MAONI: Mawaziri wazingatie Hapa Kazi Tu

Mwishoni mwa wiki, Rais John Magufuli alifanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri kwa kuwaondoa wawili na kuwateua wengine.

Mawaziri walioondolewa kwenye baraza hilo la mawaziri ni Dk Charles Tizeba wa Kilimo na Charles Mwijage wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Mabadiliko hayo yamefanyika katikati ya mgogoro wa ununuzi wa korosho kutoka kwa wakulima wa mikoa ya Lindi na Mtwara.

Jana mara baada ya kuwaapisha mawaziri wapya, Rais Magufuli alitoa maelezo ya kina juu ya sababu za kuondolewa kwa wale aliowaacha, lakini kwa kifupi kulichochewa na wao kushindwa kutatua mgogoro huo uliosababishwa na wao kushindwa kutatua changamoto kadhaa katika wizara zao na hivyo kumfanya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kulazimika kuingilia kati.

Mojawapo ya changamoto hizo ni mgogoro wa bei ya korosho ambao Serikali ilitangaza inunuliwe kwa Sh3,000 lakini wanunuzi walisusa na mawaziri hao kushindwa kumaliza mgogoro huo kulikochangiwa pengine na mazoea kwamba suala la kutafuta masoko si la mawaziri, bali nguvu ya soko au kwamba hiyo ni kazi ya vyama vya ushirika na Bodi ya Korosho. Pengine ni mazoea kwamba masuala yanayohitaji uamuzi mgumu husubiri maelekezo kutoka juu.

Kutokana na hali hiyo mawaziri wakajikuta wameingia katika mtego wa kushindwa kuwasaidia wakulima.

Rais Magufuli katika hotuba yake jana, aliweka wazi kwamba mawaziri wawili hao walishindwa kuonyesha uwezo wao sawa na walivyoshindwa katika suala la kahawa mkoani Kagera.

Katika sakata la utoroshaji wa kahawa ya Tanzania kwenda nchi jirani, ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyekwenda kutoa maelekezo mazito ya kuzuia. Aidha, katika ununuzi wa korosho ni waziri mkuu aliyetafuta ufumbuzi wa awali.

Ijumaa iliyopoita, Majaliwa aliwapa wanunuzi siku nne kwamba kufikia jana saa 10:00 alasiri wawe wamejiorodhesha na kutaja kiasi cha korosho watakachonunua. Lakini jana hiyohiyo Rais Magufuli alitoa utaratibu mwingine wa Serikali kununua.

Hatuwapi pole mawaziri hao kwa sababu kuteuliwa na kuondolewa ni utaratibu wa kawaida katika utumishi. Katika nafasi zao wamewahi kuwepo wengine – walihudumu hadi kustaafu au uteuzi wao ulitenguliwa – na sasa ni wabunge wa kawaida au wamestaafu.

Pia, hatuwapi pole kwa sababu hawakutenda dhambi, bali wanarudi kufanya kazi hasa ya ubunge ya kuwasilisha kero za wananchi ili zitatuliwe na Serikali.

Hata hivyo, kwa namna ambavyo Rais Magufuli ameelezea sababu za kuondolewa kwao, inafaa liwe fundisho kwa wabunge wengine wanaoteuliwa nafasi ya uwaziri kwamba si fursa ya kubweteka.

Kinachohitajika kama inavyosema kaulimbiu ya “Hapa Kazi Tu” ni utendaji uliotukuka na siyo porojo au blablaa. Wateule wanapaswa kwenda sambamba na matakwa ya awamu husika ndiyo maana Magufuli aliwaonya wateule hao wasifanye sherehe kujipongeza kwa kuteuliwa kwao maana wanaweza kuondolewa wakati wowote.

Tunawasihi wateule wote wa Rais kwamba Hapa Kazi Tu ni kaulimbiu ya utumishi wakati wote wa kutatua kero, shida na kuondoa migogoro kwa kasi, hekima, heshima na kujali haki za binadamu.