#WC2018: Ufaransa, Croatia ubaya ubaya tu

Muktasari:

  • Mechi hiyo kali inayotarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Luzhniki mjini Moscow, itaamua nani bingwa kati ya Ufaransa ya akina Kylian Mbappe, Paul Pogba na Antoine Griezmann au Croatia yenye nyota Luka Modric, Ivan Ivan Rakitic na Mario Mandzukic.

Moscow, Russia. Hatimaye leo baada ya saa 12 jioni, mzizi wa fitina utakatwa, baada ya mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia 2018 kati ya Ufaransa na Croatia.

Mechi hiyo kali inayotarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Luzhniki mjini Moscow, itaamua nani bingwa kati ya Ufaransa ya akina Kylian Mbappe, Paul Pogba na Antoine Griezmann au Croatia yenye nyota Luka Modric, Ivan Ivan Rakitic na Mario Mandzukic.

Wengi wanajiuliza kama Croatia iliyoiduwaza dunia kwa kutoka nyuma na kuilaza England mabao 2-1, katika mechi ya nusu fainali, itaendelea kuonyesha maajabu.

Timu hizo zinatumia mfumo mmoja, kama ilivyokuwa kwa Croatia, Ufaransa inatumia mfumo wa 4-3-3 na imeonyesha kuwa na kikosi imara ikiwa haijapoteza mechi huku kipa, Hugo Lloris akionekana imara langoni.

Croatia

Kwa upande wa Croatia, mbali na kuonyesha uwezo wa kucheza kitimu, pia inategemea uwezo binafsi wa kipa Daniel Subasic, ambaye ameonyesha umahiri katika milingoti mitatu.

Subasic (33) aliyeitumikia Croatia katika mechi 43 pia akitamba katika kikosi cha Monaco ya Ufaransa, anabebwa na urefu wake wa futi sita na inchi tatu.

Hata hivyo, shughuli pevu itakuwa katikati ya uwanja ambapo ‘mafundi’ wanne wataonyesha umahiri wao wa kutawala dimba la kati akina Pogba na Kante wa Ufaransa na upande wa pili watakuwepo Modric na Rakitic.

Eneo hilo kwa kiasi kikubwa ndilo lililotoa mchango mkubwa kuzifikisha timu hizo katika fainali kutokana na kuimarisha ulinzi na kuanzisha mashambulizi.

Viungo wa Croatia, Marcelo Brozovic, Modric na Rakitic wametia fora katika kuchezesha na kuipa nafasi ya kuongoza kati ya timu zote zilizoshiriki fainali hizo za 21 za Kombe la Dunia kwa upigaji wa pasi.

Tangu kuanza fainali hizo Juni 14, 2018 hadi mechi za nusu fainali, Croatia inaongoza kwa kupiga pasi nyingi 3,291 huku sahihi zikiwa 2,660.

Wakati Croatia ikipiga pasi hizo, Ufaransa nayo haikuwa nyuma hadi nusu fainali imepiga pasi 2,769 na kati ya hizo 2295 zilifika kwa usahihi.

Croatia imepiga mashuti 99 langoni mwa wapinzani wakati Ufaransa inayocheza mfumo wa kushambulia kwa kushitukiza imepiga mashuti 74.

Ufaransa inajivunia pia kipa Lloris,31, anayetamba na Tottenham ya England.

Lloris ambaye ni nahodha wa Ufaransa analindwa vyema na ukuta mgumu unaoundwa na mabeki Benjamin Pavard, Raphael Varane, Samuel Umtiti na Lucas Hernandez.

Ikumbukwe kuwa Pavard beki wa kulia ndiye aliyemdhibiti Lionel Messi kwa kiasi kikubwa hatua iliyoiwezesha Ufaransa kuibuka na ushindi wa mabao 4-3 na kutinga nusu fainali na baadaye kuifunga Ubelgiji na kufuzu fainali.

Ufaransa inajivunia kasi ya kinda wake Kylian Mbappe ambaye licha ya kukosa uzoefu amekuwa tishio kwa mabeki wa timu pinzani.

Mbappe ni mtulivu anapoingia ndani ya eneo la hatari jambo linalosababisha kuchezewa rafu na kumpa mwanya Griezmann kupachika mabao kwa mipira ya adhabu.

Croatia hadi inafika fainali, imefunga mabao 12 wakati Ufaransa imefunga mabao 10, imecheza rafu 99 wakati Ufaransa 74, pia imeonyeshwa kadi 14 za njano dhidi ya 10 za wapinzani wao. Rekodi hiyo inaonyesha kwamba timu zote hazina nidhamu nzuri.

Vikosi:

Ufaransa 4-3-3: Hugo Lloris, Benjamin Pavard, Raphael Varane, Samuel Umtiti, Lucas Hernandez, Paul Pogba, N’golo Kante, Kylian Mbappe, Antoine Griezmann, Blaise Matuidi na Olivier Giroud.

Croatia 4-3-3: Danijel Subasic, Sime Vrsajlko, Dejan Lovren, Domagoj Vida, Ivan Strinic, Luka Modric, Marcelo Brozovic, Ivan Rakitic, Ivan Perisic, Mario Mandzukic na Ante Rebic.