Kuachwa huru wafungwa wa kisiasa Ethiopia? Ni maneno kuliko uhalisia

Muktasari:

  • Bwana huyo na mtandao wake wa Blog yuko katika kikundi cha Zone9 ambacho hutangaza maoni huru kuhusu hali ilivyo katika nchi hiyo iliyoko katika Pembe ya Afrika.

Kwanza angalia, halafu ndio uamini”, anasema Mwanablog Suliana Shimeles kuhusu tangazo lililotolewa na Serikali ya Ethiopia kwamba wafungwa wote wa kisiasa wataachiwa huru.

Bwana huyo na mtandao wake wa Blog yuko katika kikundi cha Zone9 ambacho hutangaza maoni huru kuhusu hali ilivyo katika nchi hiyo iliyoko katika Pembe ya Afrika.

Wengi wa wanachama wa kikundi hicho wamewahi kutiwa magerezani. Mwenyewe Shimeles aliikimbia nchi kwa kuhofia hilo.

Kama walivyo wapinzani wengi wa Serikali, Shimeles pia alishangazwa na tangazo hilo lililotolewa mwanzoni mwa mwezi huu na Waziri Mkuu, Hailemariam Desalegn.

“Lakini bado kuna mengi yasiyokuwa wazi”, anasema Shimeles na kuhoji, “Lini jambo hilo litafanyika? Wafungwa wangapi wataachwa huru, na akina nani?”

Hakuna mtu anayejua wafungwa wangapi wa kisiasa walioko Ethiopia na wote wako wapi. Kuna wafungwa ambao kwa miaka mingi hawajasikika na hawajulikani walipo.

Mwaka jana Serikali iliwaacha huru maelfu ya wafungwa ambao walikamatwa baada ya kutokea machafuko makubwa katika majira ya kiangazi ya mwaka jana. Lakini, polisi haijawahi kuzungumzia juu ya kuwapo wafungwa wa kisiasa kama alivyofanya mara hii waziri mkuu. Wanasiasa wa upinzani, waandishi wa habari na wakosoaji wengine wa Serikali mara nyingi walihukumiwa kutokana na makosa ya ugaidi.

Si kila mtu ndani ya Serikali aliyekubaliana na maneno aliyoyatamka Desalegn. Msemaji wa Serikali, Zadiq Abraha, alisema: “hakuna wafungwa wa kisiasa. Lakini, wanachama wengi wa vyama vya kisiasa na watu wengine binafsi wanashukiwa kufanya uhalifu.” Mfungwa wa kisiasa aliye maarufu sana nchini Ethiopia ni Bekele Ger, makamu mkuu wa Chama cha Oromo Federal Congress (OFC), chama cha watu wa kabila kubwa la Oromo nchini Ethiopia. Japokuwa Ethiopia ni nchi ya vyama vingi vya kisiasa, lakini upinzani hauna hata kiti kimoja bungeni. Tangu mwaka 1991 wabunge wote ni wa chama cha zamani cha ukombozi, EPRDF, Chama cha Mapinduzi cha Watu wa Makabila ya Ethiopia pamoja na vyama vingine shirika. Pia, wafungwa wa kisiasa wanaojulikana ni waandishi wa habari wawili, Eskinder Nega na Woubshet Taye ambaye yuko jela tangu 2011.

Pia, cha kushangaza ni ahadi iliyotolewa na Desalegn kwamba gereza kubwa lililoko katikati ya mji mkuu wa Addis Ababa litafungwa. Likijulikana kama Maekelawi ( Central), gereza hilo liko katikati ya mji, baina ya hoteli na kanisa kubwa na linamtisha kila mtu. Wafungwa wa kisiasa uhojiwa ndani ya jela hiyo na pia huteswa. Ahadi ya Desalegn kwamba gereza hilo la Maekelawi litafanywa kuwa jumba la makumbusho limeonekana ni kama kuyatambua makosa ya Serikali. Waziri mkuu huyo anataraji yatafikiwa masikilizano ya kitaifa.

Tangazo la kushangaza la kuachiwa huru wafungwa wa kisiasa limekuja baada ya kufanyika kikao kirefu cha baraza la uongozi la chama tawala na baada ya miaka ya vitendo vya utumiaji nguvu na kuuliwa wananchi wanaojitolea kuandamana. Mamia ya watu walikufa mwaka 2016 pale ilipotokea machafuko makubwa kuonekana tangu Serikali kuingia madarakani mwaka 1991. Maandamano hayo yalitokana na malalamiko ya wananchi kupinga kuibiwa ardhi zao, ukandamizaji unaofanywa na Serikali na malumbano yaliyoko baina ya makundi 10 ya kikabila ya nchi hiyo- athari zinazotokana na maajabu ya uchumi wa Ethiopia ambao tangu kuingia karne hii umekuwa ukipanda kwa kasi- asilimia 10 kila mwaka.

Miundombinu mikubwa kabisa na miradi ya uwekezaji imetekelezwa na mara nyingi watu wamesakwa huku ardhi zao zikichukuliwa ili kujenga viwanda, mabwawa ya kutoa umeme na njia za reli. Si tu Waethiopia wengi wamefukuzwa kutoka makazi yao, lakini pia hawajafaidika na maajabu ya uchumi wa taifa kupanda. Karibu milioni sita kati ya Waethiopia milioni 100 bado wanategemea kupewa msaada wa vyakula kila mwaka. Hasa watu wa makabila ya Oromo na Amhara, makabila mawili makubwa kabisa nchini humo- yote mawili yakiwa ni asilimia 60 ya jumla ya wakazi wa nchi hiyo, ndio wanaoendesha upinzani dhidi ya Serikali ambayo inadhibitiwa na watu wa kabila la Tigray pamoja na viongozi wa zamani wa vita vya misituni, licha ya kwamba Watigray ni asilimia sita tu ya wakazi wote wa Ethiopia.

Swali linaloulizwa ni kama Ethiopia kwa kutangaza kuachiliwa huru wafungwa wake wa kisiasa sasa inachukuwa hatua muhimu kuelekea demokrasia? Mwishowe ni kwamba waziri mkuu Desalegn ambaye ameingia madarakani mwaka 2012 baada ya kufa mtangulizi wake aliyekuwa na ushawishi mkubwa wa kisiasa, Meles Zenawi ambaye hatoki kabila la Tigray. Yeye ni wa kabila la kutokea Kusini mwa Ethiopia. Wanasiasa kama Desalegn hawakamati madaraka ya kweli nchini humo.

Madaraka hasa hushikiliwa na Idara ya Usalama ya nchi. Swali jingine ni kama watu hao wa usalama wako tayari kugawa madaraka yao yasiyokuwa na mipaka?

Watu wasioridhika sana na Serikali ya sasa ya Ethiopia ni wale wa Mkoa wa Oroma. Mji mkuu wa Addis Ababa humo ndani ya mkoa huo. Lakini licha ya hayo, Waoroma wamekuwa na hisia kwamba wanatengwa na watu wa kabila la Tigray ambao wanashikilia nafasi muhimu ndani ya chama tawala cha EPRDF.

Waoromo wanawaona Watigray kuwa ni wakoloni na ambao viongozi wao waliuangusha utawala wa kidikteta wa Mengistu Haile Mariam mwaka 1991.

Tangu uchumi wa Ethiopia ulipoanza kupanda juu kwa viwango vya asilimia 10 na zaidi kwa mwaka, ulanguzi wa biashara ya ardhi umezidi sana.

Kila siku wanahamishwa watu kutoka ardhi zao ili kutoa nafasi ya kujengwa viwanda vya Wachina, kuanzishwa mashamba ya maua, wenyewe wakiwa ni Waholanzi au kufunguliwa mashamba ya kilimo ya Wahindi. Pia, kujenga majumba ya kuishi.

Ili kuepukana na mizozo ya ndani waasi walioshinda kuuangusha utawala wa kikomunisti wa Mengistu Haile Mariam waliunda Serikali ya umoja ambapo yalikuwamo ndani yake makundi yote muhimu ya kikabila.

Zaidi ya hayo ilitakiwa kuweko mfumo wa Serikali ya shirikisho, msingi wake ukiwa mikoa mipya ambayo mipaka yake ilichorwa kwa misingi ya kikabila. Hivyo, ule mfumo wa Serikali moja kuu yenye nguvu ulikomeshwa na makundi mbalimbali ya makabila yakapewa mamlaka makubwa ya mambo ya ndani na kujiamulia yenyewe mambo yao.

Hata hivyo, mara ikawa wazi kwamba Serikali ya Muungano chini ya uongozi wa mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Tigray (TPLF), Meles Zenawi, haikuwa na hamu kubwa ya kugawana madaraka na watu wa makabila mengine. Ile ahadi iliyotolewa mwanzo kwamba mikoa itakuwa na mamlaka ya kujiamulia mambo yao ilibaki kuwa ni maneno matupu tu. Mwishowe ilidhihirika kwamba pale ukabila unapokuwa ndio msingi wa kuijenga dola, basi, bila shaka yeyote, kunazuka mivutano ya kikabila.

Swali ambalo limekuwa likiulizwa hadi karibuni ni: Je, iko hatari kwa Ethiopia kusambaratika. Sifikirii. Kuna njia ya kuepukana na uwezekano huo. Suluhisho ni kuruhusu huko Ethiopia kuwako mfumo wa kweli wa Serikali ya shirikisho. Kwa hivyo Chama cha TPLF kinabidi kiuache umbele wake katika kuhodhi madaraka na kiruhusu kuweko mfumo wa kweli wa vyama vingi vya kisiasa. Hakuna uwezekano wa Ethiopia kumegukameguka kwa vile wananchi wengi wanataka sana kubakia wameungana. Muhimu ni kuweko marekebisho ya kisiasa katika nchi hiyo. Utawala wa EPRDF hauambatani kabisa na hali ya kitamaduni na kisiasa ya nchi hiyo. Nini Ethiopia inachokihitaji sasa ni mkutano wa kitaifa utakaoviweka pamoja katika meza ya majadiliano vyama vya kisiasa na jumuiya zote za kiraia.