaribia paa.

Vifaa kwa ujenzi wa banda bora

Vifaa vya ujenzi wa banda la kuku vinatofautiana kulingana na maeneo

na uwezo wa mfugaji. Ni muhimu kujenga banda kwa kuzingatia gharama na upatikanaji wa vifaa katika eneo husika. Vifaa vinavyohitajika kwa kila banda  ni sakafu,   kuta, paa na uzio

Ukubwa wa banda

Ukubwa wa banda utategemea idadi ya kuku na aina ya kundi la kuku.

Kuku wanahitaji nafasi tofauti kutegemeana na umri, aina na njia ya ufugaji. Eneo la mita moja ya mraba linatosha kwa vifaranga 16 wa umri wa wiki moja hadi nne, hivyo banda lenye mita za mraba 16 linaweza kulea vifaranga 320 hadi wiki ya nne. Baada ya wiki ya nne eneo hili liongezwe kutegemea aina ya kuku na

njia inayotumika katika ufugaji

Idadi ya kuku kwa mita moja ya mraba

Kuku wa umri wa siku moja hadi wiki nne wakiwa wa mayai au wanyama wanapaswa kuwa 18. Kuanzia wiki ya tano hadi ya nane punguza wabaki kuku tisa.

Wiki ya tisa hadi 20 kwa kuku wa mayai wanapaswa kuwa sita kwa kila eneo la mita moja ya mraba. Kuanzia wiki ya 21 na kuendelea wanapaswa kuwa watatu hadi wanne.

Makala haya yameandaliwa na matandao wa www.mkulimambunifu. mkulimambunifu.org