Matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii ina athari kisaikolojia

Muktasari:

  • Majibu ya uchunguzi uliofanywa kwenye baadhi ya mitandao ya kijamii ikiwamo ya kama Facebook, Instagram, snapchart na Whatsaap.

Kama ulifikiri kuandika au kutuma picha za kuelezea hisia zako katika mitandao ya kijamii ili upate amani ya moyo kwa kuwa umepitia magumu kwa kukerwa na watu, hiyo siyo njia sahihi wataalamu wa saikolojia wanasema.

Majibu ya uchunguzi uliofanywa kwenye baadhi ya mitandao ya kijamii ikiwamo ya kama Facebook, Instagram, snapchart na Whatsaap.

Imeonekana vijana na watu wengi ambao ni waumini wa mitandao hiyo huelezea mambo yao hasa zile yahusuyo faragha zao au za watu wa karibu yao.

Kwa mujibu wa mtandao wa Facebook, watu zaidi ya 1.28 bilioni wanautumia kila siku.

Hii imeelezwa baada ya ripoti iliyotolewa mapema Machi, mwaka huu.

Dunia sasa imehamia viganjani, ndiyo usemi unaotamalaki mitaani kwa sababu muda mwingi simu za watu zimekua msaada mkubwa kwa mawasiliano hasa katika ulimwengu wa mitandao ambao watu wanapata fursa za kubadilishana mawazo tofauti na awali, wengi walikuwa wakikutana kwa wauza kahawa na mafundi viatu.

Sufiani Rajabu (23), anasema amekuwa akitumia mitandao ya kijamii mara kadhaa na hasa wa facebook, kuandika na kuelezea hisia zake, akidai kuwa muda mwingi hushinda pekee yake akifanya shughuli zake.

“Kaka mimi nikiandika ndiyo naona kama napunguza jazba na pia najihisi kama nimetua mzigo wa matatizo, na maoni ninayoyapata mengine yananijenga lakini mengi ni yananiponda na kunisononesha,” anasema Rajabu.

Kijana mwingine, Mohamed Miraji anasema hafikirii kuanika mambo yake ya faragha kwenye mitandao kwani kufanya hivyo hakuwezi kumpatia mtu majibu sahihi ya kumaliza matatizo yanayomkabili.

“Kwa mfano mtu kama mwanaume , kuanika matatizo yako mitandaoni ni sawa na kujishushia heshima yake ya kiuanaume, waache,” anasema Miraji.

Joyce Michael, mkazi wa jijini Dar es Salaam anasema simu zimesababisha kutokuwa karibu na watu, kitu ambacho kinasababisha wengi kuamua kutumia mitandao kusaka majibu ya matatizo yao, bila kujua kuwa wanajiathiri kisaikolojia.

Lakini dawa si hiyo, bali wengi wao ndiyo hujiongezea matatizo ya kupatwa msongo wa mawazo.

“Na hali hii tunaishuhudia zaidi kwa wale wanaojiona ni mastaa, hawa wameharibu utaratibu kwani kila wanachofanya wanaweka mitandaoni kitu ambacho vijana na watu wengi wanaiga kutoka kwao,”anasema Michael.

Mwanafunzi wa chuo cha Habari TSJ, ambaye hakutaka jina lake litajwe anasema aliwahi kuandika jambo liloelezea hisia zake mtandaoni, lakini alijikuta akipoteza fursa ya ajira kwenye kampuni moja iliyokuwa ikimfuatilia kwa karibu kutaka kumuajiri.

“Sitorudia tena, sikuwa najua nini ninakifanya katika mitandao, ilikuwa mtu akinikwaza natumia mitandao kama njia ya kumjibu na kuandika chochote ninachojisikia bila kujua athari zake za baadaye,” anasema kijana huyo.

Wataalamu wa saikolojia wanasemaje kuhusiana na hatua hiyo?

Charles Nduku ni mtaalamu wa saikolojia, anasema mitandao ya kijamii inatumika kinyume na malengo yake.

Anasema badala ya watu kuitumia kwa ajili ya kupashana habari na taarifa mbalimbali za kujenga jamii, imegeuka kuwa uwanja wa matusi na mambo ya ajabu yanayofanywa na vijana wengi nchini.

Anasema mbali na kuanika mambo yake katika hadhara inayotumia mitandao hiyo yenye wafuasi wengi bado wanatamani vitu ambavyo wanavikuta suala ambalo linachangia kumomonyoka kwa maadili hasa jamii za kiafrika.

Nduku alienda mbali na kusema hata fursa za kazi na mambo mengine kwa vijana itabaki kuwa ndoto kutokana na kile ambacho mtu atakuwa amekituma au kuandika katika mitandao hiyo.

“Mtu hawezi kukupa fursa ya ajira au nafasi ya kufanya jambo lake mara atakapobaini ulichoandika katika ukurasa wa mtandao wako ni ukiukaji wa maadili.

Kwenye upande wa ajira, waajiri siku hizi huangalia tabia ya mtu pia kupitia kwenye mitandao yake ya kijamii,” anasema.

Nduku anasema jamii inaweza kukupa heshima ila kupitia mambo ambayo hayastahili kuwekwa katika mitandao, inaweza kushusha heshima yako kwa sababu unatoa mwanya wa watu kukujadili kwa mema na mabaya.

Anasema matatizo ya kuelezea hisia hayawezi kutatuliwa katika mitandao, bali kwa kupitia wataalamu wa saikolojia ambao wanaweza kukupa msaada wa karibu.

Karoli Mabula, pia ni mtaalamu wa saikolojia anasema kuandika kitu ambacho kimekukwaza kwa namna yoyote ni moja ya tiba ya kutibu dukuduku ambalo linakusumbua, haijalishi ni katika mazingira gani.

Kwanini watu wanaamua kuanika siri zao kwenye mitandao?

Mabula anasema wengi wao hukosa watu waaminifu wanaoweza kuwaambia mambo yao na wakayatunza bila kuyatoa kwa mtu mwingine.

“Sasa hali hiyo inawafanya wengi waone suluhu ni kuandika kwenye kurasa zao za mitandao, jambo ambalo si ufumbuzi,” anasema.

Anasema maandiko yanayoandikwa kwenye kurasa wake na watu, mara nyingi hayamsaidii bali huchangia kumuingiza kwenye matatizo zaidi.

“Hakuna faida wala uhusiano wowote wa kuandika au kuelezea hisia zako mitandaoni na kutafuta suluhu ya tatizo hilo, na kumbuka si watu wote wanaweza kukuelewa kwa kile unachokifanya, lakini mtu akienda kwa washauri nasihi, watapata tiba ya matatizo yanayowasibu,” anasema Mabula na kuongeza: “Watu wengi wanaugua maradhi ya sonona, lakini badala ya kutafuta tiba kwa wataalamu, wanakimbilia kwenye mitandao ambako wanajikuta wakishusa thamani yao.

Tukumbuke thamani ya mtu inashuka kwa kitu kidogo sana, ndiyo maana vijana na watumiaji wa mitandao wanapaswa kuwa makini kwa wanachoandika kwani kuna wafuasi wengi ambao pia wanaweza kushusha heshima yao katika jamii.”

Lakini pia anasema si mitandao hiyo inalenga mambo hasi tu, wapo baadhi wanayoitumia kwa malengo chanya, wanafanikiwa kimaisha.