Mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida

Muktasari:

  • Umeme huo wenye tabia ya kipekee, huweza kutolewa katika kiwango maalumu kinachowezesha misuli ya moyo kudunda na kutoa mapigo yenye mpangilio sawa na yenye ufanisi pasipo kudunda ovyo ovyo.

Moyo wenye afya njema huweza kutoa mapigo yake katika mpangilio sawa ukiratibiwa na uwapo wa mpitisho wa nguvu wa msukumo wa umeme wa moyo.

Umeme huo wenye tabia ya kipekee, huweza kutolewa katika kiwango maalumu kinachowezesha misuli ya moyo kudunda na kutoa mapigo yenye mpangilio sawa na yenye ufanisi pasipo kudunda ovyo ovyo.

Mapigo ya moyo kwenda bila mpangilio na uwapo wa dosari ya upitishwaji wa umeme wa moyo, husababishwa na tatizo la uzalishaji au upitishawaji wa umeme huo.

Hata hivyo, kukua kwa maendeleo ya kisayansi katika fani ya tiba kumesaidia kwa kiasi kikubwa kuokoa wagonjwa wanaougua maradhi ya moyo, ikiwamo kasoro ya mapigo ya moyo ambayo kitabibu hujulikana Arryhthmia.

Maendeleo hayo ndiyo yamechangia kutengenezwa kwa mashine iitwayo Pacemaker inayopandikizwa mwilini kusaidia kuzalisha umeme wa moyo.

Uzalishaji wa umeme huo husaidia kurekebisha athari ya mfumo wa umeme wa moyo.

Mtu maarufu ambaye amepachikwa mashine hiyo ya pacemaker kifuani kwa zaidi ya miaka 10 sasa, ni kocha aliyewahi kuifundisha klabu ya soka ya nchini Uingereza, Manchester United, Sir Alex Furgerson.

Mashine hii ndiyo inamfanya kuendelea kuishi bila kupata mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida.

Mashine hii pia ndiyo mbadala wa kituo cha uzalishaji umeme wa moyo kwa ajili ya kuwezesha kuwapo kwa mapigo ya moyo yasiyo na hitilafu.

Umeme wa moyo

Moyo umeumbwa ukiwa na umeme wake wa asilia unaopita kwenye nyaya maalumu ambazo zimejitandaza kwenye misuli ya chemba za moyo.

Mfumo huu wa umeme ndiyo unauwezesha kudunda na kutoa mapigo yanayosukuma damu kwenda maeneo mbalimbali mwilini.

Chanzo cha Tatizo la mapigo ya moyo

Tatizo lolote katika mfumo wa umeme wa moyo na misuli ya chemba zake inayoletwa na maradhi mbalimbali ya moyo, huweza kuathiri udundaji wa mapigo yake.

Sababu kubwa ya kutokea tatizo hilo ni kuingiliwa na mfumo mzima wa usambazaji wa umeme wa moyo. Maradhi yanayoweza kusababisha hali hiyo kutokea ni pamoja na ya misuli ya moyo, mtu kuzaliwa akiwa na ugonjwa wa moyo, shinikizo la damu, homa, matumizi ya tumbaku, ulevi wa kupindukia, shambulizi la moyo au kama mtu alishafanyiwa upasuaji wa moyo.

Mambo mengine yanayoweza kuchangia ni utumiaji wa vinywaji vyenye caffein, matibabu ya dawa kama kwinini na za pumu aina ya Aminophiline na kutowiana kwa chumvichumvi na maji mwilini.

Vile vile, utumiaji wa dawa za kulevya na matatizo ya tezi inayozalisha homoni zinazochangia ukuaji wa mwili. Wakati mwingine chanzo cha tatizo kinaweza kisugundulike moja kwa moja. Tatizo la mapigo ya moyo linaweza pia kusababisha mapigo yake kuwa na kasi ya juu, au kuwa na kasi ndogo au kutolewa bila mpangilio.

Moyo una misuli inayofanya kazi ya kujikunja na kukunjuka ili kusukuma damu mwilini. Kila pigo moja la moyo huzalisha mtiririko wa haraka wa mapigo makuu mawili ya misuli ya chemba za moyo.

Kwa kawaida moyo una chemba nne, juu ziko mbili na chini mbili, chemba hizi, misuli yake ndiyo hutoa mapigo kwa ajili yakusukuma damu.

Pigo la kwanza la moyo hutokea kwenye chemba za juu, yaani Atria, wakatika pigo la pili kusukuma damu hutokea katika chemba za chini ziitwazo ventricles.

Chemba za juu hupokea damu inayoingia kwenye moyo na kuisukuma kwenda chemba za chini zinazopokea damu hiyo na kuisukuma kutoka ndani ya moyo kwenda kwenye mapafu na sehemu nyingine mwilini.

Kwa kawaida, mapigo ya moyo hudhibitiwa na nguvu ya msukumo wa umeme. Katika hali ya kawaida, nguvu ya msukumo wenye umeme hutolewa na kitu kilichopo kiasili kwenye moyo kiitwacho Sinus node, kilichopo upande wa kulia wa moyo kwenye chemba ya juu.

Sinus node ni sawa na mashine ya Pacemaker ambacho mwanadamu amekitengeneza kutatua tatizo la mfumo wa umeme wa moyo. Mawimbi yenye nguvu ya msukumo wa umeme huzalishwa kwa kila pigo la moyo katika Sinus node na mawimbi hayo ndiyo yanawezesha kutoa ishara kutokea kwa mkunjuko wa misuli ya moyo.

Baada ya mawimbi, msukumo wa kuwezesha kutoa mapigo katika chemba za juu, husafirishwa na huweza kufika na kutulia kwa muda mfupi katika kituo kingine cha moyo kiitwacho AV node, kilichopo sehemu ya juu ya ukuta unaotenganisha chemba mbili za chini.

Kutulia huko ndiko kunatoa nafasi kwa damu kumiminika kutoka chemba za juu kwenda chemba za chini.

Hivyo basi, mawimbi ya nguvu ya msukumo huweza kwenda chini kwenye chemba mbili za chini na kusababisha zao la mkunjuko wa misuli ya chemba za chini, hivyo msukumo wa pili hutokea na damu husukumwa kutoka kwenye vyumba hivyo.

Madhara gani yanaweza kutokea

Mapigo ya moyo yanapoenda kwa kasi isiyo ya kawaida, inaweza kusababisha damu kutosukumwa kwa ufanisi katika maeneo ya mwili mzima.

Hali hii inaweza kuchangia ogani na tishu za mwilini kukosa hewa ya oksijeni ikiwamo sehemu nyeti za mwili, misuli ya moyo na ubongo kukosa damu.

Hivyo kusababisha maeneo hayo kushindwa kufanya kazi. Madhara makubwa yanayoweza kujitokeza ni pamoja na moyo kushindwa kufanya kazi, shambulizi la moyo, kiharusi na kifo cha ghafla.

Halii hii inaweza kuleta dalili mbalimbali ikiwamo kizunguzungu, kukatika pumzi au kupumua kwa shida, kichwa kuuma na kuona nyota nyota, kuhisi mapigo ya moyo yako juu na kudunda vibaya, kifua kuuma na kupoteza fahamu.

Ingawa si mara zote wenye tatizo la mapigo ya moyo huwa na dalili za wazi, mara zingine hugundulika na matatizo haya pale anapokuwa katika uchunguzi wa kawaida.

Nini cha kufanya

Tatizo linapopata matibabu ya uhakika, mara chache linaweza kuhatarisha maisha. Hata madhara yake pamoja kuwa ni makali, lakini yanazuilika kwa matibabu.

Vipimo muhimu ambavyo hufanyika ni pamoja na cha ECG na ECHO ambavyo huweza kubaini matatizo mbalimbali ya moyo.

Matibabu hutegemeana na bainisho la aina ya mapigo ya moyo yasiyo yakawaida. Mgonjwa anaweza kutohitaji kutumia dawa au kutumia dawa za kurekebisha dosari ya mapigo yasiyo kuwa ya kawaida, njia ya upasuaji na kubadili mitindo na mienendo ya kimaisha.

Kwa upande wa matibabu ya hitilafu ya uzalishaji umeme, mashine ya pacemaker inaweza kupandikizwa kwa njia ya upasuaji chini ya ngozi maeneo ya kifuani au tumboni ili kusaidia kurekebisha hitilafu ya umeme katika moyo.

Mashine hii inatoa umeme mdogo usio na nguvu kubwa pale inapohisi umeme au mapigo ya moyo hayako sawa. Mashine hii hupendekezwa na madaktari wa moyo kuwekewa mtu mwenye tatizo la kutoa mapigo ya moyo yenye kasi ndogo, kwa kawaida kasi ya mapigo kwa mtu aliyetulia ni kati ya 60-100 kwa dakika.

Pia, inapendekezwa kutumika kwa mgonjwa mwenye kizuizi cha mpitisho wa umeme wa moyo, tatizo linalotokana na kuingiliwa utiririkaji wa umeme wakati unaposambaa au umeme kuwa mdogo. Kuna aina nyingine ya mashine inayopandikizwa kwa upasuaji ijulikanayo kama Implantable Cardioverter defibrillator(ICD) inayotumika kutatua aina ya mapigo yasiyoyakawaida na ni hatari.

Aina hiyo ya mapigo yasiyo yakawaida husababisha chemba za chini kutoa mapigo ya kasi. Mashine ya ICD huweza kubaini tatizo na kutoa shoti ya umeme katika misuli ya moyo ya chemba za chini na kusahihisha tatizo hilo na mapigo kurudi katika hali yake ya kawaida.

Matibabu mengine ili kurekebisha hitilifu ya mapigo ya moyo ni pamoja na Catheter Ablation inayotumika kutatua aina ya mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida kwenye chemba za juu.

Njia hii huwa na mrija ulio kama waya huingizwa kwenye mishipa ya damu ya miguuni na kufika katika moyo ambao hutoa mawimbi yenye nguvu ya umeme ili kurekebisha hitilafu ya mapigo ya moyo. Ili kuzuia matatizo haya, inashauriwa kuepuka mambo hatarishi yanayochangia kutokea kwa magonjwa ya moyo ikiwamo udhibiti wa uzito wa mwili, matumizi ya tumbaku, unywaji wa pombe kupita kiasi na matumizi ya dawa za kulevya.

Zingatia kula vyakula visivyo na mafuta mabaya, kula zaidi mboga za majani, matunda na wanga isiyokobolewa na fanya mazoezi mara kwa mara. Inashauriwa kufanya uchunguzi wa afya ya moyo mara kwa mara angalau mara moja baada ya miezi sita ili kubaini matatizo mapema kabla ya kuleta madhara.