Zijue mashine za kutotolesha vifaranga

Muktasari:

Kwa bahati mbaya nalazimika kutolijadili hilo wiki hii na kulihamishia wiki ijayo kutokana na maombi ya idadi kubwa ya wasomaji wa safu hii.

Wiki iliyopita niliahidi kuchambua kwa uchache mtaji ambao mtu unaweza kuanza nao katika ufugaji wa biashara wa kuku wa kisasa.

Kwa bahati mbaya nalazimika kutolijadili hilo wiki hii na kulihamishia wiki ijayo kutokana na maombi ya idadi kubwa ya wasomaji wa safu hii.

Wasomaji wengi wameonyesha kuvutiwa na njia ya utotoleshaji wa mayai unaofanywa na mashine maalumu za kutotolesha mayai maarufu kwa jina la la viatamishi (incubators).

Eneo hilo limezungumzwa na wasomaji wengi ambao waliuliza maswali mbalimbali.

Wengi walikuwa na kiu ya kutaka kujua gharama, faida, hasara na upatikanaji wa mashine hizi.

Kwa kuthamini mchango wa wasomaji wa safu hii, nimelazimika kuitumia wiki hii kujibu maswali yote yaliyoelekezwa kwangu mashine hii.

 

Viatamishi ni nini?

Hizi ni mashine maalumu zinazotumika kurahisisha utotoleshaji wa mayai ya aina zote hasa ya kuku wa asili na wale wa kisasa. Pia, inaweza kutumika kwa mayai ya kwale, bata na kanga.

Mashine hizi hutofautiana ukubwa, lakini pamoja na tofauti hiyo, bado kila moja ina uwezo wa kutumia muda mfupi kutotolesha mayai, tofauti na muda anaoutumia kuku kuatamia hadi kupata vifaranga.

 

Aina za viatamishi

Kwa jumla, mashine hizi zote zina kazi moja tu ambayo ni utotoleshaji, japo zimetofautishwa kwa mifumo yake ya kiuendeshaji.

Mfumo wa kwanza unazijumuisha mashine zote zinazototolesha mayai kwa kujiendesha zenyewe (automatic).

Mfumo wa pili unaziunganisha mashine zote zinazofanya kazi kwa kuendeshwa kwa msaada wa kibinadamu.

Mashine zinazojiendesha zenyewe zinatumika sana kibiashara kwa sababu zinarahisisha kazi tofauti na ilivyo kwa zile zinazoendeshwa na binadamu.

Mashine hizi zina faida kubwa kwani si rahisi kuharibu mayai kutokana na kuwa na mashine ndani ambayo kazi yake ni kusaidia kutawanya joto kwenye mayai.

Uzuri wake ni kwamba hata joto likizidi uwezekano wa kuharibu mayai haupo kwa sababu feni inasaidia kupunguza joto ndani ya mashine.

Kundi la pili linajumuisha mashine zinazofanya kazi zake kwa kutumia uwapo wa mtu muda wote.

Aina hii ya mashine hutumia upepo wa kawaida kuendesha zoezi la utotoleshaji, haina feni maalum la kupoza joto.

Hii ina maana lazima mtu awe karibu na mashine wakati wote wa utotoleshaji ili aweze kufanikisha mchakato wote.

 

Sifa za viatamishi

Kama nilivyotangulia kusema hapo awali kuwa mashine hizihazitofautiani sana, ukiachilia mbali ukubwa na mfumo wa uendeshaji.

Zipo mashine zenye uwezo wa kutotolesha mayai mengi zaidi kwa pamoja na nyingine kulingana na udogo wake zinalazimika kutotolesha mayai machache kwa muda mfupi pia.

Kwa kawaida mashine nyingi za utotoleshaji hutumia umeme kidogo wa unaokadiriwa kuwa wa Voltage:110V- 220V.

Ukifanikiwa kupata mashine bora, unajijengea uhakika wa kutotolesha asilimia 95 ya mayai yote.

 

Unazijuaje mashine bora?

Si jambo rahisi kuzijua mashine bora, lakini unaweza kutazama baadhi ya vitu muhimu kama vile tochi maalumu yenye uwezo wa kukagua uhai wa mayai yaliyomo ndani ya mashine.

Zipo mashine zenye uwezo wa kila trei ya mayai kuwa na sehemu ya kuangulia vifaranga, kuangalia mfumo maalumu ‘full Automatic’ unaoweza kugeuza mayai, kudhibiti joto na unyevu ndani ya mashine.

Jambo muhimu zaidi ni kuhakikisha unatumia mashine yenye uwezo wa kutunza joto kwa muda wa saa sita mara baada ya umeme kukatika.

 

Viatamishi vya mafuta

Ni muhimu pia kueleza kuwa mbali ya nishati ya umeme, viko vitamishi vinavyoweza kujiendesha kwa kutumia nishati ya mafuta kama ya taa au petrol. Kwa kawaida aina hizi za viatamishi huwa nagharama ndogo.

Kwa Watanzania na hata viwanda vidogo vimekuwa vikitengeneza aina hizi za viatamishi. Ni muhimu kutafuta taarifa za viatamishi hivi kutoka kwa wataalamu wa ufugaji au wafugaji wakubwa.

 

0789063838-Barua pepe [email protected]