Mamilioni CAF Yanga yatumike kuandaa timu, yasiibue mgogoro

Muktasari:

  • Mbali na fedha za shirikisho hilo klabu hiyo kongwe inatarajiwa kuvuna Sh250 milioni zinazotolewa na wadhamini, Kampuni ya SportPesa Tanzania.

Klabu ya Yanga imejihakikishia kuweka kibindoni Dola 275,000 (Sh616 milioni) kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF) baada ya kuitupa nje ya mashindano ya Kombe la Shirikisho, Welaytta Dicha ya Ethiopia.

Mbali na fedha za shirikisho hilo klabu hiyo kongwe inatarajiwa kuvuna Sh250 milioni zinazotolewa na wadhamini, Kampuni ya SportPesa Tanzania.

Licha ya kufungwa bao 1-0 katika mchezo wa marudiano uliochezwa jijini Awassa, Ethiopia, Yanga ilisonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1, baada ya kushinda 2-0 jijini Dar es Salaam.

Kati ya fedha hizo za CAF Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limepata Dola 13,750 (Sh30.8 milioni) ambazo ni mgawo kwa mujibu wa kanuni za shirikisho hilo.

Yanga iliangukia katika Kombe la Shirikisho baada ya kuondolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufungwa jumla ya mabao 2-1 na Township Rollers ya Botswana.

Haikuwa kazi rahisi kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara kupenya kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kutokana na mazingira magumu ya kiuchumi yaliyoikabili msimu huu.

Yanga imepitia kipindi kigumu tangu mwenyekiti wake, Yusuf Manji ambaye alikuwa chachu ya mafanikio katika mashindano mbalimbali yakiwamo ya kimataifa alipojiweka kando.

Manji alikuwa ‘kila kitu’ kwa Yanga na mafanikio ya timu hiyo katika mashindano mengi yalichangiwa na kigogo huyo ambaye aliboresha masilahi ya wachezaji na benchi la ufundi.

Tangu Manji alipojiengua, Yanga imeshiriki Ligi Kuu na mashindano ya kimataifa katika mazingira magumu baada ya kuyumba kiuchumi.

Mishahara kwa wachezaji na benchi la ufundi ilikuwa tatizo kubwa msimu huu, lakini jambo la kufurahisha ni kwamba timu hiyo ilicheza soka kwa kiwango kinachostahili kulingana na mazingira yaliyoizunguka.

Kimsingi wachezaji na benchi la ufundi wanastahili pongezi kwa kufanya kazi katika mazingira magumu, lakini bado timu yao ikaendelea kuwa tishio kwa watani wao wa jadi katika kampeni ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.

Wachezaji walicheza kufa au kupona kuipigania timu yao kuhakikisha inapata matokeo mazuri licha ya kutokuwa na mshahara kwa muda mrefu na wakati mwingine walilipwa kiduchu kupunguza makali ya maisha.

Bila shaka viongozi wa Yanga wameshuhudia vijana wao walivyovuja jasho kuipigania timu hiyo katika mashindano mbalimbali.

Juhudi za wachezaji hao zimeonekana, hivyo ni jukumu lao kuthamini mchango huo kwa kuwapa motisha kupitia fedha za CAF baada ya kufanya kazi nzuri.

Pia, fedha hizo zitumike kuleta morali kwa wachezaji wakati wakijiandaa kwa mechi za hatua ya makundi ambayo ni ngumu zaidi na inayohitaji kujiandaa kikamilifu.

Yanga inatakiwa kutumia fedha hizo kwa uangalifu mkubwa ikitambua kuwa ipo vitani katika mashindano ya kimataifa ni muhimu kujiandaa mapema.

Fedha ni sabuni ya roho, hatutegemei kuona mamilioni hayo yakiibua mzozo ndani ya klabu hiyo, bali yageuke kuwa chache cha kujiimarisha kusonga mbele zaidi.

‘Siasa’ ndani ya klabu hizi kongwe Yanga na Simba zinafahamika suala la fedha mara nyingi limekuwa tatizo kubwa kwa viongozi wasiokuwa waaminifu.

Mara kwa mara tumeshuhudia baadhi ya viongozi wa klabu hizo wakidai wanatoa fedha zao kwa mapenzi binafsi kwa lengo la kusaidia timu, lakini muda mfupi baadaye tunasikia wanadai fedha zao kwa njia isiyokuwa ya kistaarabu.

Tumeshuhudia baadhi ya vigogo wa klabu hizo wakiweka ‘makomandoo’ milangoni katika mechi za Ligi Kuu wakidai sehemu ya mapato katika mchezo husika.

Ni ukweli usiopingika kuwa baadhi ya vigogo walitoa fedha zao kutoka mifukoni kuisaidia katika mashindano mbalimbali, hilo ni jambo jema.

Lakini bila shaka hilo lilikuwa kwa makubaliano baina ya pande hizo mbili, hivyo ni vyema wakati wa kurejesha fedha hizo kuwe na ukweli, uwazi ili kuepuka manung’uniko.

Kila upande upate haki stahiki kulingana na makubaliano yao ambayo kimsingi tunatarajia yalikuwa ya maandishi ili kuepuka mgogoro usiokuwa na lazima.

Yanga ina jukumu kubwa mbele yao katika maandalizi ya kujiandaa na mchezo wa hatua ya makundi dhidi ya USMA Algiers ya Algeria. Timu nyingine zilizopangwa Kundi D ni Gor Mahia ya Kenya na Rayon Sports ya Rwanda.

Timu hiyo isidhani kuwa imepangwa kundi ‘laini’, hakuna timu nyepesi, zote zilizofuzu ni ngumu kwa hiyo maandalizi ya mapema muhimu.