Masilahi ya wazee yapewe uzito unaostahili

Muktasari:

  • Licha ya baadhi ya watu kwenye jamii zetu kuwaona ni mzigo au tegemezi, kundi hili lina umuhimu wake hasa pale linapohusishwa katika mipango mbalimbali ya maendeleo sanjari na kusimamia ustawi wao.

Wazee ni kundi muhimu katika jamii yoyote ile duniani. Pamoja na changamoto za umri, wazee wameendelea kuwa walezi na wasimamizi wa familia.

Licha ya baadhi ya watu kwenye jamii zetu kuwaona ni mzigo au tegemezi, kundi hili lina umuhimu wake hasa pale linapohusishwa katika mipango mbalimbali ya maendeleo sanjari na kusimamia ustawi wao.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, Tanzania ina wazee milioni 2.5 (sawa na asilimia 5.6 ya idadi ya watu wote). Idadi hii ni kubwa na inaongezeka.

Mara nyingi linapotajwa neno “wazee” wengi wetu tumekuwa na fikra potofu juu yao - tunawapuuza kutokana na kupungua kwa ufanisi wao katika utendaji kazi. Pengine inaweza isiwe kweli.

Tafsiri sahihi ya mzee ni mtu yeyote mwenye umri wa kuanzia miaka 60 na kuendelea. Kuwa mzee haina maana umuhimu wake umepungua. Wapo ambao wako imara na wameweza kufanya mambo ambayo rika la vijana hawajayafanya.

Ni fikra zetu za kuwapuuza na kubeza jitihada zao za maendeleo ndizo zinawafanya kukosa nguvu na kuendelea kubaki chini kiuchumi. Hii ni moja ya changamoto ambayo wazee wanakumbana nayo kila siku.

Pamoja na changamoto za umri, rika la watu wenye umri mkubwa bado lina mchango mkubwa katika kuliletea Taifa maendeleo.

Hili linaweza kuwa katika kushauri, kusimamia pamoja na kuongoza jamii kutokana na uzoefu wao.

Hata hivyo kutokana na kutopewa uzito unaostahili, wazee wamezidi kuonekana duni na tegemezi, hali inayokwamisha ushiriki wao katika shughuli za maendeleo.

Ni ukweli usiopingika kuwa wazee wanakumbana na changamoto lukuki za kijamii ikiwamo mauaji, kiafya pamoja na umaskini unaotokana na kushuka kwa nguvu ya uzalishaji.

Moja ya sekta muhimu inayogusa ustawi wa wazee ni afya. Ni dhahiri kuwa wazee wanahitaji huduma za afya za uhakika na bora zinazoendana na hali zao kiuchumi.

Naipongeza Serikali kwa kuja na mpango wa matibabu bure kwa wazee unaolenga kuwatambua katika kila halmashauri nchini na kuwapa vitambulisho maalumu vya matibabu bila malipo.

Mpango huu umeokoa wazee wengi ikiwa ni pamoja na kupunguza mzigo wa gharama kwa familia nyingi.

Hata hivyo, ripoti mbalimbali zimekuwa zikieleza malalamiko ya wazee juu ya tatizo la ukosefu wa dawa hospitalini, jambo linalohatarisha ustawi wao.

Takwimu zinaonyesha asilimia 96 ya wazee nchini hawana pensheni ya uzeeni, hali inayowafanya kushindwa kugharamia huduma za msingi ikiwamo afya.

Changamoto hii inapaswa kupewa uzito wa kutosha ili kupata suluhu ya haraka kwa kuwa wazee wengi wanaishi katika lindi la umaskini.

Mbali na hilo, kuna changamoto ya ukosefu wa sheria ya wazee kwa muda mrefu sasa. Kwa sasa ipo Sera ya Wazee ya mwaka 2003 ambayo kwa miaka 15 bado haijatungiwa sheria.

Ni wazee hawa wamekuwa wakilalalamikia ukosefu wa sheria itakayosimamia masilahi yao pamoja na masuala mengine ya msingi.

Serikali imekuwa ikiahidi juu ya utekelezaji wake na mwaka huu imeahidi kuwa hadi ifikapo Juni, 2019 sheria itapatikana. Ni hatua nzuri lakini inahitaji utekelezaji ili kunusuru masilahi ya wazee nchini.

Kuna mambo mengi yamewezekana kutekelezeka baada ya Serikali na wadau kuungana pamoja na kutafuta suluhu. Hili la wazee nalo linawezekana. Hivyo ni rai yangu waliokabidhiwa madaraka nchini walione hili na kulishughulikia ipasavyo.